Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Pinda na Slaa kuna namna? Upigaji kura majimbo saba yaliyokuwa yamesalia wamalizika

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisalimiana na mgombea urais wa Chama Cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa furaha kubwa







UPIGAJI kura katika majimbo saba ambayo hayakufanya uchaguzi mwishoni mwa mwezi uliopita, jana yalifanya shughuli hiyo huku wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, huku idadi ndogo ya wapigakura ikijitokeza vituoni, hasa Bara.
Majimbo hayo ni Mpanda Mjini, Mpanda Vijijini na Nkenge ya Tanzania Bara ambako ushindani ulikuwa baina ya CCM na Chadema wakati kwenye majimbo ya Zanzibar ni Magogoni, Wete, Mwanakwerekwe na Mtoni ambako CCM iliendelea kupambana na CUF.

Majimbo hayohayakufanya uchaguzi Oktoba 31 kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa vifaa.
Taarifa kutoka kwenye majimbo hayo zinaeleza kuwa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa ni ndogo, isipokuwa kwenye majimbo ya visiwani Zanzibar na imeelezwa kuwa miongoni mwa sababu za kutokuwepo na watu wengi ni mvua.
Lakini ulinzi ulikuwa mkubwa ikilinganisha na idadi ya watu waliojitokeza. Askari wengi walimwagwa kufanya doria karibu na vituo vya kupigia kura ambako hata hivyo ni watu wachache waliojitokeza kupiga kura.
Doria hiyo ilijumuisha gari la maji ya kuwasha ambalo lilikuwa likirandaranda kwenye baadhi ya maeneo huku kukiwa na askari wa kawaida walioonekana kuwa tayari kukabiliana na vurugu zozote.
Kama vile haitoshi, kazi ya ulinzi iliongezewa nguvu na askari wa wanyama pori kutoka hifadhi ya Katavi kuhakikisha vurugu haziwezi kutokea.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa, Isunto Mantage alisema ulinzi huo ni wa kawaida na kwamba lengo lilikuwa ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na usalama.

Karani mwongozaji wa kituo cha kupigia kura cha Paradise kilicho katika Kata ya Kashauriri wilayani Mpanda, Didadi Nguo aliiambia Mwananchi kuwa zoezi la upigaji kura lilikuwa likifanyika vizuri.
Akizungumza na gazeti hili, msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mpanda Vijijini ambalo lilikuwa na vituo 94 vya kupigia kura, Mhandisi Emmanuel Kalobelo alisema kuwa zoezi hilo lilitarajiwa kunalizika kwa kwa amani na utulivu.
Alifafanua kwamba zoezi la kuhesabu kura litafanyika kwa haraka ni matokea ya uchaguzi huo yatolewa mapema iwezekanavyo.

Jimbo hilo la Mpanda Vijijini lina watu 35,911 waliosajiliwa katika daftari la wapigakura na watu wawili kutoka CCM na Chadema ndio waliokuwa wanawania ubunge. Wagombea hao ni Moshi Seleman Kakoso wa CCM pamoja na Masanja Mussa wa Chadema.
Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mpanda Mjini, Henry Haule alisema kuwa jimbo hilo lenye watu 42,215 walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura, lina wagombea watatu ambao ni Said Amour Alfi wa Chadema, Sebastian Kapufi wa CCM pamoja na Aron Ndimubenya wa CUF.
Katika jimbo la Nkenge mkoani Kagera uchaguzi umeonekana kutopewa umuhimu mkubwa na wananchi baada ya wasimamizi kutumia muda mwingi kupiga soga vituoni kutokana na kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapigakura.
Miongoni mwa mambo yaliyoonekana kuchangia kuzuia watu wengi kujitokeza kupigakura ni mvua iliyonyesha kwa wastani wa saa moja.

Ulinzi uliongozwa na askari mgambo kwenye vituo vya kupiga kura na hata hivyo hawakuwa na kazi kubwa kwa sababu hakukuwepo na hamasa kubwa ya kupiga kura ambayo mara nyingi huzaa vurugu.

Katika kituo cha Chekechea Kabwela 'A' nje kidogo ya mji wa Bunazi, hadi saa 4:00 asubuhi ni watu 19 tu waliokuwa wamejitokeza kati ya watu 483 waliojiandikisha. Hadi mwisho, wakati wa zoezi la kuhesabu kura, ilielezwa kwamba waliojitokeza walikuwa 38 tu katika kituo hicho.
Karani mwongozaji wa kituo hicho, David Matungwa aliiambia Mwananchi kuwa kulikuwa hakuna mategemeo makubwa ya kupata wapigakura wengi zaidi kwa sababu hata katika uchaguzi wa rais na madiwani uliofanyika mwezi uliopita, walijitokeza wachache.

