Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Waislamu kupendekeza wanaostahili kukusanya maoni ya Katiba mpya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter ILI kumsaidia Rais Jakaya Kikwete apate wajumbe wanaokubalika wa tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya, Waislamu nchini Jumamosi ijayo watapendekeza majina ya viongozi wa taasisi na jumuiya wanaoona wanastahili kuwa miongoni mwa watakaoteuliwa kusimamia wajibu huo.

Vilevile, wamejitolea kusaidia kukusanya maoni ya Waislamu wote nchini kupitia njia za mawasiliano zinazofahamika kama vile misikiti na mabaraza ya Kiislamu, na kuyakabidhi kwa tume hiyo, ili kuirahisishia kazi.

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa majina hayo ambayo hata hivyo hakutaja idadi yake, yatapendekezwa kwenye mkutano huo mkubwa utakaojumuisha taasisi kubwa za Kiislamu 20, ikiwamo Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

“Mkutano utafanyika kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi jioni kwenye ukumbi wa Tanzania Muslim Solidarity, Mtaa wa Mafia, karibu na Ofisi za Makao Makuu ya CCM Mkoa, Jijini Dar es Salaam na utahusisha taasisi na Jumuiya za Kiislamu kama 20 hivi kati ya zaidi ya 50 zilizopo kwa kuwa hizi ndizo kubwa na zenye uwakilishi mkubwa,” alisema Shehe Ponda.

Alitaja baadhi ya tasisi na jumuiya hizo kuwa ni Jumuiya ya Wanataaluma wa Kiislamu Nchini (TAMTRO), Shura ya Maimamu Tanzania, Baraza Kuu, Umoja wa Wahadhiri wa KiislamuTanzania, Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu wa Vyuo Vikuu Nchini (MSAUD), Muslim Solidarity, Jumuiya ya Maendeleo ya Waislamu (IDF), Kituo cha Kiislamu (MARKAZ) na nyinginezo.

“Barua ya mwaliko wa Bakwata itapelekwa kwa uongozi wake kesho (leo) asubuhi ili nao washiriki na kutoa mapendekezo yao. Taasisi na jumuiya nyingine zinataarifa na kwa msisitizo zaidi nazo zitapatiwa barua kuhusu mkutano huo kesho hiyo hiyo (leo),” alisema Ponda.

Kwa mujibu wa Ponda, pamoja na kupendekeza majina hayo, mkutano huo utaendeleza hoja za ule wa Desemba 24, uliojadili njia zinazofaa kutumika kukusanya maoni ya Waislamu nchini.

Katika hatua nyingine, Ponda ameeleza kufurahishwa kwa wana jumuiya na taasisi za Kiislamu na maelezo ya Rais Jakaya Kikwete kwamba tume atakayoiunda itajumuisha wawakilishi mbalimbali kutoka katika taasisi tofauti zikiwamo za dini.

“Tunaamini kwa kufanya hivyo tutakuwa na tume yenye mawazo tofauti yatakayoleta changamoto na matokeo yanayotegemewa na Watanzania wengi.

Tunaamini pia kuwa Rais hatatupilia mbali mapendekezo ya majina ya wajumbe kutoka upande wetu Waislamu kwa sababu tunawafahamu zaidi na tutawachagua kwa kuzingatia uaminifu na uadilifu wao kwa nchi hii,” alisema.

Rais Kikwete alieleza msimamo wake kuhusu Katiba mpya na tume atakayoiunda mwishoni mwa mwaka uliopita wakati akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni na redio kama ilivyo ada kwa kila mwisho wa mwezi.
Tags:

0 comments

Post a Comment