Ujerumani, Urusi, China, India na Brazil zimepinga azimio lolote dhidi ya Libya
Jamii ya kimataifa, ikiongozwa na Ufaransa katika kuyashambulia maeneo yanayolengwa nchini Libya, inajiingiza katika safari yenye hatari kubwa. Vikosi vya kiongozi wa Libya, kanali Muammar Gadhafi havitashindwa kwa kufanya mashambulio machache tu ya angani yatakayolenga barabara maeneo yanayonuiwa. Wanajeshi wa Gadhafi wanaweza kurudi nyuma kutoka uwanja wa mapambano, ikihitajika, na kusubiri kwa wiki nzima, kuuzingira mji wa Benghazi ama kuyafunga maji yasifike katika mji huo.
Gadhafi anadhibiti asilimia 80 ya Libya, eneo lenye raslimali muhimu za nchi hiyo. Kama muungano wa kimataifa hauko tayari kufanya mashambulizi makali ya ardhini kuuharibu kabisa mfumo wa ulinzi wa anga ya Libya na kuharibu silaha za jeshi la angani la nchi hiyo, basi muungano huo hautaweza kufanikisha mengi katika kutekeleza marufuku ya ndege kutopaa katika anga ya Libya.
Huko Marekani kuna fikra kwamba nchi hiyo ishiriki kikamilifu Libya, lakini sio kwa kiwango kikubwa sana. Rais wa nchi hiyo, Barack Obama amefutilia mbali uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa nchi kavu nchini Libya na kuuondoa uwezekano wa kufanya harakati ya muda mrefu nchini humo. Kinachotakiwa kufikiwa na harakati hiyo ya kijeshi hakijabainika wazi mpaka sasa. Kama lengo ni kuwalinda raia kutokana na mashambulizi ya Gadhafi, basi muungano wa kimataifa unatakiwa ujiandae kufanya mashambulizi yatakayodumu miezi kadhaa. Kwa sababu Gadhafi ana muda wa kutosha, anaweza kusubiri.
Mashambulizi kutoka nje ya Libya yatakuwa na maana ikiwa yanalenga kuuondoa utawala wa Gadhafi. Na pia ingekuwa muhimu kufanya mashambulizi dhidi ya majengo ya serikali mjini Tripoli na eneo ambalo Gadhafi anaishi. Pasipo kubadili utawala, hakutapatikana suluhisho la kudumu na thabiti katika mzozo wa Libya.
Lengo pekee la kuleta mageuzi ya kiutawala, ambalo halimo kwenye azimio nambari 1973 la Umoja wa Mataifa lililoidhinisha marufuku ya ndege kutoruka katika anga ya Libya, halikuzingatiwa sana kwenye mkutano wa mjini Paris hapo jana, huku washiriki wa mkutano huo nao wakilifutilia mbali waziwazi.
Hata kwa vita hivi pia ina maana: Mtu anapoingia vitani lazima ajue vipi na lini anataka kuvimaliza vita hivyo. Nina wasiwasi muungano wa kimataifa umejiingiza katika vita hivi kwa kupuuza masomo yaliyojitokeza katika vita vya eneo la Balkan, Irak na Somalia, pengine kwa makusudi kabisa. Haijabainika wazi vipi mwisho wa vita hivi utakavyokuwa.
Ndio maana uamuzi wa serikali ya Ujerumani kutoshiriki katika harakati ya kijeshi nchini Libya ni sahihi. Hata kama mshikamano wa Ulaya utalazimika kutolewa kafara. Kumuachia rais wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy kuongoza harakati hiyo, huku yeye mwenyewe akikabiliwa na shinikizo kubwa kisiasa nchini mwake, si suluhisho la kuridhisha. Sarkozy anapenda kupitisha maamuzi kulingana na mihemko ya ghafla.
Kama muungano wa kimataifa utakuwa na bahati, kiongozi wa Libya kanali Muammar Gadhafi atakubali kusitisha mapigano na kutii amri ya Umoja wa Mataifa. Lakini ukiwa na bahati mbaya, Gadhafi atakuwa kitisho kwa silaha za maangamizo makubwa anazomiliki. Je Ufaransa na Italia zimejiandaa kwa hilo, kama Gadhafi atawaamuru wanajeshi wake wa angani washambulie kwa mabomu mji wa Napoli au Marseille? Akishinikzwa, yuko tayari kufanya hivyo.
Kama harakati ya kijeshi ya muungano wa kimataifa itasababisha idadi kubwa ya raia wasio na hatia kuangamia, je maoni ya umma katika nchi za magharibi na za Kiarabu yatageuka haraka na kuupinga muungano huo? Ama kweli safari ya hatari isiyokuwa na njia ya kutokea imeanza!
0 comments