Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mpango wa chakula Marekani kuineemesha Tanzania

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
BALOZI wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zinazoendelea ambazo zitafaidika na mpango maalum wa kuendeleza sekta ya kilimo unaolenga kuwa na uhakika wa chakula kuanzia ngazi ya familia.
Lenhardt aliasema hayo alipokuwa akizungumza na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati alipokutana naye ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar es Salaam jana.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Lenhardt alisema mpango huo unaojulikana kwa jina la ‘Feed the Future’ unazihusisha nchi za Ghana, El Salvador, Philippines na Tanzania.
Kwa mujibu wa balozi huyo mpango huo unalenga kukuza kiwango cha uzalishaji wa mazao ya kilimo kupitia vichocheo maalum ili kupunguza njaa, umaskini na utapiamlo.
“Tanzania ni moja ya nchi zenye uwezo wa kuboresha kilimo na kuwa na uhakika wa kulisha watu wake, kinachohitajika ni zana za kisasa na teknolojia ya uhakika kwa kutumia fursa ilizonazo kama vile hali nzuri ya hewa, ardhi ya kutosha ambapo tunaamini tunaweza kusonga mbele sana katika uzalishaji wa chakula…,” alisema.
Hata hivyo Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Hilary Clinton wanaunga mkono mpango huo ambao mbali na kulenga kukuza uzalishaji wa chakula kupitia kilimo cha umwagiliaji pia unalenga upatikanaji wa chakula kwa wanawake na watoto.
Waziri Mkuu aliishukuru serikali ya Marekani kwa kuijumuisha Tanzania katika mpango huo muhimu na kusema kwamba anaamini utasadia juhudi za serikali za kukuza kilimo ili kuondoa umaskini kwa Mtanzania na taifa kwa ujumla.
Mpango huo pia unalenga kuwasaidia wakulima wadogo kwa kuwapa zana za kisasa na uhakika wa masoko ya mazao yao ambapo utawasaidia kuwa na nguvu ya kipato, kuongeza eneo la kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji utakaowawezesha kupanda hadhi kuondokana na umaskini,” alisema.
Katika hatua ningine, Waziri Mkuu alikutana na Balozi wa India nchini Kocheril Bhagirath ambapo katika mazungumzo yao walijadiliana zaidi masuala ya Kilimo Kwanza na hatua ambazo nchi hiyo imefikia katika kusaidia uagizaji wa matrekta Tanzania.
Pia Balozi Bhagirath alimweleza Waziri Mkuu kwamba mahusiano ya kibiashara baina ya Tanzania na India kwa mwaka 2010 yalikuwa mazuri kiasi cha kufikisha dola za Marekani bilioni 1.125 ikilinganishwa na dola milioni 960 za mwaka 2009.
Alisema kwa mujibu wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA) katika mwaka 2010 Tanzania imeuza India bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 230 wakati bidhaa zilizoagizwa kutoka nchi hiyo zinafikia dola za Marekani milioni 895.
Balozi huyo alizitaja bidhaa ambazo Tanzania imeuza kwa wingi India kuwa ni mazao jamii ya dengu, korosho na madini kwa kiasi kidogo.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema bado Tanzania inahitaji kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji na kwamba serikali inajipanga kutafuta njia za kuwawezesha wakulima wadogo kumiliki zana za kilimo cha umwagiliaji.
Tags:

0 comments

Post a Comment