Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Diwani wa Chadema amtetea wa CCM kortini

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
DIWANI wa Kata ya Mabogini, Moshi Vijijini, Albert Msando (Chadema) jana alikuwa kivutio mahakamani baada ya kujitokeza na kumtetea Diwani wa Kata ya Machame wilayani Hai, Rajab Nkya (CCM) anayeshitakiwa kwa uhujumu uchumi.

Katika baadhi ya maeneo mkoani Kilimanjaro, ni nadra kwa mfuasi wa Chadema kumtetea mwenzake wa CCM, kufuatia uhasama wa kisiasa uliopo. Msando ni wakili wa kujitegemea na miongoni mwa mawakili wanaoitetea Chadema na wafuasi wake katika kesi mbalimbali.

Diwani huyo ndiye ambaye CCM inamnyooshea kidole kuwa aliihujumu  katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai na kuiwezesha Chadema kuchukua nafasi hiyo.

Hata hivyo yeye binafsi, mara kadhaa amekanusha madai hayo.Wakili huyo ndiye anayemtetea pia Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Justine Salakana ambaye amekwama kulipa Sh10 milioni za dhamana.

Msando ndiye anayemtetea Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe katika kesi kuhusu tuhuma za kumpiga makofi, Nassir Othman wakati wa kupiga na kuhesabu kura wilayani Hai, katika uchaguzi mkuu wa  Oktoba mwaka jana.

Kesi hiyo nayo ilitajwa jana katika mahakama ya Wilaya ya Hai, lakini iliahirishwa kwa kuwa Mbowe hakwenda mahakamani kwa sababu alikuwa na udhuru.

Jana Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) alikuwa asomewe maelezo ya awali katika kesi hiyo.Kesi ya diwani huyo wa CCM anayeshtakiwa pamoja na wenzake wawili ilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Denis Mpelembwa.

Hata hivyo iliahirishwa  hadi Mei 5 mwaka huu.
Mapema, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Anneth Mavika, aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba ipange siku ya kuwasomea watuhumiwa maelezo ya awali.

Diwani Nkya ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Nkuu, anashtakiwa pamoja na Katibu wa chama hicho, Esther Shoo na mfanyabiashara Awadhi Lema.

Mfanyabiashara huyo anakabiliwa na tuhuma za kukiuuzia chama hicho, trekta lililochakaa.
Inadaiwa kuwa kati ya Machi na Oktoba mwaka 2007, washtakiwa walikisababishia chama hicho hasara ya Sh38 milioni kwa kununua trekta hilo.

Takukuru ilidai kuwa kitendo kilichofanywa na washitakiwa hao ni matumizi mabaya ya ofisi.

0 comments

Post a Comment