IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MJADALA wa Katiba mpya uliobarikiwa na Rais Jakaya Kikwete baada ya kutangaza kuunda tume ya kukusanya maoni, umeanza kushika kasi kwa mapendekezo mbalimbali kutolewa huku Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini, akipendekeza mawaziri wasiwe wabunge.
Kilaini, ambaye ni mmoja wa viongozi waliozungumza na gazeti hili jana kuhusu baadhi ya mambo ambayo yanayohitaji mjadala wa kina kuhusu ujio wa Katiba hiyo, alisema lengo ni kuongeza uwajibikaji majimboni.
Alisema mfumo wa sasa wa uteuzi wa mawaziri unaotamkwa katika Katiba iliyopo, unawafanya mawaziri walio wengi kutumia nafasi zao kufanya mambo ya majimboni kwao na baadaye kujisifu kuwa wamefanya mambo hayo kwa kuwa ni wabunge wakati si kweli.
Katiba ya sasa, kifungu cha 55, kifungu kidogo cha 4, kinasema kuwa lazima mawaziri wawe wabunge.
“Nampongeza Rais kwa hatua hiyo ya kuruhusu mchakato wa Katiba mpya, lakini mapendekezo yangu ni kutoruhusu uteuzi wa mawaziri kuwa lazima wawe wabunge, mawaziri watolewe katika mfumo mwingine wa serikali,” alipendekeza Kilaini.
Hoja hiyo ya Kilaini, iliungwa mkono na mwanaharakati wa haki za binadamu na jinsia, Gema Akilimali, ambaye alisema mbali ya kutoka nje ya Bunge, lakini alipendekeza mawaziri wawe wataalamu wa sekta wanayokabidhiwa kuisimamia, ili watumie upeo wao kufanya uamuzi kwa maslahi ya jamii.
“Kumekuwa na shida ya kuchambua ni wapi mtu anawajibika kama mbunge na wapi kama waziri, haiwezekani mtetezi huyo huyo wa wananchi awe mtetezi wa serikali, wananchi ndiyo wenye sauti kwa serikali hivyo mawaziri wawe nje ya wabunge,” alisema Akilimali.
Hata hivyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alipinga hoja hiyo na kufafanua kuwa waziri lazima awe mbunge kwa kuwa kazi yake ni kutengeneza sera zinazomtetea mwananchi.
Mukandala aliponda dhana kwamba mawaziri ambao si wabunge watasaidia kuondoa siasa katika utendaji, na kuongeza kuwa dhana hiyo ikikubaliwa, ni sawa na kunyamazisha sauti ya umma kwa serikali kwa kuwa watengeneza sera wanapaswa kuwa wawakilishi wa wananchi.
“Sera zikitengenezwa na wataalamu, si wawakilishi zitamnufaisha nani? Faida ya kuwa na mfumo tulio nao ni nyingi maana sera zinazungumzwa na wawakilishi wa wananchi,” alisema Mukandala akiutetea mfumo uliopo.
Mbali na hoja hiyo, Kilaini na Akilimali walipendekeza kuwepo idadi maalumu ya mawaziri, tofauti na ilivyo sasa ambapo Katiba kifungu hicho cha 55, kifungu kidogo cha 3, kimempa Rais mamlaka ya kuchagua idadi yoyote anayoitaka.
Kilaini alishauri idadi ya mawaziri iwekwe kwa mujibu wa sheria ili kuepusha uteuzi kwa misingi ya kujuana.
Akilimali katika hilo alisema, “baada ya uchaguzi, nilishtushwa na kusikitishwa na idadi ya mawaziri wapya, binafsi nilitegemea ingepungua lakini haikuwa hivyo, kupunguza Baraza la Mawaziri ni suala la msingi, ingefaa hata kuwa na mawaziri 15 na wasaidizi watano.”
Hata hivyo, Mukandala katika hoja ya idadi ya mawaziri, alitofautiana na Kilaini na Akilimali kwa kufafanua kuwa hoja hiyo itaharibu mfumo mzima wa utendaji kama itakubaliwa.
“Kuna ugumu mkubwa katika ukomo wa idadi ya mawaziri hasa kwa nchi zetu, Marekani na Uingereza wana ukomo, lakini wana msururu wa watendaji kiasi kwamba gharama zinakuwa zaidi ya ingekuwa baraza. “Kubwa ni kuangalia namna ya kubana matumizi na si idadi, kuwe na mlinganisho wa matumizi na mapato, kuwe na uwiano na kumuachia Rais apunguze au kuongeza (mawaziri) akisimamia uwiano huo,” alisema Mukandala.
