UJIO wa noti mpya katika mzunguko wa fedha hapa nchini, umeleta hofu kwa baadhi ya wananchi na wafanyabiashara mkoani hapa kwa baadhi yao kufikia hatua ya kukataa kuzipokea.
Hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa kwa baadhi ya watu ambao tayari wameanza kuzitumia.
Benki kuu ya Tanzania (BoT) iliruhusu kuingizwa kwenye mzunguko noti hizo mpya za viwango vya sh 500, 1000, 2000, 5,000 na 10,000 Januari mosi mwaka huu, huku ikitoa angalizo kwa wananchi kuwa noti za zamani bado ni fedha halali na zina thamani sawa na zile mpya.
Lakini katika hali isiyo ya kawaida abiria mmoja aliyepanda gari ya abiria kutoka eneo la Mbalizi kuelekea Sokomatola jijini hapa jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kondakta wa daladala aliyefahamika kwa jina moja la Suleiman kugoma kupokea noti mpya ya sh 10, 000, aliyopewa na abiria huyo kama nauli.
Hali hiyo iliibua malumbano makali baina ya kondakta wa daladala na abiria huyo, jambo lililolazimisha abiria mwingine kuamua kumaliza sakata hilo kwa kumlipia nauli sh 300 abiria huyo.
Hata hivyo, baadhi ya abiria waliokuwa ndani ya daladala hiyo wengi walionekana kuiona kwa mara ya kwanza noti hiyo hali iliyosababisha kila mmoja wao kutaka kuishika.
Mmoja alisikika akisema, “Kwa kweli noti hizi za viwango vya kimataifa maana ukiwa na sh 1,000,000 kwa namna zilivyo utadhani umebeba fedha kidogo sana,” alisikika mmoja wa abiria hao.
Mbali na kondakta huyo kuonekana kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya ujio huo mpya wa noti za Tanzania, baadhi ya wafanyabiashara wa mazao katika masoko ya Mbalizi na maeneo mengine wamekuwa wakisita kupokea fedha hizo mpya kwa kutokuwa na imani nazo.
Melezo ya elimu kwa umma yaliyotolewa na Benki kuu yalifafanua kuwa noti mpya zitaingia kwenye mzunguko sanjari na noti za zamani mpaka hapo zitakapotoweka taratibu na hatimaye kuisha kabisa kwenye mzunguko.
0 comments