Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Askofu amshitaki Katibu wa CCM. Atiwa mbaroni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
JESHI la Polisi wilayani Mpanda limemkamata Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo, Jacob Nkomola, kwa tuhuma za kumtolea maneno ya kashfa na kumtishia maisha Makamu wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Padri Patrick Kasomo.

Kukamatwa na kuhojiwa kwa Katibu huyo wa CCM kunatokana na kufunguliwa kwa jalada namba RB/849/2011 na Padri Kasomo dhidi yake juzi kwenye Kituo Kikuu cha Polisi mjini humo.

Kasisi huyo ambaye pia ni Paroko wa Kanisa Katoliki Karema anadai Nkomola alitoa pia maneno ya uchochezi akihamasisha vijana kuandamana hadi nyumbani kwake (Kasomo) ili wamvue joho la kichungaji na kumpiga, kwa kuwa hana sifa za kuwa kiongozi wao wa kiroho.

Inadaiwa maneno hayo ya kejeli na kashfa pamoja na kutishia maisha aliyatoa alipohutubia mikutano kwenye vijiji vya Karema na Kaparamsenga, iliyoitishwa na Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso kwa lengo la kushukuru wananchi kwa kumchagua.

Hadi jana haikuwa imefahamika mara moja kama Katibu huyo ataachiwa kwa dhamana au la, kwani ilielezwa kuwa bado anaendelea kutoa maelezo kwa maandishi kituoni hapo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaluanda, alithibitisha kukamatwa na kuhojiwa kwa Katibu huyo, na kuongeza kuwa kasisi huyo aliamua kumshtaki baada ya jitihada za usuluhishi za Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo kushindikana.

Hata hivyo habari ndani ya Jeshi la Polisi Mpanda zinadai kuwa upo uwezekano mkubwa Katibu huyo wa CCM kufikishwa mahakamani kesho kutwa.
Tags:

0 comments

Post a Comment