Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Hatma ya serikali ya mseto Z’bar Julai 31

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KURA za maoni zitakazoamua kuwapo au kutokuwapo kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, sasa zinatarajiwa kupigwa Julai 31, mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande alipozungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za tume hiyo zilizopo Maisara, mjini hapa.

Alisema Mei 11 mwaka huu, ZEC ilipokea kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume maagizo ya kufanya mchakato wa kupata kura za maoni kutoka kwa wananchi.

“Tayari maandalizi yameshaanza kwa kasi ili kuwahi tarehe husika,” alisema Mwinyichande aliyeongeza kwamba, fedha kwa ajili ya kazi hiyo imeshapatikana kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP).

Amewataka wadau, wanasiasa, wanahabari na wengine kuunganisha nguvu katika kuwaelimisha wananchi ili wachukue uamuzi sahihi katika maamuzi yao.

“Waliojiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu ndio watakaopiga kura za maoni,” alisisitiza Mwinyichande.

Naye Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, amesema kiasi cha Sh. bilioni 3.77 kitatumika, huku UNDP ikiwa imeshatoa dola za Kimarekani 650,000 (Sh milioni 850).

Uamuzi wa kura za maoni umekuja baada ya Rais Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kutangaza maridhiano ya kisiasa Novemba mwaka jana.

Baraza la Wawakilishi lilipitisha Sheria ya Kura ya Maoni Na 6 ya mwaka 2010 Januari mwaka huu, likiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa ambayo inatoa nafasi ya chama kitakachoshinda kutoa Rais na kitakachofuatia kutoa Makamu wa Rais.

Pia vyama hivyo vitatoa mawaziri kulingana na uwiano wa ushindi katika Baraza la Wawakilishi.
Tags:

0 comments

Post a Comment