Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovic Etouh |
Onyo hilo la Utouh, limekuja siku chache baada ya ripoti ya ofisi yake inayoishia Juni 30, 2010 kuvianika vyama sita, ambavyo vimetumia Sh17.14 bilioni bila kuwasilisha mahesabu kwa wakati.
Akizungumza na Mwananchi, Dar es Salaam, jana Utouh alisema: "Sitashughulika na vyama, nitashughulika na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Huwa sishughuliki na ‘individual’ (mtu mmoja mmoja)."
Vyama vyenye wawakilishi bungeni na vinavyopata ruzuku ni CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP.
Katika hesabu za kawaida kuhusu fedha hizo, chama tawala, CCM kitakuwa kimepata mgawo wa Sh12 bilioni kwa kuwa kinapata asilimia 70.
CUF kinachopata asilimia 20 ya ruzuku kitakuwa kimepata mgawo wa Sh3.43 bilioni, Chadema chenye asilimia nane Sh1.37 bilioni na vyama vitatu vinavyoshikilia asilimia mbili Sh343 milioni.
Utouh alisema kwa mujibu wa utaratibu, baada ya kuanza mchakato wa ukaguzi, wahusika wanapewa siku 180 kwa ajili ya kukamilisha taratibu husika.
"Kwa hiyo baada ya miezi sita, kama hakutakuwa na utekelezaji, kitakachofuata ni taratibu tu za kisheria. Ofisi ya Msajili itapaswa kujieleza kwenye Kamati ya Bunge," alisema.
Alisema kitakachofanyika ni sawa na kinachofanyika sasa kwenye Baraza la Sekretarieti ya Maadili ambako watu waliokaidi taratibu wamekuwa wakiona cha moto.
Utouh alisema hatakuwa na simile kwa chama chochote cha siasa ambacho kitakuwa kimeshindwa kufuata taratibu kwani Sheria ya Matumizi ya Fedha inawabana.
"Sitaogopa chama chochote cha siasa, kitakachofuata ni sheria tu. Lakini ni mapema mno pia kuanza kusema ninapendekeza hatua zipi zichukuliwe kwani muda bado wanao. Naomba tu tuwe wavumulivu," alisisitiza Utouh.
Mbatia: Ripoti iko kwa Msajili
Akizungumzia ripoti hiyo jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alionyesha kuchukizwa kutokana na kile alichokiita kutokuwepo ushirikiano miongoni mwa ofisi za Serikali.
Mbatia alisema chama chake kilikwishawasilisha taarifa zake tangu Januari 4, mwaka huu: “Inakera sana, kuonyesha sisi ni mafisadi tunakula kodi za wananchi."
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, NCCR-Mageuzi kimekuwa kikiwasilisha taarifa zake za mwaka hata kabla ya kupata ruzuku... "Kama kuna watu wanaokula ruzuku na kufanya ufisadi wasituhusishe na sisi."
Mwenyekiti huyo alisema waliwasilisha taarifa hiyo kwa barua yenye kumbukumbu namba NCCR-M/MM/MS/10/25 iliyosainiwa na Beatus Mpitabakana kwa niaba ya Katibu Mkuu wa chama hicho.
Mbatia alisema NCCR pia iliwasilisha fomu namba PP17/ ya Desemba 30, mwaka jana na kuongeza kwamba, katika mwaka huo, fedha zao, ruzuku na michango ya wanachama jumla ilikuwa Sh956 milioni.
Mbatia alisema NCCR-Mageuzi hakijawahi kuacha kuwasilisha taarifa katika ofisi hiyo ya Msajili kama Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inavyoelekeza na kusisitiza: "Aliyemchafu awe mchafu yeye siyo kuchafua na wengine."
Mrema naye amtwisha Tendwa mzigo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP Agustino Mrema, kama ilivyo kwa Mbatia alielezea kukerwa kwake na taarifa hizo za chama chake kushindwa kufuata taratibu za utawala bora na kusema Ofisi ya Msajili ilikalia taarifa yake.
Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, alisema walipata barua ya Msajili wa Vyama Septemba Mosi, 2010 ikiwataka kuwasilisha taarifa za mahesabu yao.
Aliongeza kwamba katika barua hiyo, Msajili alikitaka chama hicho kuwasilisha taarifa zake kuanzia mwaka 2006/07, 07/08 na hadi za mwaka jana kitu ambacho walikifanya.
Hata hivyo, alisema walikataa mwongozo wa kuwataka watoe ada kulipa mkaguzi kutoka nje kwani tayari walikuwa na mkataba na kampuni mbili za ukaguzi.
Alisema kutokana na hali hiyo, mnamo Septemba 3, mwaka jana TLP kiliwasilisha barua hiyo ya ufafanuzi kwa Msajili iliyokuwa na taarifa hizo yenye kumbukumbu namba TLP/HQ/F/02 iliyosainiwa na Naibu Katibu Mkuu, Hamad Tao.
"Kwa hiyo sisi tulijua tumeshamaliza kazi. Hatukujua kama hiyo haikuwa sahihi. Sisi hatuna ufisadi ndugu yangu, wapo waliokula tunawajua."
"Tulishakaguliwa na watu binafsi, tuko tayari kwa kila kitu. Kitu ambacho hatukujua ni kama tunampelekea yeye CAG au Msajili. Sisi hatuna ufisadi."
"Sasa hivi (jana mchana) kuna kijana nimemwagiza akachukue ile taarifa yetu kwa Msajili tukae nayo wenyewe tujue kama tunampelekea CAG au la. Maana taarifa ipo siku zote."
Msimamo wa Tendwa
Alipoulizwa kuhusu madai hayo jana, Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa aligoma kuzungumza na licha ya kufuatwa ofisini kwake kama alivyomtaka mwandishi wa gazeti dada la The Citizen, juzi. Tendwa alimtaka mwandishi huyo afike ofisini kwake kwani jambo hilo ni nyeti na asingeweza kulizungumza kwenye simu.
Msajili akiwa nje ofisini kwake, alisisisitiza kuwa hatalizungumzia suala hilo kwa sasa mpaka baada ya Sikukuu ya Pasaka.
“Kwanza si mmeshaandika kwamba nimekataa kuzungumza, mimi nimeyasoma magazeti yenu yote, lakini mimi sikusema hivyo mimi nilichosema ni kwamba aje ofisini nimpe ufafanuzi,” alisema Tendwa mara tu baada ya mwandishi wa Mwananchi kujitambulisha, kabla hata ya kumwuliza swali lolote.
“Kwanza ile ripoti ya CAG siyo confidential (siri), ila tu ni kwamba hatukui-publish (chapisha) kwenye gazeti la Serikali, hivyo siwezi kukataa kuizungumzia. Kwani mara ngapi nimekuwa nikiitisha Press Conference (mkutano wa waandishi) hapa? Basi kama unataka sasa nitafute baada ya Sikukuu ya Pasaka,” alisema.
0 comments