Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mwandosya: Maji ya Victoria kufika Tabora 2014

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


WAZIRI wa Maji ,Profesa Mark Mwandosya, amesema  serikali itatekeleza mradi mkubwa wa kupeleka maji ya Ziwa Viktoria katika makao makuu ya Mkoa wa Tabora kabla ya mwaka 2014.
 
Waziri Mwandosya aliyasema hayo juzi mjini Tabora kwenye majumuisho ya ziara yake ya siku sita mkoani humo, kwa ajili ya kuona hali halisi ya maji katika mkoa ambao umekuwa na shida kubwa ya maji.
 
Alisema hakuna njia ya kumaliza tatizo kubwa linaloukabili Mji wa Tabora kupata maji ya uhakika isipokuwa kutumia njia hiyo ambapo alibainisha kwamba hatua za awali zimekwishaanza ijapokuwa muda zaidi unahitajika.
 
Waziri Mwandosya, alisema kinachosumbua kwa sasa ni jinsi gani maji yafike Tabora kutoka ama Kahama au Isaka kuja Tabora na kazi inayofanyika sasa ni kuona njia ipi bora na Miji ya Nzega, Igunga, Bukene inapataje maji kutoka katika Ziwa Viktoria.

 Alisema kimsingi uamuzi muhimu kuhusu suala hilo umefanyika na kinachobakia ni utekelezaji wa hatua hiyo, kwani serikali inajua ugumu wa tatizo la maji unaoukabili mji huo na kwa kipindi kirefu tumekuwa tunahangaikia hilo.

Akizungumzia udhaifu wa vyanzo vya maji katika Mkoa wa Tabora, alisema unatokana na hali ya mkoa kuwa kwenye ukanda mgumu wa upatikanaji wa maji na kwamba katika baadhi ya visima kuna maji yenye chumvi nyingi hivyo kutoweza kutumika kwa matumizi ya binadamu.

Alisema Pamoja na tatizo hilo njia pekee ya kulikabili ni kutegemea maji ya mabwawa ambayo nayo kwa siku za karibuni yamebainika kutotosheleza mahitaji ya maji katika Mji wa Tabora kutokana na mabwawa hayo ya Kazima na Igombe kuanza kukauka na kujaa matope.

“Hivyo ndugu zangu njia bora iliyopo ni kuvuta maji kutoka Ziwa Viktoria na  tuendelee kutunza vyanzo vya maji tulivyonavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mabwawa yetu yanaishi muda mrefu zaidi”, alisisitiza.

Awali wakazi wa Manispaa ya Tabora, walimlalamikia Waziri wa Maji kwamba Mamlaka ya Majisafi na Majitaka katika Manispaa ya Tabora ( Tuwasa) inatoa huduma mbaya ya maji kiasi ambacho kinawakatisha tamaa wananchi kupata huduma nzuri.

Walisema baadhi ya maeneo yamekuwa yakipata maji saa nane usiku, mgao mdogo wa maji kwa siku nane tu kwa mwezi na mengine yakikosa maji huku mita zikisoma hewa tu na wananchi wakitakiwa kulipia ankara za mwezi ambazo ni Sh 15,000.
Tags:

0 comments

Post a Comment