MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge wa Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), Agustine Mrema ametoa siku saba kwa meneja wa kiwanda cha sukari cha Kilombero kumpa sababu za kutolipa ushuru na kuisababishia serikali hasara Sh700 milioni kwa mwaka.
Mrema alisema hayo jana alipokuwa akihutubia wananchi waliofurika kwenye viwanja vya Fire mjini Morogoro katika kongamano la amani lililoandaliwa na Taasisi ya Kiisilamu ya Al-Shababu Islamic Da-awah'.
Alisema hivi sasa wananchi hawana amani kutokana na mafisadi ndani ya serikali kuendelea kuitafuna nchi wakishirikiana na wafanyabiashara kwa mbinu mbalimbali ikiwamo kukwepa kodi na ushuru unaoliingizia pato taifa.
Mrema ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo (TLP) mkoani kilimanjaro, alitoa mfano wa halmashauri ya Kilosa na kiwanda hicho cha sukari kuwa bila huruma kimeshirikiana na viongozi wabadhirifu kuiba fedha hizo zilizotokana na tozo la asilimia tano kwa tani na kutoza Sh 200 kwa tani.
“Ina maana kwa tozo la Sh 200 kwa tani halmashauri inapata Sh 58milioni badala ya takriban Sh 750 milioni ,mimi siwezi kuwafumbia macho hawa nitahakikisha wanakamatwa na kufungwa mpaka kieleweke,” alisema Mrema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) 2007/09, mbali na wizi huo halmashauri hiyo pia iko mstari wa mbele kuhujumu hata mapato ambapo makusanyo yasiyozingatia gharama yameisababishia hasara serikali.
0 comments