Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Chadema wachafua hali ya hewa bungeni. Watoka tena nje

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WABUNGE wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe jana walichafua hali ya hewa bungeni pale walipotoka tena nje ya Ukumbi ya Bunge kupinga azimio la kuondoa utata wa tafsiri ya Kanuni ya Bunge inayotoa fursa kwa chama chenye asilimia 12.5 ya wabunge wote kuunda kambi rasmi ya upinzani.
Tukio hilo linalofanana na lile la  Novemba 18, mwaka jana, Rais Kikwete alipozindua Bunge lilifanywa na Chadema baada ya Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro kuchangia mjadala wa huo akiwa mchangiaji wa mwisho.

"Madamu Bunge limeona busara kuleta hoja hii, na vijembe vile, kwa masikitiko nasema hatutashiriki kumalizia hoja hii, naomba kutoa hoja," alimalizia maelezo yake Mbowe na kuanza kutoka nje akifuatiwa na wabunge wa chama hicho.

Hata hivyo, wakati wabunge hao wa Chadema wakitoka nje, wabunge waliobaki wengi wakiwa wa chama tawala CCM, walisikika wakitoa maneno ya kebehi dhidi ya wabunge wa Chadema.

"Tumewazoea kukimbia, kwisha, uchoyo, weak politicians, na kwenye posho msije, mnadaiwa na mabenki,"walisikika wabunge wakisema kwa kupiga kelele.

Awali Mbowe akichangia mjadala huo alisema kuwa ushirika ni jambo la msingi, lakini katika Bunge la Kumi kuna tofauti za msingi.

"Bunge la Kumi kuna tofauti za msingi, haki ya kila chama haiondolewi kwa dhana za juu juu. Kuchagua mshirika ni haki yetu kikatiba na hatuwezi kulazimishwa ndoa, tumeona vijembe vilivyotokea leo tutawezaje kuwa na kambi moja?. Tunahitaji muda zaidi" alisema Mbowe na kuongeza:

“Ni vigumu ukalazimishwa uchumba na mtu hivyo hivyo hatuwezi kulazimishwa  katika ushirikiano,’’ alisema na kuongeza: “ Hakuna trust(uaminifu) katika ushirika huu.’’

Aliongeza: "Viongozi wa vyama kushirikiana ni vizuri, tupeane muda, maridhiano hayawezi kuwa ndani ya wiki moja au mbili. Uamuzi wenu unabomoa, kwani hapa tatizo si tafsiri bali dhana ya ushirika tunaotaka bungeni. Yapo ya msingi, lakini si kutulazimisha kuingia katika jambo ambalo hatujaridhia."

Mbowe alisema tofauti zilizopo zinazungumzika huku akionya kuwa wingi usitumiwe kugandamiza Chadema na kwamba kanuni zisitumiwe kuua msingi wa haki ambapo pia alieleza kuwa chama chake hakitakubali hilo na ndiyo dhamira ya Chadema.

Wakati wakitoka kwenye ukumbi huo, majira ya saa 11:30 jioni wabunge wengine wa CCM, TLP, NCCR-Mageuzi, UDP na CUF walioonekana kushikwa butwaa kwa kitendo hicho.


Mkutano na Waandishi wa Habari

Baada ya kutoka nje,  Mbowe alizungumza na wanahabari, mkutano ambao ulirushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Star (Star TV).

Katika mkutano huo, Mbowe alisema wataendelea kupinga vitendo vyote vinavyovunja Kanuni za Bunge kwa maslahi ya Bunge na Taifa.

"Hatutawaheshimu kamwe wabunge 'wanaocompromise' haki zao (wanaokubali haki zao kudhulumiwa), na tutaendelea kupinga kilichotokea leo, ndani na nje ya Bunge," alisema Mbowe.
Hata hivyo, baada ya kumalizika na kupitishwa marekebisho hayo ya kile kilichoelezwa kuwa kuondoa utata wa tafsiri katika kanuni ya 14 hadi 16 ya Bunge, wabunge hao wa Chadema walirudi ndani ya Ukumbi wa Bunge na kuzua tena maneno ya chini chini kutoka kwa wabunge.

