IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema kauli zinazopingana kutoka kwa viongozi wa serikali kuhusu madai ya katiba mpya zinaonyesha kwamba serikali ni dhaifu na kwamba viongozi hao hawana msimamo wa pamoja.
Amesema kitendo cha kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani pamoja na ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kupishana na tamko la Rais Jakaya Kikwete ambaye amebariki kuanza kwa mchakato wa kuandikwa katiba mpya ni dosari kubwa ndani ya serikali na taifa.
Kombani ambaye ndiye waziri mwenye dhamana ya Katiba alisema kuundwa kwa Katiba mpya kwa sasa hakutawezekana kwani sio muhimu na kwamba serikali haina bajeti ya kushughulikia katiba mpya.
Waziri huyo aliyeingia madarakani kuiongoza wizara hiyo kwa mara ya kwanza, alisema serikali itaendelea kufanya marekebisho ya sheria hiyo mama wakati wowote inapolazimika.
Wakati Kombani akitoa kauli hiyo Jaji Frederick Werema alisema haitawezekana kuandikwa kwa katiba mpya bali linalowezekana ni kufanya marekebisho kwa kuondoa au kuongeza mambo fulani kwenye katiba inayotumika hivi sasa ambayo watu wa kada mbalimbali nchini wanataka ibadilishwe.
Lakini jana akizungumza na Mwananchi Kafulila alisema, “ Kitendo cha Waziri wa sheria, Mwansheria mkuu na Rais Kikwete ambao wapo ndani ya serikali moja kutofautiana hadharani kwenye suala nyeti kama la Katiba ni kielelezo kwamba tuna serikali dhaifu,”
Aliongeza, “Serikali sio moja ndio maana hakuna msimamo mmoja, hali hii inatia mashaka na kuongeza wasiwasi katika mchakato mzima wa ufanisi wa utendaji kazi wa serikali, “.
Alifafanua kuwa hivi karibuni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja nao walitoa msimamo tofauti kuhusu hoja nyeti ya kesi ya Dowans na Tanesco.
Kafulila ambaye ametangaza kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhoji sababu zinazoifanya serikali isiwajibike kwa kuliingizia taifa hasara ya mabilioni ya fedha kwenye sekta ya nishati ya umeme alisema
“Ngereja alisema maoni ya waziri Sitta ni sawa na maoni ya Watanzania wa kawaida, akasahau kuwa wote ni wajumbe wa cabinet (Baraza), hiki ni kilelezo kuwa serikali hii ina mgongano mkubwa wa kiuongozi,”.
You Are Here: Home - - Mbunge David Kafulila adai viongozi serikalini hawana msimamo wa pamoja
0 comments