Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Baada ya Arusha sasa yawa zamu ya UDOM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAKATI Jeshi la Polisi likiendelea kushutumiwa na kulaaniwa kwa kufanya mauaji na kusababisha uvunjifu wa amani jijini Arusha hivi karibuni, jana jeshi hilo lilitumia tena mabomu kuwasambaratisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kushinikiza kutatuliwa kwa madai yao.
Wanafunzi waliogoma na kuanza maandamano kuelekea ilipo ofisi ya Waziri Mkuu mkoani hapa ni wa kitivo cha elimu ambao kimsingi wanalalamikia kile waliochokiitaubabaishaji unaofanywa na serikali katika utoaji wa fedha za mikopo kwa wanafunzi pamoja na tatizo la maji chuoni hapo.
Wanafunzi hao walieleza kuwa hawataki kuongea na kiongozi yeyote badala yake wanataka kuonana na waziri mkuu pekee ili aweze kutoa ufafanuzi wa suala lao kwani ubabaishaji wa serikali umekithiri.
Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kilitembeza bakora kwa wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kupiga mabomu ya machozi katika jitihada zake za kuwatawanya wanafunzi hao pamoja na kuvunja maandamano hayo.
Maandamano hayo yalianza saa 10 alfajili ya kuamkia leo yakitokea Ng'ong'onha ambapo pia waliharibu mali nyingi zikiwemo taxi ambazo zilifika chuoni hapo kwa ajili ya kuchukua wanafunzi na kuwapeleka mjini.
Wakati wakiandamana kuelekea kwenye ofisi ya Waziri Mkuu, FFU walikuwa wametanda katika kona zote za chuo hicho huku wakiwasubiri watokee.
Hata hivyo, hawakufanikiwa kufika mbali kwani FFU walianza kuwatawanya kwa kuwarushia mabomu ya machozi huku nao wakijibu kwa kurusha mawe.
Akizungumzia mgomo huo rais wa wanafunzi chuoni hapo, Muta Frederick, alisema sababu ya kuandamana ni kucheleweshewa fedha zao za mikopo.
Pia hawamtaki Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, ProfesaShabaan Mlacha, kwa sababu amekuwa ni chanzo kikubwa cha migogoro.
Alisema naibu huyo amekuwa hashughulikii ipasavyo madai ya wanafunzi yanayopelekwa ofisini kwake na badala yake anayakalia.
Aidha Fredrick alisema tatizo lingine ni ukosefu wa huduma muhimu kama vile maji na fedha za mafunzo kwa vitendo ambapo uongozi wa chuo umekuwa hautoi maelezo ya kutosha.
Baada ya kukurupushwa na FFU wanafunzi hao walikusanyika katika viwanja vya Nyerere Square huku wakiimba wimbo wa kumuenzi Baba wa Taifa wakiwa wamesimamiwa na askari hao na kuongezea vionjo kwa kudai kuwa wataendelea na mgomo hadi kieleweke la sivyo wauawe kama Arusha.
Wanafunzi hao pia wamewapiga waandishi wa habari waliotaka kupata habari zao ambapo mwandishi wa gazeti la Mwananchi Habel Chidawali amejeruhiwa na kuchaniwa nguo alizovaa pamoja na begi alilokuwa amebebea kamera lengo likiwa ni kutaka kumnyang'anya kamera hiyo aliyokuwa akifanyia kazi.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya kujinasua mikononi mwa wanafunzi hao mwandishi huyo alisema kuwa alikuwa katika harakati za kutafuta habari ndipo alipokutana na wanafunzi hao waliomtaka awape kamera kabla ya kumshushia kipigo.
"Waliponitaka niwape kamera niligoma kwa sababu sikujua wanaitaka kwa kazi gani na usalama wangu ungekuwa vipi, baada ya kukataa kuwapa kamera walianza kunirushia mawe huku wengine wakinipiga ngumi, mateke na makofi na kunichania nguo" alisema mwandishi huyo.
Kufuatia kitendo hicho mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Dodoma Rahel Chizoza ametoa tamko la chama la kulaani kitendo hicho na kutangaza kutoifanya kazi yoyote na wanafunzi wa chuo cha UDOM kwa wakati huu.