Hali ya wananchi kuonekana kama wanasusia uchaguzi huo ilionekana pia katika kituo cha Shule ya Msingi ya Mushasha ambako hadi majira ya saa 3:00 ni wapiga kura saba tu waliokuwa wamejitokeza kati ya watu 362 walioandikishwa.
Nao mawakala wa vyama vya siasa Alistides Tiba na Emiliana Fotidas waliohojiwa katika vituo vya sekondari ya Bunazi walionyesha wasiwasi wa mshindi wa nafasi hiyo kuchaguliwa kwa idadi ndogo sana ya kura kutokana na wananchi kutoonyesha mwamko wa kupiga kura.

"Wananchi wamekata tamaa kutokana na matokeo ya uchaguzi uliopita, uhamasishaji haukuwepo na hata uchaaguzi uliopita ulipoisha hakuna mgombea aliyeendelea na kampeini," alisema Alistides
Pia katika vituo viwili vilivyopo karibu na kituo cha polisi cha Kyaka wasimamizi walionekana kuendelea na mazungumzo huku idadi ndogo ya watu ikijitokeza kituoni.

Akizungumza na Mwananchi katika kituo cha Tarafani 'A', mjumbe kutoka Tume ya Uchaguzi (Nec), Mchanga Hassan alikiri kushuhudia idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza na kusema kati ya vituo vitatu walivyotembelea hadi saa 5:00 asubuhi ni wastani wa wapiga kura 16 kati ya 344 waliokuwa wamejitokeza.

Hata hivyo mjumbe huyo ambaye alikuwa na maofisa wengine wa tume hiyo kutoka makao makuu alisema asingeweza kuzungumzia sababu za kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapigakura kwa kuwa walikuwa wanaendelea kuzungukia vituo.
Habari zilizopatikana kutoka Kata ya Kanyigo zilieleza kuwa idadi kubwa ya askari ilipelekwa katika kata hiyo kutokana na kuenea kwa uvumi wa maandalizi ya wafuasi wa chama kimoja cha siasa kufanya vurugu kwa madai ya kupinga ushindi wa mmoja wa wagombea.

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Nkenge, Dk Isdory Mtalo alisema wapigakura 90,631 wameandikishwa katika jumla ya vituo 254, na katika uchaguzi wa madiwani na rais uliofanyika wiki mbili zilizopita ni wapigakura 42,074 tu waliojitokeza.
Kwenye majimbo ya visiwani Zanzibar, ulinzi mkali wa polisi ulitanda, lakini kuliibuka zogo kubwa kwenye kituo cha Shule ya Kinuni ambako baadhi ya wafuasi wa CUF walidaiwa kufanyiwa hujuma za kunyimwa haki ya kupiga kura.
Katika zogo hilo, sheha wa eneo hilo alijikuta akiambulia kipigo kutoka kwa wafuasi wa CUF kutokana na kutuhumiwa kushiriki kwenye njama hizo, ambazo walidai kuwa ni pamoja na kugawa vitambulisho kwa wapigakura hewa.

Kutokana na vurugu hizo mmoja wa watu waliokuwepo eneo hilo, Fakih Ali Bakari aliumia na ikabidi apelekwe Hospitali ya al-Rahma. Kwa mujibu taarifa zilizopatikana hospitalini hapo, Fakih alijeruhiwa kwa mapanga.
Habari zinasema kulikuwa na hali ya kutoaminiana miongoni mwa wafuasi wa CCM na CUF hasa kutokana na kuonekana kwa magari yaliyokuwa yamebeba idadi kubwa ya watu hivyo kudhaniwa kwamba walikuwa wakipelekwa kwenye majimbo yaliyofanya uchaguzi kuongeza idadi ya wapigakura.

CUF walishinda uchaguzi wa wajumbe wa baraza la wawakilishi katika majimbo ya Magogoni na Mtoni katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, huku CCM wakinyakua jimbo la Mwanakwerekwe lakini katika uchaguzi wa jana wa wabunge kila chama kilikuwa kikijitahidi kupata ushindi katika majimbo hayo bila kujali matokeo hayo.
Mratibu wa uchaguzi unaofanyika kisiwani Unguja, Pandu Mugunya alisema licha ya kasoro hizo uchaguzi uliendelea kama kawaida na matokeo yangetangazwa jana usiku.

Idadi ya wapiga kura katika majimbo hayo matatu ya kisiwani Unguja ni kati ya 8,000 na 9,000 kwa kila jimbo huku kukiwa na vituo 81 vya kupigia kura katika majimbo yote.
Licha ya ulinzi mkali, kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura majira ya asubuhi na mchana ijapokuwa idadi yao ilionekana kupungua majira ya jioni kabla ya vituo kufungwa kwa ajili ya kuhesabu kura.
Tags:

0 comments

Post a Comment