Kuhusu suala la mgombea binafsi, Kilaini, Akilimali na Mukandala walikubaliana kuwa ni haki ambayo inatakiwa kulindwa na Katiba mpya.
Mukandala alisema huu ni wakati muafaka kuwa na mgombea binafsi kwa kuwa ni haki ya msingi ya kikatiba na ya binadamu.
Hata hivyo alisema ni vigumu kwa mgombea binafsi wa nafasi ya urais kushinda urais kwa hapa nchini, labda awe na mvuto mkubwa kwa wananchi na kama atakuwa hivyo, ataweza pia kuunda serikali kwa kutumia nguvu ya mvuto wake.
Kauli ya Mukandala iliungwa mkono na Kilaini ambaye alishauri kuwa mgombea binafsi awepo lakini akasema iwe kwa nafasi ya ubunge na udiwani pekee na kuacha rais atokane na chama cha siasa.
“Nchi zinazoendelea bado mfumo huu utatusumbua kwa ngazi ya rais, hata Marekani ingawa ni taifa tajiri bado hawajaweza hili ingawa ni ruksa kwao kuwa na mgombea binafsi,” alishauri Kilaini.
Naye Akilimali alisema huu ndio wakati muafaka kwani wapo Watanzania wengi wanaoweza kuongoza nchi ila wanashindwa kwa sababu hawataki propaganda za vyama vya siasa.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwette akizungumzia suala la Katiba mpya hasa vipengele hivyo vya idadi ya mawaziri, mawaziri kuwa wabunge na mgombea binafsi, alisema msingi wa yote utaonekana baada ya Rais Kikwete kuteua tume huru na kutoa adidu za rejea.
Prof. Mbwette alisema kinachotakiwa katika kushughulikia mchakato huo ni uwazi na ukweli huku akimtaka Rais asiwe na mkono katika utendaji wa tume na kutoa angalizo wakati wa kushughulikia masuala ya Muungano kuwa makini la sivyo vurugu zinaweza kutokea.
“Ni mapema kusema nini kibadilishwe au nini kitabaki kilivyo, tusubiri adidu za rejea, Rais azitoe kwa kuzingatia uwazi na ukweli na pia angalizo ni namna masuala ya Muungano yatakavyozungumziwa, kuwe na umakini mkubwa ili kuepusha vurugu.
Katika hilo la Muungano, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila alisema Katiba mpya inapaswa kuangalia masuala ya Muungano akitolea mfano serikali ya mseto ambayo Katiba ya Muungano haisemi kitu kuihusu.
Kuhusu mabadiliko mengine, Lolila alisema si haki kuanza kuchambua kipi kibadilishwe kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kutomtendea haki Rais aliyeridhia suala hilo, lakini alishauri mchakato usichukue muda wala usiharakishwe kuruhusu kila wadau kutoa mchango na maoni yao.
Kuhusu suala hilo la muda wa lini Katiba mpya ipatikane, Kilaini alishauri suala hilo lisiharakishwe wala kupoteza muda mrefu na kupendekeza miaka mitatu Katiba mpya iwe mezani.
“Pengine liwekwe na kufanyiwa kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mitatu, mfumo wa kura za maoni utumike, ili tupate miaka miwili ya kujiandaa katika uchaguzi wa 2015 tukiwa na Katiba mpya,” alishauri Kilaini.
Mukandala katika hilo alisema si rahisi sherehe za miaka 50 ya Uhuru kuwa na Katiba mpya kama baadhi ya watu wanavyoshinikiza na kuongeza kuwa suala hilo linahitaji kushirikisha wananchi, wadau wengi lakini akaafiki kuwa mpaka uchaguzi ujao (2015) tuwe na Katiba mpya.
Akilimali naye alishauri muda uwe miaka mitatu lakini akachambua kuwa mwaka mmoja wa kura za maoni kwa wananchi na wadau, wa pili kufanyia kazi maoni na mwaka wa tatu kutengeneza Katiba mpya na kuiweka mezani tayari kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na Katiba mpya.
Rais Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mwaka, alibainisha mambo yaliyofanywa na Serikali yake mwaka jana na kutaja baadhi ya mipango ya mwaka huu ikiwemo kuridhia Katiba mpya na kubainisha kuwa ataunda tume itakayoanza mchakato wa kukusanya maoni na kuipa adidu za rejea ili kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya taifa.
You Are Here: Home - - Kilaini: Katiba mpya ipunguze mawaziri
0 comments