YATOA SIKU 21 SERIKALI IMALIZE TATIZO LA UMEYA ARUSHA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepuuza kauli za na vitisho vya Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali na sasa kimesema kinaandaa maandamano mengine makubwa na mikutano ya hadhara kama kilivyofanya Kanda ya Ziwa wiki mbili zilizopita.
Zamu hii kitaelekeza mashambulizi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwamo Mbeya, Ruvuma, Iringa na Morogoro.
Lengo la maandano hayo ni kuwashukuru wananchi kwa kura za urais na ubunge; na kuishinikiza serikali kuchukua hatua muhimu ili kuboresha maisha ya wananchi.
Taarifa ya maandamano hayo ilitolewa jana katika tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA lililowasilishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, akiambatana na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam.
Katika tamko hilo, CHADEMA kilisisitiza kwamba hakiwezi kufungwa mdomo na hofu au vitisho vya serikali na CCM, ambazo zimekuwa zikilalamika na kudai CHADEMA kinahatarisha amani.
Kilitoa pia siku 21 kwa serikali kupatia ufumbuzi wa mgogoro wa umeya jijini Arusha, kama fursa ya mwisho ya serikali kumaliza suala hilo kiungwana.
Katika tamko hilo, CHADEMA kilizungumzia maeneo sita: maandamano yaliyomalizika katika Kanda ya Ziwa; maandamano yajayo katika Nyanda za Juu Kusini; uchaguzi wa Baraza la Vijana la Taifa; taarifa ya kutaka kuuawa kwa Waziri Harrison Mwakyembe na wenzake; uchaguzi wa meya Arusha; na tatizo la umeme na mengine.
CHADEMA kilisema kuwa kutokana na maandamano yaliyofanyika Kanda ya Ziwa, serikali imelazimika kutekeleza baadhi ya madai ya msingi ya chama hicho, ikiwa ni pamoja na agizo la Rais Jakaya Kikwete kuhusu kupunguzwa kwa bei ya sukari na gharama za umeme.
“Kamati Kuu inamhimiza Rais Kikwete na serikali yake wasiwe wazito wala wasione aibu ya kutekeleza yale yote ambayo CHADEMA inawashauri yenye manufaa kwa nchi, lakini wayatekeleze kwa ufanisi badala ya kufanya kiini macho,” alisema Mbowe.
Kuhusu maandalizi ya maandamano yajayo, Mbowe alisema yatafanyika Mei 4 na yataanzia mkoani Mbeya.
CHADEMA pia kimeitaka serikali ifuatilie na kutoa tamko kuhusu madai ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwamba yeye na wenzake, akiwamo Dk. Willibrod Slaa, wanafanyiwa njama kuuawa.
“Kamati imesikitishwa na ukimya wa serikali kwa ujumla kwa jambo kubwa kama hilo linalohusu maisha ya viongozi, wakati ina historia ya kuwa na haraka ya kutoa kauli katika matukio ambayo hayana maslahi kwa umma,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Kuhusu mgogoro wa umeya Arusha, CHADEMA kimepuuza maelezo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyesema wasioridhika na uchaguzi wa meya waende mahakamani.
Akijibu maswali ya waandishi kufafanua msimamo wa chama, Mbowe alisema wanachotaka wao si CHADEMA kushinda umeya, bali meya apatikane kutokana na utaratibu halali kisheria.
Alisema kwenda mahakamani ni sawa na kukubali kwamba uchaguzi ulifanyika, jambo ambalo linajenga msingi wa CCM kung’ang’ania madaraka popote inaposhindwa, huku ikidhani wananchi watakiachia tu na kukimbilia mahakamani.
Alisema baada ya siku 21 kuanzia leo Jumatatu, chama hicho kitaamua la kufanya, kama njia ya kurejesha majibu kwa wananchi wa Arusha ambao wamekuwa wakidai majibu na hata kutaka kuchukua hatua ambazo viongozi wa CHADEMA wamekuwa wanazuia.
Vile vile, alipuuza hoja ya Pinda aliyesema kwamba kwa idadi ya madiwani 16 wa CCM, 14 wa CHADEMA na mmoja wa TLP, ilikuwa wazi CCM kingeibuka mshindi.
Mbowe alihoji kama wingi wa madiwani ni hoja, ilikuwaje TLP yenye diwani mmoja ikapigiwa kura na madiwani 16 wa CCM; na akatoa mfano wa Halmashauri ya Hai ambako CCM kina madiwani wengi lakini mwenyekiti wa halmashauri aliyechaguliwa kwa kura nyingi ni wa CHADEMA.
Kuhusu matatizo ya umeme, CHADEMA kimeiona serikali dhidi ya hatua yoyote ya kuchukua hatua zitakaziligharimu zaidi taifa, kwa kufanya biashara na kampuni yoyote iliyoingia nchini katika mazingira ya utata.
