Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Barua za kuwang’oa kina Lowassa zakamilika

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
 •  YADAIWA ZIKO MEZANI KWA MSEKWA

Barua za makada watatu wanaotu humiwa kwa ufisadi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rostam Azizi, Edward Lowassa, na Andrew Chenge, za kuwataka wajiondoe katika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, ziko tayari.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umethibitisha kwamba makada hao, waasisi wa mtandao uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani mwaka 2005, wanaweza kupokea barua zao wakati wowote kuanzia leo Jumatano.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, barua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) iliyomaliza kikao chake hivi karibuni mjini Dodoma.
Inadaiwa makada hao maarufu na wenye ushawishi mkubwa ndani ya nje ya chama hicho tawala, walipewa siku 90 tangu siku ya kikao, wapime wenyewe uzito wa kashfa zinazowakabili na wajiengue kwenye nafasi za uongozi, vinginevyo chama kitawaengua katika kikao kijacho cha NEC.
“Barua za Lowassa, Chenge na Rostam ziko tayari, na suala lao liko mikononi mwa Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chama. Wiki hii watakabidhiwa,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya CCM.
Pamoja na mambo mengine, barua hizo zimeorodhesha tuhuma zao na kurejea maazimio ya NEC yanayowahusu.
Alipohojiwa na Tanzania Daima Jumatano juu ya barua hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alithibitisha kwamba tayari barua hizo zimeshaandaliwa. Naye alisema watakabidhiwa barua hizo wakati wowote kuanzia leo Jumatano.
“Kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa maazimio ya NEC, si jambo geni. Ninachojua, tulikuwa tunasubiri mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka yapite, kila mtu ale Pasaka yake,” alisema Nape.
Wakati barua hizo zikisubiriwa kwa hamu, baadhi ya makada wajumbe wa NEC wamekaririwa na vyombo kadhaa vya habari na katika mazungumzo yasiyo rasmi wakisema hakukuwa na azimio lolote lililopitishwa la kuwataka makada hao wapewe siku 90 za kujiengua. Vilevile, wamekanusha kuwapo kwa azimio lolote la kuwaandikia barua.
Hata hivyo, Nape amekuwa akisema kwa waandishi na katika mikutano ya hadhara kwamba NEC ilitoa azimio hilo. Baadhi ya makada wasiokubaliana na kauli za Nape, katika hali ya kuwaonea huruma au kuwatetea watuhumiwa, wamekuwa wakidai kwamba kauli za Nape zimetoka nje, si ndani ya kikao cha NEC.
Lakini baadhi yao wamekuwa wakidokeza kuwa si rahisi Nape kujitungia maneno makali ya aina hii, huku wengine wakisema anatumwa na wakubwa “kuwashughulikia” kina Rostam.
Katika kujaribu kuthibitisha kwamba Nape anazungumza jambo lisilotokana na maazimio ya NEC, baadhi ya makada wanakumbushia kauli za hivi karibuni za mtangulizi wake, John Chiligati, ambaye amepata kutaja mara kadhaa taarifa zisizosahihi za maazimio ya vikao vya Kamati Kuu na NEC, tofauti na kilichojadiliwa ndani ya vikao hivyo.
Wanasema, kwa mfano, Chiligati alipata kulalamikiwa kwa kutoa taarifa potofu kuhusu maamuzi ya Kamati Kuu kuhusu uamuzi wa ama kuilipa au kutoilipa fidia kampuni ya uzalishaji umeme ya Dowans ambayo inaidai TANESCO shilingi bilioni 94.
Vilevile, wanasema Chiligati aliwahi kutoa maazimio ya kupotosha aliposoma maazimio ya NEC kuhusu utata ulioibuka baada ya kukatwa kwa jina la Hussein Bashe katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM kwa jimbo la Nzega katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Hata hivyo, Nape anasisitiza kuwa kauli yake ni ya chama na inatokana na maazimio ya NEC. Katika mikutano ya hadhara inayodaiwa ni ya kujitambulisha, amekuwa akisisitiza kwamba Lowassa, Rostam na Chenge wametakiwa kujiondoa kwenye ujumbe wa NEC ndani ya siku 90, vinginevyo watang’olewa kwa nguvu.
Ndiye pia aliyesema kwamba wataandikiwa barua za kuwaorodheshea tuhuma zao na kuwataka waondoke kwenye uongozi wa chama. Hata hivyo, hakuna kiongozi hata mmoja aliyesema kama makada hao watavuliwa pia ubunge.
Lowassa ni Mbunge wa Monduli, Chenge anawakilisha jimbo la Bariadi Magharibi, na Rostam Azizi ni mwakilishi wa Igunga.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanasema kilichotokea mjini Dodoma ni muendelezo wa minyukano ndani ya CCM na kwamba hoja kuu inayosababisha haya si ufisadi, bali urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, hasa kwa kuwa baadhi yao wanasemekana wanatamani kugombea au kuunga mkono baadhi ya wagombea.
Nguvu yao ya kifedha na ushawishi wao ndani ya chama ni baadhi ya mambo yanayoogopwa na washindani wao ndani ya chama tawala. Ingawa wote watatu wamekuwa watu wa karibu sana na Rais Kikwete, habari zinasema kumekuwapo na taarifa za kuchongeana miongoni mwao, zikichochewa na makachero wanaomwaminisha Rais Kikwete kwamba sifa yake iliyopotea mbele ya jamii inaweza kurudi iwapo ataondokana na watatu hao.
Rais Kikwete naye anatumia ushauri huo kama fursa ya kurejesha matumaini ya wananchi kwake na CCM, akitumia kaulimbiu ya kujivua gamba.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wakosoaji wa Rais Kikwete wamesema kujivua gamba kunakofanywa naye ni unafiki mtupu, kwani kama lengo ni kupiga vita ufisadi, naye yu miongoni mwa waliotajwa kwa ufisadi pamoja na Chenge, Rostam na Lowassa.
Baadhi ya makada wamesema kwamba kama CCm inaazimia kuondoa mafisadi, basi kiwaondoe viongozi wote waliopatikana kwa pesa za kifisadi za EPA.
Katika orodha ya viongozi waliofaidika na ufisadi wa EPA, anatajwa pia Rais Kikwete, kwa maelezo kwamba pesa hizo zilitumika kununua kura ili ashinde.
Wanasema hata kuvunja Kamati Kuu na kuingiza wajumbe wengine hakukusaidia kuisafisha, kwani walioingia ni wachafu kama waliotoka, maana historia zao na wasifu wao vinafahamika.
Wengine wanakwenda mbali na kusema kwamba iwapo Rais Kikwete atatekeleza azima yake hii, atakuwa anaandaa anguko lake lisilotarajiwa, maana atakuwa anaongeza idadi ya maadui miongoni mwa watu wanaomjua vema, waliomjenga na kumsaidia hadi hapo alipo.

0 comments

Post a Comment