IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema hakitakwenda mahakamani wala kuleta vurugu wakati wa kudai haki ya msingi ya kufanyika upya uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha, badala yake kitaishinikiza Serikali ikubali kwa kuwa uchaguzi uliofanyika wa kumweka Gaudence Lyimo kuwa Meya ni batili.
Mbali ya hilo pia kimeendelea kusisitiza kuwa Mery Chatanda, Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Tanga, sio mjumbe halali wa Baraza la Madiwani la Arusha na hapaswi kuingia katika kikao chochote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, aliyekuwa mgombea wa kiti cha meya kupitia Chadema, Estomih Mallah alisema Chadema haijafanya uchaguzi wa meya na haiko tayari kufanya uchaguzi wenye kuleta madhara, bali itahakikisha utaratibu na kanuni zinafuatwa kwa mujibu wa sheria iliyowekwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mallah alisema yeye kama Diwani Kata ya Kimandolu, hana ‘’uroho’’ wa madaraka ya umeya bali yuko katika kusimamia haki ya msingi iliyowekwa na serikali kupitia wizara yake.
Alimuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa la kushawishi pande zote zikae pamoja na kuangalia nini cha kufanya juu ya mstakabali wa Jiji la Arusha na sio kulumbana bila ya kuwa na hoja ya msingi.
Mallah alisema kuwa keshokutwa viongozi wa juu wa Chadema na wabunge wa chama hicho, watafanya mkutano mkubwa katika uwanja wa NMC kuishinikiza Serikali ikubaliane na madai ya chama hicho ya umeya na Chatanda kutokuwa mjumbe wa Baraza la Madiwani la Jiji la Arusha.
Alisema suala hilo limefika katika hatua ya mwisho ikiwa ni pamoja na kwa Mkuu Polisi nchini, IGP Said Mwema ili wapate kubali cha mkutano huo.
‘’Tutaishinikiza Serikali ya CCM ikubali mazungumzo kuhusu utata huo kwa amani bila kumwaga damu,” alisema.
You Are Here: Home - - Chadema kudai umeya Arusha kwa shinikizo
0 comments