Mbowe alisema inashangaza serikali inapanga kukodi mitambo ya umeme kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 260, huku ikipanga pia kubadili sheria ya manunuzi ya umma iruhusu kununua mitambo iliyotumika.
Badala yake, alisema ni vema serikali inunue mitambo yake yenyewe na itengeneze umeme usiotumia mafuta, bali wa upepo na maji.
“Tunapozungumzia umeme, watawala hawajui makali ya mgawao wa umeme, maana wote wana jenereta nyumbani na ofisini kwao,” alisema.
Katika hatua nyingine, CHADEMA kimeitaka serikali kupitia upya mikataba yote ya umeme, ya zamani na mipya, ikiwamo ya IPTL, Songa, Kiwira, Tan Power, Richmond, Dowans na mingine; na kufanya tathmini itakayoboresha mikakati mipya ya nishati ya umeme kitaifa.
Pamoja na kutaka serikali iwawajibishe wote walioliiingiza taifa katika mikataba yote mibovu, chama hicho kimeendeleza kushinikiza Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ajiuzulu.
Pamoja na mambo mengine, chama hicho kimepuuza ushauri wa serikali uliokuwa unakitaka chama hicho kipeleke hoja zake bungeni badala ya mikutano ya hadhara.
Kwa mujibu wa CHADEMA, ni haki yake kufanya mikutano ya hadhara bungeni na nje ya Bunge; na kwamba hakiwezi kufuata mipango ya CCM bali yake ya ndani, kwa sababu CCM inategemea Bunge ili itumie wingi wa wabunge wake kunyanyasa wapinzani.
Akifafanua, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema: “Vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria vina wajibu wa kutoa maoni popote, bungeni na nje ya Bunge. Tumevunja sheria gani kufanya siasa nje ya Bunge? Wanachoogopa CCM ni kwamba hawana nguvu nje ya Bunge…wamezoea kutuchakachua bungeni kwa kutumia wingi wao…lakini huku kwa wananchi hawatuwezi. Kumbuka yaliyotokea wakati wa EPA. Walitunyanyasa bungeni, tukaenda kwenye ‘mahakama ya wananchi’ na matokeo yake mmeyaona…
“Labda nimwambie (Msajili wa Vyama vya Siasa, John) Tendwa kwamba Watanzania hawana fomu bali watawala ndiyo wenye hofu, CHADEMA inafanya kazi kubwa ya kuwazuia wananchi kuingia mitaani kama walivyofanya Misri, Tunisia… kama sio sisi kuwazuia hawa watu wangeingia barabarani siku nyingi.”
Kwa mujibu wa Mbowe, serikali imepwaya na sasa inatapatapa na kulalama ikisingizia maandamano ya CHADEMA kuwa yanataka kuing’oa madarakani, jambo ambalo si lengo la maandamano hayo.
Alisema lengo la maandamano ni kuamsha wananchi kujua haki na wajibu wao, kuwashukuru kwa kura nyingi walizokipa CHADEMA, na kuiwajibisha serikali. Katika hali ya kejeli, Mbowe alisema: “Tunaandamana kushinikiza uwajibikaji wa serikali...wakitekeleza tunayosema, tutaandamana tena kuwapongeza.”
CHADEMA pia kimehoji sababu za kupanda kwa deni la taifa hadi dola za Kimarekani milioni 11,041.8 ndani ya mwaka mmoja.
“Deni hili limeongezeka kwa asilimia 18 ndani ya mwaka mmoja. Kamati Kuu imewataka wabunge wa CHADEMA kuibana serikali kueleza chanzo cha kupanda kwa deni la taifa katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Kikwete,” alisema Mbowe na kumtaka Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Ben Ndulu kutoa maelezo juu ya deni hilo lilivyopanda kwa ghafla.
CHADEMA pia imetahadharisha serikali juu ya dhamira yake ya kutaka kuongeza matumizi ya mikopo kutoka nje yenye gharama kubwa, ambapo inapanga kuchukua dola za Marekani milioni 525, hatua ambayo inaweza kuongeza deni.
Mwenyekiti huyo alisema, Kamati Kuu ya chama hicho inashauri serikali kuwa makini na dhamira yake ya kuwekeza katika uchimbaji wa madini ya uranium, ambapo izingatie athari za nyuklia katika sehemu mbalimbali duniani.
Alisema ingekuwa vema serikali itengeneze sera ya uvunaji na utunzaji wa madini hayo kabla ya kuanza uchimbaji wake, ili kuondokana na athari ambazo zinaweza kulikumba taifa kutokana na kukosa maandalizi ya kutosha kuchimba na kutumia madini hayo adhimu.

0 comments