Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CCM yaisadia CHADEMA kushinda Hai

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshinda uchaguzi na kufanikiwa kuongoza Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Diwani wa Kata ya Machame Kaskazini, Clement Kwayu, ndiye alishinda nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo. Hai ni Halmashauri ya sita kuongozwa na CHADEMA nyingine ni Kigoma Ujiji, Mwanza, Musoma Mjini, Karatu, Moshi Mjini.
Kabla ya jana, uchaguzi huo ulishindikana na kuahirishwa mara mbili, baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Melkizedeck Humbe, kukataa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, aliyeruhusu wabunge wawili wa Viti Maalumu mkoani Kilimanjaro kupitia CHADEMA, Lucy Owenya na Grace Kiwelu, kuwa ni wajumbe halali wa baraza hilo.
Kwayu alipata kura 12 dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ally Mwanga, aliyepata kura 10. Nafasi ya makamu mwenyekiti haikupata mshindi, kwani walifungana kwa kura, hata baada ya kurudiwa.
Baraza la Madiwani wa wilaya hiyo, lilikubaliana na kauli moja kuwa waliokuwa wakigombea nafasi hiyo waongoze kwa kuachiana.
Atakayeanza kuongoza kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti katika mwaka wa kwanza ni Diwani wa Kata ya Weruweru, Adris Mandrai (CCM). Baadaye atafuata Diwani wa Kata ya Masama Kati, Deogratius Kimaro (CHADEMA).
Hata hivyo, matokeo hayo yameibua mtafaruku ndani ya CCM baada ya viongozi wa chama hicho kudai kuwa kuna diwani wao mmoja ambaye amewasaliti na wanamjua. Walidai watamfukuza kwenye chama.
Kila chama kilikuwa na wajumbe 11, hali iliyokuwa inaviweka katika wakati mgumu wa kupata mshindi.
Awali, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa kikao hicho, aliwataka watendaji wa serikali kujifunza taratibu za uongozi.
Alisema kuwa kitendo cha watendaji kukaidi maelekezo ya Mwanasheria Mkuu ni ushahidi kwamba watendaji hao hawajui taratibu za uendeshaji wa shughuli za kila siku ndani ya serikali yao.
Tags:

0 comments

Post a Comment