SERIKALI ya Tanzania inalifanyia uchunguzi shirika la utangazaji la Uingereza (BBC), ikilishuku shirika hilo la Serikali ya Uingereza kwamba linafanya shughuli za uchochezi nchini. Halikadhalika, Serikali pia inafuatilia kwa karibu nyendo za Radio ya Kimataifa ya Ufaransa (Radio France International, RFI), ili kubaini iwapo hatua yake ya kuanzisha Idhaa yake ya Kiswahili inayotangazia kutoka jijini Dar es Salaam haina ajenda ya siri ndani yake.
Kitengo cha BBC kinachotiliwa shaka na Serikali ni kile cha mfuko wa misaada wa matangazo yake ya kimataifa, yaani BBC World Service Trust (BBCWST), ambacho mapema mwaka jana kiliingia mkataba wa kulisaidia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa mafunzo na vifaa. Mfuko huo wa misaada ya BBC hivi sasa unafanya kazi katika nchi nyingi duniani hasa zile zinazoendelea zikiwemo nchi kadhaa za kiafrika kwa kutumia fedha wanazozipata kutoka kwa wahisani wakisadia kuimarisha utangazaji wa kisasa.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa mkataba wa baina ya TBC na BBCWST ni wa miaka mitano na unafadhiliwa na fedha kutoka Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DFID). Nchi nyingine za Afrika zenye mkataba kama huo ni Angola na Siera Leone. Hatua ya kuchunguza ushirikiano huo wa BBCWST na TBC umo kwenye maelekezo ya barua ulizoandikiwa uongozi wa juu wa TBC, mwezi Novemba, 2010.
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo katika moja ya barua ya maelekezo yake, alimtaka Mwenyekiti wa Bodi ya TBC, Wilfred Nyachia kumpa maelezo ya kina kuhusu mikataba ya mashirika hayo.
Mmoja wa maofisa waandamizi katika wizara ya Habari, Vijana, na Michezo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kumekuwepo na wasiwasi serikalini ya kwamba BBCWST limehusika katika kuifanya TBC itangaze matukio yaliyoikera wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa jana.
Kadhalika kumekuwepo na hisia miongoni mwa watu kwamba matangazo ya uchaguzi ya TBC ndiyo yaliyoifanya Serikali iamue kutomuongezea mkataba mwingine aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Tido Mhando.
Mhando hakuongezewa mkataba na Serikali licha ya tathimini isyo rasmi ya wadau wa habari nchini kuonyeha kuwa chini ya uongozi wake shirika hilo limeweza kufanya kazi yake bila kuegema upande wowote hasa wakati wa uchaguzi, taarifa ambayo pia imo kwenye ripoti mbalimbali za waangalizi wa kimataifa na kitaifa wa uchaguzi huo. Hata hivyo, akihutubia maafisa wa habari wa wizara mbalimbali mjini Mbeya mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, na Michezo, Seth Kamuhanda alisema Serikali ilikuwa ikiyafanyia uchunguzi mashirika ya habari ya kimataifa ambayo yamekuwa yakiendesha ama kutangaza mambo ya uchochezi.
Radio ya RFI inayomilikiwa na Serikali ya Ufaransa, ilianza kutangaza matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili kupitia radio ya TBC FM katikati ya mwaka uliopita lengo likiwa ni kusaidia kusambaza lugha ya Kiswahili kwenye nchi nyingine za kiafrika ambako radio hiyo husikika. Maafisa kadhaa wa Serikali walihudhuria sherehe za uziinduzi wa kituo hicho mwezi Septemba mwaka jana katika hafla iliyofanyika katika ofisi za ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam. Baada ya maelekezo kutoka kwa Luhanjo, uchunguzi wa Mwananchi umegundua kuwepo kwa vikao mfululizo karibu kwa mwezi mmoja na nusu sasa kuhusu suala hilo, ambavyo vinawahusisha wajumbe wa kamati mbalimbali za bodi ya TBC.
Mwenyekiti wa Bodi ya TBC Wilfred Nyachia, pamoja na kulijadili kwa kirefu suala hilo kwenye kikao kamili cha bodi kilichofanyika Desemba 21 mwaka 2010, pia amekuwa na mfulilizo wa vikao vingine. Wiki mbili zilizopita Nyachia alizungumza na wajumbe wote wa Bodi yake mmoja, mmoja, ana kwa ana na mapema wiki iliyopita, Mwenyekiti huyo akiwa pamoja na baadhi ya wajumbe wa bodi walikutana na viongozi wa BBCWST na RFI na baadaye wakafanya mazungumzo na baadhi ya viongozi waandamizi wa TBC. Wajumbe wengine wa bodi waliokuwepo kwenye vikao hivyo ni pamoja na Balozi Ben Mosses, Profesa Henry Mgombello na Kiongozi wa idara moja nyeti ya Serikali.
Mwenyekiti wa Bodi ya TBC Wilfred Nyachia, pamoja na kulijadili kwa kirefu suala hilo kwenye kikao kamili cha bodi kilichofanyika Desemba 21 mwaka 2010, pia amekuwa na mfulilizo wa vikao vingine. Wiki mbili zilizopita Nyachia alizungumza na wajumbe wote wa Bodi yake mmoja, mmoja, ana kwa ana na mapema wiki iliyopita, Mwenyekiti huyo akiwa pamoja na baadhi ya wajumbe wa bodi walikutana na viongozi wa BBCWST na RFI na baadaye wakafanya mazungumzo na baadhi ya viongozi waandamizi wa TBC. Wajumbe wengine wa bodi waliokuwepo kwenye vikao hivyo ni pamoja na Balozi Ben Mosses, Profesa Henry Mgombello na Kiongozi wa idara moja nyeti ya Serikali.
