IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ALIYEWAHI kupambana na Profesa Ibrahim Lipumba kwenye kinyang'anyiro cha kugombea nafasi ya mwenyekiti wa CUF,
Profesa Abdallah Safari, amejivua uanachama wa chama hicho.
Taarifa ambazo zilipatikana jana na baadaye kuthibitishwa na Profesa Safari, hazikubainisha sababu za kujitoa kwake kwenye chama hicho na kwamba, anapanga kuanika hadharani keshokutwa.
“Pamoja na kwamba zipo sababu za mimi kufikia uamuzi huu, lakini kwa leo (jana) siwezi kueleza chochote zaidi ya kutangaza nimejiondoa CUF,’’ alisema Profesa Safari na kuongeza: “Kesho kutwa (Alhamisi) nitatangaza rasmi azma yangu ya kujivua uanachama wa CUF.’’ Profesa Safari ambaye ni mwanazuoni aliyebobea kwenye taaluma ya sheria, alijiunga CUF mwaka 2005 na Februari 2009, aliwania uenyekiti na Profesa Lipumba akaambulia ushindi kura sita.
Alisema amefikia uamuzi wake huo kwa utashi wake, bila kushinikizwa na mtu. “Napenda wananchi waelewe kuwa uamuzi huu, nimeufikia bila shinikizo lolote,’’ alisema Profesa Safari.
Hata hivyo, Profesa Safari alieleza kuwa pamoja na kung'atuka kwake CUF, ataendelea kuwa mwanasiasa bila kueleza atashabikia chama atakachoshabikia. Uamuzi huo ameufikia ikiwa ni takriban mwaka mmoja na nusu baada ya kuangushwa vibaya kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa CUF na Profesa Lipumba aliyepata kura 646.
Kufuatia matokeo hayo, Profesa Safari aliwashtumu wajumbe wa mkutano mkuu kuwa, walimdhalilisha na angeandaa kitabu kueleza udhalilishaji huo. Februari 23, 2009 wakati Profesa Safari akijieleza katika mkutano mkuu wa kuchagua mwenyekiti wa CUF, wajumbe walikuwa wakimzomea na baadaye kumrushia maswali yaliyomtingisha, ikiwamo kumtaka kutaja jina la katibu wa tawi lake. “Nimedhalilishwa; nimezomewa; nimeulizwa maswali ya kipuuzi.
Ule ni uhuni hakuna kitu pale,” alisema Profesa Safari na kuongeza: “Wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF wamepotosha na kuharibu maana ya demokrasia ndani ya CUF na kutumia vibaya nafasi hiyo ya kuchagua viongozi.” Alipobanwa kueleza iwapo anafikiria kuwania tena nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho, Profesa Safari alisema hawezi na hana nia ya kuwania uongozi wa chama hicho.
Hata hivyo, taarifa ambazo zilikuwa zikisikika ni kwamba, Profesa Safari alikuwa haelewani na uongozi wa CUF hasa baada ya kuhoji taratibu zilizotumika kati ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume kusaini mkataba wa siri kuunda ya umoja.
You Are Here: Home - - CUF kumekucha. Profesa Safari ajivua Uanachama CUF
0 comments