SAKATA la uongozi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) limeingia katika hatua nyingine baada ya Rais Jakaya Kikwete kumwagiza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo kuunda Tume tatu zitakazoshughulikia madai ya msingi ya wahadhiri hao.
Agizo hilo lilitolewa katika taarifa ya maandishi iliyopatikana jana baada ya wahadhiri hao kusisitiza kutoingia madarasani hadi kero zao zitakaposhughulikiwa ikiwemo ya kutolipwa mishahara mipya iliyoanza kutolewa Novemba, 2010.
Kauli ya Rais imekuja siku chache baada ya wahadhiri wa UDOM kutaka kumwona Rais na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ili kuwaeleza madai hayo na kero nyingine zinazohusu ustawi wa chuo hicho.
Miongoni mwa tume zitakazoundwa ya kwanza itakuwa chini ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo itakua na kazi ya kukagua mishahara ya wahadhiri hao kazi iliyotarajiwa kuanza mapema kwa kukagua orodha ya mishahara ya ‘Pay roll’ za wafanyakazi wa chuo hicho.
Tume ya pili iliyoundwa ni ile ya Makatibu Wakuu ambayo itadadisi masuala mbalimbali yanayohusu UDOM ili kujua matatizo yaliyopo na chanzo chake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo tume ya nyingine inamhusisha Kamishna wa Vyuo Vikuu vya Tanzania ambayo itaangalia masuala mbalimbali na masomo ya taaluma.
Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, leo anatarajia kukutana na serikali ya wanafunzi pamoja na kuzungumza na wahadhiri wa chuo hicho kikubwa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loisulie Pinda, anakuja kushughulikia matatizo mbalimbali yanayojitokeza na yanayoendelea chuoni hapo.
Adiha, mwenyekiti huyo alisema wanaendelea na mkutano endelevu ambao pamoja na mambo mengine wanajadili namna ya kuufikisha mahakamani uongozi wa chuo chao.
0 comments