Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - UVCCM wacharuka, waiponda serikali

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MSUGUANO wa maneno kwa baadhi ya mawaziri na wajumbe wa vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umewakera viongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), ambao umewaonya viongozi hao kufuata utaratibu au waachie ngazi na nafasi zao zijazwe na vijana.

Pia umoja huo umewalaumu baadhi ya wajumbe wa vikao hivyo, Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC) kuwa chanzo cha chama hicho kupoteza majimbo na kata kadhaa katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

UVCCM, ambayo imejinasibu kuwa waangalizi wa chama hicho na Serikali, mbali na kuwakemea viongozi wao, pia imeingia katika msuguano uliopo wa malipo ya Kampuni ya kufua umeme ya Dowans Costa Rica kwa kutaka majina ya wamiliki wa Kampuni ya Richmond yatajwe.

Viongozi hao wamesema haiingii akilini wamiliki wa Dowans Costa Rica, wajulikane na walipwe fidia ya Sh bilioni 94, wakati aliyerithisha mkataba kwa kampuni hiyo, Kampuni ya Richmond wamiliki wake hawajulikani.

Wamependekeza, kama Serikali haiwajui wamiliki wa Richmond, basi wamiliki wa Dowans Costa Rica, ambao wameshatambulika, waisaidie Serikali kuwataja waliowarithisha mikoba yao iliyowasaidia kushinda kesi ya kulipwa mabilioni hayo na si kuendelea kuwaumiza Watanzania.

Kauli hizo ni sehemu ya tamko la Kamati ya Utendaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa, lenye vipengele vitano, lililotolewa jana, Dar es Salaam na kamati hiyo kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini baada ya Kaimu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Beno Malisa kueleza kuwa walikaa juzi na kufikia uamuzi huo.

Vipengele hivyo ni hali ya CCM na UVCCM, mpango wa Dk. Willibrod Slaa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuvuruga amani na kufanya nchi isitawalike, viongozi wa dini na mjadala wa siasa, sakata la Dowans na matatizo ya vijana nchini.

Katika suala la hali ya CCM na UVCCM, Mwenyekiti wa umoja huo Mkoa wa Mara, Marwa Mathayo alisema viongozi wa CCM hawapendani, wamejenga chuki, uhasama na majibizano ya hovyo na hivyo hawana urithi wowote kwa vijana wa leo.

“Waache mara moja wanaofanya hivyo kwa kuwa wao walipokuwa vijana, hawakufanyiwa hayo, wasipoacha tutawataja kwa majina na kuwataka vijana kote nchini kuandamana na kuwalaani maana uhasama na chuki zao zinaleta mpasuko katika jamii na chama kwa ujumla,” alisema Mathayo.

Katika hilo, Mathayo alisema baadhi ya mawaziri wameacha kufuata msingi wa Ilani ya chama hicho na kila mtu amekuwa akisema lake bila kujali Katiba ya CCM, tofauti na zamani ilivyozoeleka kuwa kauli ya mawaziri ni moja.

“Hivi sasa kila mtu anasema lake, sisi tunarithi nini? Haieleweki kauli ya Serikali ni ipi, hii inahatarisha amani ya nchi, sasa amebaki Rais (Jakaya Kikwete) pekee kusema kauli ya Serikali.

“Hatupo tayari kwa hilo, tumepoteza majimbo na kata kwa sababu ya baadhi ya wajumbe wa NEC na CC wasioheshimu Katiba ya chama, kama kuna kiongozi anajiona bora kuliko wengine, tutamweka wazi,” aling’aka Mathayo.

Baadaye katika maswali, Katibu Mkuu wa umoja huo, Martin Shigela alisema tabia ya mawaziri kuropoka haivumiliki, “Leo Ngeleja (Waziri wa Nishati na Madini) anasema hili, kesho Sitta (Waziri wa Afrika Mashariki) anasema lile, hii si sawa, kama kuna mtu anaona Ilani ya CCM haimfai, aachie ngazi.”

Kuhusu Kampuni ya Dowans Costa Rica, mjumbe wa kamati hiyo, James Millya ndiye aliyetolea tamko ambapo alisema mara baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) kuitaka Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuilipa kampuni hiyo Sh bilioni 94, kauli mbalimbali kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri mwenye dhamana, Ngeleja ziliamua fedha hizo zilipwe ikiwa kesi itasajiliwa katika Mahakama Kuu.

Alisema hata hivyo baadhi ya wanaharakati na wanasiasa akiwemo Samwel Sitta waliibuka na kupinga fedha hizo kulipwa na kueleza kuwa suala hilo halijajadiliwa katika Baraza la Mawaziri.

“UVCCM tunalaani kitendo cha mawaziri kupingana hadharani na kutokuwa na uwajibikaji wa pamoja, tunataka kama wamechoka kuziongoza wizara zao, waachie ngazi, wawapishe vijana wenye nia njema na kufuata maadili ya taifa letu.

