Obama awakutanisha mahasimu wawili wakuu wa Mashariki ya kati
Rais wa Marekani Barack Obama amewahimiza viongozi wa Israeli na Palestina wasiache fursa ya kupatikana kwa amani iwapite, wakati alipowaleta pamoja katika ikulu yake mjini Washington hapo jana. Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Palestina yanatarajiwa kuanza tena hii leo.
Rais Obama aliwaalika kwa chakula cha jioni waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, rais wa Misri, Hosni Mubarak na mfalme Abdullah wa Jordan katika ikulu yake hapo jana usiku, baada ya kufanya mazungumzo mbalimbali na viongozi hao wanne. Akizungumza kabla chakula hicho, Rais Obama ameeleza wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa juhudi mpya za amani kufaulu, mahali ambapo viongozi wengine wa Marekani waliomtangulia walishindwa. Hata hivyo amesema Marekani haitayumbishwa katika juhudi zake kuhakikisha usalama wa Israel.
"Marekani haitayumba katika kuunga mkono usalama wa Israel. Kuna wale watakaojaribu kufanya kila watakaloweza kuvuruga mazungumzo haya, lakini tutaendelea kuwa imara."
Waziri mkuu Netanyahu kwa upande wake ameahidi kutafuta makubaliano ya kihistoria kati ya Waisraeli na Wapalestina, yatakayosaidia kufikia suluhisho la amani la mzozo wa Mashariki ya Kati uliodumu muda mrefu.
Netanyahu amesema anaamini amani inawezekana na kumuita rais Abbas kama mshirika wake katika kutafuta amani.
"Tunatafuta amani itakayomaliza kabisa mzozo kati yetu. Tunafuta amani itakayodumu kwa vizazi. Hii ndiyo amani wanayoitaka Waisraeli. Hii ndiyo amani wanayostahili."
Netanyahu pia amesema kuwa amani ya kudumu italeta manufaa ya kiuchumi kwa Wapalestina, lakini sharti ijengwe katika misingi ya usalama kwa Israel ili iweze kufaulu.
Rais wa Misri, Hosni Mubarak, ameihimiza Israel ikubali mkono wa amani ulionyoshwa na Waarabu na isitishe kabisa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina mpaka mchakato wa amani utakapokamilika. Amemtaka Netanyahu atimize ahadi yake ya kutafuta amani na Wapalestina.
Naye mfalme Abdullah wa Jordan amewataka rais Abbas na Netanyahu wafanye kazi kwa haraka kuyashughulia masuala ya mustakabali wa mwisho wa amani kwa kuwa muda umewatupa mkono.
Polisi wa Israel wanalinda eneo yalikotokea mashambulio jumanne iliyopita,karibu na mtaa wa wahamiaji wa kiyahudi Kiryat Arbah
Juhudi za kutafuta amani baina ya Israel na Wapalestina zimepata pigo jengine baada ya Waisraeli wawili kujeruhiwa wakati motokaa waliokuwa wakisafiria ilipofyetuliwa risasi karibu na mji wa Ramallah katika eneo la Ukingo wa Magharibi. Redio ya jeshi la Israel imetangaza kuwa mmoja kati yao amepata majeraha mabaya.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, risasi zilifyetuliwa kutoka gari jengine ambalo lilikuwa limeipita motokaa yao. Shambulio hilo limetokea karibu na makaazi ya walowezi wa Kiyahudi ya Rinomin. Kitengo cha kundi la Hamas cha Ezzedine al Qassam, kimedai kufanya shambulio hilo ambalo ni la pili katika kipindi cha saa 24.
Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, amelilaani shambulio hilo na kuahidi kufanya kila jitihada kufikia mkataba wa amani na Waisraeli.
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema magaidi hawatoifunga njia ya kuelekea amani na kushukuru kwamba hakuna aliyekufa katika shambulio hilo.
Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Palestina yanatarajiwa kuanza tena hii leo.
0 comments