Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sitta ashtakiwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ameingia kwenye mgogoro mwingine na CCM baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, kuwasilisha hoja akitaka chama kimwadhibu.
Waziri Sitta na Mgeja walianza kuingia kwenye malumbano Desemba 19, mwaka jana, baada ya Sitta kueleza kuwa aliondolewa nafasi ya uspika wa Bunge kutokana na hila za viongozi ambao walishindwa kuhimili kasi ya utendaji wake kwenye chombo cha kutunga sheria.

Sitta, ambaye alipata umaarufu baada ya kuliongoza Bunge la Tisa kwa mafanikio, alitoa kauli hiyo wiki chache baada ya kukaririwa na vyombo vya habari, akisema bayana kuwa kuilipa kampuni tata ya Dowans fidia iliyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC), ni sawa na kuhujumu uchumi.

Kauli hiyo ya Waziri Sitta ilimkera Mgeja, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, huku akimtaka kuifuta vinginevyo angewasilisha hoja binafsi CCM kuomba achukuliwe hatua.

Hata hivyo, msimamo huo wa Mgeja ulionekana kutomtisha Sitta ambaye alieleza kuwa anaiubiri kwa hamu hoja hiyo. Juzi, Mgeja alisema tayari amewasilisha hoja hiyo kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ili ijadiliwe kwenye kikao cha Nec hivi karibuni. Mgeja alisema katika hoja hiyo anaitaka CCM kumwadhibu Sitta kwa kukiuka sheria, taratibu na kanuni za chama kwa kuituhumu Kamati Kuu ya CCM, kinyume na taratibu kupitia vyombo vya habari.

“Tayari nimewasilisha barua hiyo kwa Katibu Mkuu. Msingi wa hoja yangu ni kutaka kurejesha maadili na upatanisho ndani ya CCM," alisema Mgeja. Alisema hana ugomvi na Sitta na kwamba, ni kiongozi anayemheshimu.

 “Sina ugomvi na mzee Sitta na ninamheshimu, wala sipingani na hoja yake hiyo ingawa kutofautiana kwa hoja ni kitu cha kawaida,” alisema. Alisema lengo la kuchukua hatua hiyo, ni baada ya kuona sheria, kanuni, taratibu na maadili ndani ya chama hicho vinakiukwa na kusisitiza kuwa, ni wajibu wa chama kuchukua hatua ya kurekebisha. “Ukiona behewa moja la treni linaacha njia na kupita pembene ni kazi ya  mafundi wa treni kulirudisha kwenye reli, ndipo safari iendelee.

Mimi kama kiongozi nimetimiza wajibu na kiapo changu kwa chama kwa kuchukua hatua ili kurejesha mwenendo wa CCM,” alisema Mgeja.  Makamba alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema bado hajapata barua na kwamba, hawezi kuongelea suala hilo hadi atakapolipata rasmi. Mwisho
Tags:

0 comments

Post a Comment