Nyachia alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alailiambia gazeti hili kuwa hana habari za kuwepo kwa hali hiyo, hajui lolote na wala hajaambiwa. Nyachia alisema katika bodi hiyo ya TBC yeye ni mwenyekiti wa vikao tu na si mtendaji hivyo, hilo linaweza kuwepo na yeye asijue na si ajabu. "Sina habari ya mambo hayo, kama yapo unajua siku hizi mambo si kama zamani hakuna 'executive chairman' (Mwenyekiti mtendaji) enzi za mwalimu kama walivyokuwa wakina Mwaikambo NBC," alisema Nyachia.
Aliongeza,"Mimi ni mwenyekiti wa vikao, si executive, inawezekana lipo, lakini mimi sijui hilo." Mjumbe mmoja wa bodi ya TBC ambaye naye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema baadhi yao hawaelewi tatizo hasa ni nini. “Ni nani ambaye hafahamu umahiri wa BBC kwenye shughuli za utangazaji, na ni nani ambaye hangependa wafanyakazi wake wapatiwe mafunzo na BBC?", alihoji mjumbe huyo. Aliongeza, “Kama kuna kitu kingine kizuri ambacho Tido ameifanyia TBC wakati wa uongozi wake basi ni ushirikiano huu aliouunda na mwajiri wake huyo wa zamani yaani BBC”.
Imefahamika ya kwamba uchunguzi wote huo umefanywa kwa nguvu, baada ya kumalizika kwa mkataba wa Tido, huku taarifa nyingine zikidai kwamba Mkurugenzi Mkuu huyo wa zamani wa TBC ambaye anatajwa kuwa mhusika mkuu katika suala hilo huku alihusishwa katika mchakato unaoendelea hivi sasa. Baadhi ya wafanyakazi wa TBC waliozungumza na Mwananchi kuhusu hali ya TBC kwa sasa, walisema wasiwasi mkubwa uliopo ni muelekeo mzima wa hali ya uongozi wa shirika hilo.
Walisema awali hali ya shirika ilikuwa imeanza kupata mwelekeo mzuri unaoeleweka, lakini sasa haifahamiki ni nani mwenye kufanya uamuzi kuhusu shirika hilo la umma ambalo miaka mitatu tu iliyopita ilifanya sherehe kubwa ya uzinduzi, kutoka kuwa taasisi ya Serikali na kuwa shirika kamili la umma la Utangazaji, mgeni rasmi akiwa Rais Jakaya Kikwete. Kwenye hotuba yake ya uzinduzi huo, Rais Kikwete alisema mabadiliko hayo maana yake ni kuwa kuanzia wakati huo TBC ni shirika la utangazaji la umma wa Watanzania wote, litakaliokuwa na uamuzi wake wenyewe na hasa katika masuala ya uandishi wa habari kwa kuzingatia misingi ya weledi na linalotarajiwa katika muda usio mrefu kujitegemea wenyewe kimapato.
“Lakini sasa tunaona mambo yanakwenda kinyume na hayo, labda Rais pekee ndiye aliyejua ni nini maana ya mabadiliko aliyoyafanya maana kwa sasa amri nyingi zinatokea wizarani,” waliongeza, huku wakitoa mfano wa kipindi maalum cha ghasia za hivi karibuni zilizotokea mkoani Arusha kilichorushwa hapo mwishoni mwa wiki. Uchunguzi unaonyesha kwamba kwamba kipindi hicho kilisimamiwa na mkurugenzi wa idara nyeti ya Serikali aliyewataka kutumia vifaa vya shirika hilo kukiandaa kisha kutangazwa siku ya Jumamosi na Jumapili na TBC1 pamoja na TBC Taifa.
Tayari kipindi hicho kimezua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi, huku wataalamu wa mambo ya habari wakisema haikuwa sahihi kutangazwa kipindi kilicholalia upande mmoja tu na kwamba kiweledi idara ya Polisi ingefanya mkutano na vyombo vyote vya habari na kutoa picha zote walizotaka kuonyeshea utetezi wao kuhusu tukio hili. Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa TBC, Joe Rugarabamu alipoulizwa alisema kurushwa kwa kipindi hicho ni matakwa ya polisi na kwamba walilipia kipindi hicho.
"Ile ni kama baada ya tukio upande mmoja umetoa maelezo yao nawe umekwenda kuwahoji polisi, nao wameeleza upande mmoja unaowahusu wao, walitaka kitoke na wamelipia," alisema Rugarabamu. Alipotakiwa kueleza wamelipia kiasi gani cha fedha, Rugarabamu alisema, "Siwezi kusema kwa sasa kwani nipo nje ya ofisi". Alipotakiwa kuzungumzia hatua hiyo ya Serikali kuwachunguza na kutaka kuwafukuza nchini, mkurugenzi wa RFI nchini, Victor Robert Wile alisema hawaweze kukurupuka na kulizungumzia hilo hadi watakapopata taarifa kamili juu ya kuwepo kwa mkakati huo wa Serikali.
"Hatuwezi kulizungumzia hilo, sisi tuna msemaji wetu, tukipata hilo kwa undani tutazungumzia, lakini sasa hatuwezi kukurupuka," alisema Victor Robert Wile. Hivi karibuni, wakati wa sherehe za Mapinduzi Zanzibar, kwa kuzingatia mabadiliko mazuri yaliyotokea tangu kuanzishwa kwa TBC, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo ilitangaza kuanzisha kwa Shirika lake la Utangazaji la Zanzibar, kwa kuziunganisha Sauti ya Tanzania Zanzibar na Televisheni Zanzibar.
0 comments