"Siyo mara ya kwanza kwa wanafunzi hawa kuleta vitendo vya uvunjifu wa amani kwa wanahabari, shida ni ya kwao na siyo ya waandishi upo uwezekano wa kufanya kazi bila hata kuandika habari za UDOM, hivyo kwa muda huu tunasitisha kufanya kazi na wanafunzi hao" alisema.
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini, Jonn Tuppa, alifanya juhudi za kutaka kuwatuliza lakini walionekana kutokubaliana naye hadi alipowahakikishia kuwa FFU hawatawapiga kwa mabomu tena.
Wakati hayo yakitokea, nao wahadhiri wa chuo hicho wameanzisha mgomo wa kutoingia darasani na kufanya kile walichokiita mkutano endelevu kujadili hatma ya maslahi yao ikiwa ni pamoja na mshahara mpya na fedha za kujikimu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOMASA), Paul Loisulie, aliiambia Tanzania Daima wakati wa mkutano huo kwamba wataendelea hadi hapo atakapokuja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuwasikiliza.
Alisema uongozi wao tayari umeshaandika barua kwa Rais Kikwete na kupeleka malalamiko yao ambapo nakala wamezituma kwa Ofisi ya Wizara ya Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya UDOM.
Alisema kuwa wahadhiri hawana mpango wa kugoma lakini hawataingia madarasani mpaka hapo watakapopata ufumbuzi wa suala lao kutoka kwa rais.
"Sisi hatujagoma ila tuko kwenye mkutano endelevu na hatutaingia madarasani hadi Rais Kikwete aje hapa ili tumpe malalamiko yetu" alisema mwenyekiti huyo.
Alisema tangu mshahara mpya uanze kulipwa wao kama wafanyakazi wa UDOM hawajawahi kupata fedha hizo ikiwa ni pamoja na zile za kujikimu ambazo ni haki ya kila mwajiriwa.
Loisulie alisema licha ya Hazina kutoa fedha hizo na kuufikia uongozi wa UDOM bado wao kama waajiriwa hawajawahi kulipwa mshahara huo mpya.
"Sisi kama viongozi tulijipanga na kwenda kwa uongozi kuulizia suala hilo, lakini walitujibu kuwa mshahara ulikosewa ndiyo maana haujaanza kulipwa" alisema.
Wahadhiri hao pia wamelalamikia kupunguzwa kwa mishahara yaotofauti na inavyotolewa na Hazina.
Alisema tatizo hilo waliligundua baada ya mshahara kutolewa na UDOM na kupewa'Pay Slip' badala ya kupewa'Salary Slip' inayotoka HAZINA.
Alisema licha ya kuwauliza viongozi wao walishindwa kuwapa jibu sahihi na badala yake walikuwa wakirushiana mpira na Hazina jambo ambalo linawafanya wafanyakazi washindwe kutambua kinachoendelea.
"Tulienda hazina na kufuatilia kwa ukaribu zaidi lakini tukaambiwa kuwa hawana taarifa zozote kuhusiana na suala hilo na kutuambia tatizo lipo kwenye uongozi wetu, lakini huku nako wanakataa" alisema.
Wakati mgomo UDOM, wanafunzi wa chuo kikuu cha St. Johns kilichopo chini ya kanisa Anglikana nao walitishia kugoma wakiulalamikia uongozi wa chuo hicho kutumia pesa za wanafunzi za kununulia vifaa kinyume na maelekezo.
Kwa upande wake rais wa wanafunzi kitivo cha sayansi alidai kuwa uongozi umekuwa ukitumia pesa za wanafunzi bila maaelezo yoyote na wanapohoji juu ya matumizi ya pesa hizo wamekuwa hawapewi maelezo ya kutosha.
Alisema wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi wanatakiwa kupewa sh laki 1.8 kila mwaka lakini uongozi wa chuo umekuwa ukiwapatia kiasi cha sh 60,000 tu.
Afisa uhusiano wa chuo hicho Karim Meshack akiongea kwa niaba ya mkuu wa chuo alisema madai ya wanafunzi haoni ya kweli lakini chuo kimeamua kuwapatia pesa hizo ili waweze kununua vifaa wenyewe badala ya kununuliwa na chuo.
Tags:

0 comments

Post a Comment