Kwa kupitishwa mabadiliko hayo na kwa mujibu wa kanuni ya 15(2) tafsiri ya Kambi Rasmi ya upinzani bungeni ni kambi inayoundwa na vyama vya upinzani vinavyowakilishwa bungeni.

Hata hivyo, bado Chadema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ndicho kitakachotoa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na naibu wake. Pia kiongozi huyo ana mamlaka na uhuru wa kuteua Baraza la Mawaziri Kivuli kutokana na wabunge wa upinzani waliopo.

Hata hivyo, azimio hilo linaondoa dhana iliyokuwepo kwamba Chadema ndicho kingetoa wenyeviti wa Kamati za Hesabu za Serikali ambazo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge zinatakiwa kuongozwa na wapinzani.

Tofauti na ilivyokuwa ikifahamika awali, mabadiliko ya jana yanatoa fursa kwa mbunge yeyote wa upinzani kugombea nafasi hizo bila kuhitaji idhini ya  uongozi wa kambi ya upinzani.

Wachunguzi wa mambo ya siasa wanaiona hatua hiyo kuwa ni kuwanyima Chadema nafasi ya kuongoza kamati hizo, kwani kwa kuzingatia uhusiano wake mbaya na CCM ni dhahiri nafasi za wenyeviti zitakwenda kwa vyama vya CUF, NCCR – Mageuzi , TLP au UDP ambavyo wabunge wake walikuwa wakiunga mkono azimio la kuingizwa kwa tafsiri hiyo katika Kanuni za Bunge.


Spika Anne Makinda
Kabla ya kuhitimishwa kwa hoja hiyo iliyopigiwa kura na kupitishwa, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema kuwa:
"Katika hoja hii, Chadema haikuwa na ukweli, wananchi wajue hili. Wenzetu wamepitiwa. Kitendo kilichotokea  hapa si utaratibu mzuri, watawaambia nini wananchi?."

Spika alionekana kukerwa na kitendo hicho cha Chadema na kuhoji iwapo kweli wabunge hao wapo kwa ajili ya maslahi ya umma au maslahi yao wenyewe.

Hata hivyo, mkutano wa Bunge uliendelea kwa Naibu Spika, Job Ndugai kufafanua baadhi ya vipengele vinavyohalalisha uwepo wa kambi ya upinzani bungeni.

Kwa pamoja wabunge waliobaki walipitisha azimio la kuwepo kwa kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Vijembe vya Mrema na Lusinde
Mbunge wa Jimbo la Vunjo(TLP), Augustine Mrema pamoja na Livingstone  Lusinde wa Jimbo la Mtera (CCM) waliwapiga vijembe Chadema wakati wakichangia hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa Novemba 18 mwaka jana alipokuwa akizindua rasmi Bunge la Kumi.

Mrema aliwapiga vijembe Chadema akisema alistahili kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani kutokana  na uzoefu pamoja na sifa alizonazo.

“Nimekuwa mbunge mara tatu kwa vyama vitatu tofauti, nimekuwa naibu waziri mkuu, nikakamata kontena la dhahabu, niliweza kupambana na ufisadi  hivyo nilistahili kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani,” alisema Mrema.

Naye Lusinde alikwenda mbali na kusema kutokana na viongozi kuonekana kuchoshwa na amani iliyopo, alipendekeza wabunge wapigane bungeni ili wajue uchungu wa kupoteza amani.

“Nafikiri kuliko kuwashawishi kwanza wananchi wavunje amani kwanza ningependa kuona siku moja bungeni humu wabunge tukizichapa ili tujue  uchungu wa kupoteza  na si tu kuwashawishi wananchi halafu sisi viongozi hatudhuriki na tunajipatia sifa za bure,’’ alisema Lusinde

Tags:

0 comments

Post a Comment