IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
UONGOZI wa Yanga umesema haukubaliani na dau la Azam la kumtaka mshambuliaji wake Mrisho Ngasa kwa Sh milioni 25.
Akizungumza na HABARILEO jana, Katibu Mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako alisema thamani ya Ngasa ni kubwa zaidi ya kiasi hicho cha fedha.
Mwalusako alisema kila mchezaji wa timu hiyo anayo thamani yake halisi na thamani ya Ngasa itathibitishwa rasmi kesho wakati uongozi utakapofanya kikao kujadili masuala muhimu yahusuyo klabu hiyo.
Alisema Ngasa ana umuhimu kwa Yanga na pia zipo klabu nyingine za nje ya nchi ambazo nazo zinamhitaji kwa dau kubwa zaidi.
Alisema Yanga itakuwa tayari kwa majadiliano siku chache zijazo baada ya uongozi kukubaliana na kuweka wazi thamani ya mauzo ya mchezaji huyo.
“Kwa sasa siwezi kusema gharama halisi ambayo tunaweza kuichukua na kama tukitaka kumruhusu mchezaji huyu ahamie timu hiyo sio kwa Sh milioni 25 kama ambavyo Klabu ya Azam imependekeza itakuwa ni zaidi ya hapo,” alisema Mwalusako.
Ngassa hivi karibuni alikwenda Rwanda kwa majaribio na timu ya APR ambako aliamua kurudi nchini baada ya kutofikia muafaka.
Jana alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akiitaka Yanga ilipe fadhila kwa kumruhusu ajiunge na Azam.
“Azam wanataka kunipa fedha nyingi sana, mimi nimeshapata ofa ya kucheza sehemu mbalimbali lakini uongozi haukuwa radhi kuniruhusu sasa basi na mimi inilipe fadhila kwa kuniachia niende Azam,” alikaririwa Ngasa.
You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - Yanga yagoma kumuuza Ngasa kwa Sh mil 25
0 comments