“Tunaitaka Serikali kuwataja rasmi wamiliki wa Richmond ili ijulikane kipi ni kipi na hoja hii irudi bungeni ili Watanzania wajue nani aliifikisha Serikali hapa ilipo, kama ni Tume ya Mwakyembe (Dk. Harrison-aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata hilo wakati ule, sasa Naibu Waziri wa Miundombinu) ililidanganya taifa, iwajibike na kama ni serikali basi imtaje mmiliki, ili yeye alipe pesa hizo na si wananchi,” alisema Millya.

Millya alisema wanayotaarifa kuwa sakata hilo lilianzia bungeni na hatimaye Tume (ya Mwakyembe) ilitoa ripoti kuwa Richmond ni kampuni hewa na wamiliki wake halali hawajulikani.

Wakati wa kujibu maswali ya waandishi, Shigela alijibu suala la Dowans na kusisitiza kuwa UVCCM inataka wamiliki wa Richmond watajwe kama ni Lowassa (Edward-aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo) au Rostam Aziz (Mbunge wa Igunga), ili kama Mwakyembe alidanganya ijulikane na kuwajibishwa au la wamiliki hao ndiyo walipe fedha hiyo.

Kipengele cha matatizo ya vijana nchini, kilizungumzwa na Zainabu Kawawa ambaye aliipongeza Serikali kwa juhudi za kutengeneza ajira milioni 1.2 lakini alisema umoja huo unaona bado haijatekeleza wajibu wake kwa vijana.

Alifafanua kwamba vijana wanaozalishwa kila mwaka katika soko la ajira ni 700,000 wakati katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ni ajira milioni 1.2 tu zilizalishwa na milioni moja zikiwa si rasmi huku 200,000 rasmi.

Alisema kwa takwimu hizo za Serikali, inaonesha kuwa vijana karibu milioni mbili hawana ajira. Pia waliitaka Serikali kuivunja Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HLSB) na kuiunda upya kwa kuwa hawana imani na utendaji kazi wa Bodi hiyo, kwa kuwa imekuwa chanzo cha migomo katika vyuo vikuu wakati madai ya wanafunzi yangeweza kutatuliwa kabla ya migomo.

“Unashangaa kama Mkwawa (Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) waligoma na baada ya siku mbili fedha ikapatikana, hivi hiyo fedha ilipatikanaje? Yaani kuna watendaji wapo kusubiri wanafunzi wagome ndipo fedha itoke, hatupo tayari kuona hilo linaendelea, Bodi ipinduliwe na kuundwa upya,” alitoa tamko Kawawa na kuongeza:

“Tunataka CCM na Serikali yake iwawajibishe wanaohusika kwa kuwapeleka mahakamani kwa kusababishia hasara serikali na wasiofaa wapishe nafasi hizo wachukue wanaofaa, tunataka vijana wasome kwa raha kwa kuwa ndiyo watendaji wajao wa Serikali hii.”

Mpango wa Dk. Slaa Baada ya Kawawa kuzungumza hilo, Shigela alisema taasisi hiyo imehuzunishwa na matukio ya vurugu yaliyosababisha vifo vya vijana huko Arusha ambayo kwao wanaamini yalichochewa na Chadema pamoja na Dk Slaa.

Shigela alisema kamati yao ilitafakari mpango wa Chadema na hasa Dk. Slaa, Katibu Mkuu wa chama hicho na kwamba kashfa ya kufukuzwa upadri inadhihirisha upungufu wa mtu huyo.

“Tunaomba Serikali imkamate ... akachunguzwe maana si mtu wa kawaida, UVCCM tunataka Watanzania wajihadhari na Dk. Slaa maana historia na matendo yake yanaonesha ...ni dhahiri kuwa uongozi wa Chadema umechakaa na kupauka.”

Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa alizungumzia suala la viongozi wa dini na mjadala wa siasa ambapo aliwataka viongozi hao wasimame katika nafasi zao kidini na si kuwagawa Watanzania kwa kushabikia siasa kama ilivyojitokeza hivi karibuni.

“UVCCM inatambua na kuthamini nafasi ya viongozi wa dini nchini, kitendo cha baadhi yao kuanza kushabikia siasa kama ilivyojitokeza hivi karibuni, hakikubaliki hata kidogo na kinagawa waumini wa dini kwa kuingiza itikadi za siasa katika misikiti na makanisa, hatupendezwi na hili na tunawaomba wabaki katika kusaidia kuleta amani, upendo, mshikamano na umoja,” alisisitiza Malisa.

Hali ya Kisiasa, Vijana Zanzibar Hili lilizungumzwa na Tauhida Cassian Galoss, aliyesema hali ya siasa visiwani humo ni shwari lakini alionya kuwa pamoja na muafaka, CCM itabaki kuwa CCM na CUF kuwa CUF na kwamba maana ya muafaka ni CCM kuendelea kuwa madarakani.

Hata hivyo alisema UVCCM hawakuridhishwa na ushindi wa asilimia 51.4 aliyoupata DK. Ali Mohamed Shein (Rais wa Zanzibar) na wamejipanga kama vijana kuhakikisha kuwa CCM visiwani inaendelea kutawala.
Tags:

0 comments

Post a Comment