Aidha, balozi huyo amesisitiza kwamba uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa kwa uhuru na amani.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, balozi huyo alisema taarifa za baadhi ya vyombo vya habari zimekuwa zikipotosha kuwa huenda kutatokea uchakachuaji wa kura kwa wakazi wa Kusini wanaoishi Kaskazini ili malengo yaliyowekwa yasifikiwe.
“Kufuatia kuandaliwa kura ya maoni kuhusu uhuru wa Kusini, kutakakofanyika siku ya Jumapili ijayo (kesho), ubalozi wa Sudan nchini Tanzania unapenda kueleza kwa vyombo vya habari na dunia kwa ujumla kwamba hakutakuwa na wizi wowote wa kura ulioelezwa kufanywa na Sudan ya Kaskani,” alisema.
Alisema kura zote zitapigwa na wananchi wa Sudan halali wenye hati ya makazi.
Akimnukuu rais wa nchi hiyo, Omar al-Bashir katika ziara aliyoifanya Juba alisema atakuwa na furaha endapo Wasudan kusini watapiga kura kwa umoja lakini atakubali uamuzi wao kama watachagua kugawanyika.
Akiendelea kumnukuu alisema, Rais Bashir atakuwa radhi kwa Wasudan wengine kuungana pamoja na taifa jipya kuendelea na amani, usalama na maendeleo kwa wote.
“Sudan iko tayari kumaliza migogoro yake kwa amani na kutoa picha ya makubaliano hayo kwa vitendo,” alisisitiza balozi huyo.
Kura hiyo ya maoni itakayochukua wiki nzima inayoanza siku ya Jumapili ni sehemu ya makubaliano ya mwaka 2005 yaliyomaliza vita vilivyodumu kwa miongo miwili nchini humo.
0 comments