IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya ametumia mkutano wa hadhara kwenye moja ya kata za jimboni kwake kuzungumzia mgomo ulioandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), akidai ulichochewa na vyama vya upinzani.
Uamuzi wa Kapuya, ambaye ni mmoja kati ya watu wanaoshutumiwa na Tucta kwa madai ya kutomshauri vizuri rais, kutumia mkutano wa hadhara kuzungumzia mgomo huo, umekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kushutumiwa kwa kutumia wazee wa Dar es salaam kuzungumzia suala hilo ambalo kwa sasa limewekwa kiporo.
Profesa Kapuya, ambaye pia alilalamikia polisi wakidai kuwa wana hisa na vyama vya upinzani kutokana na kutompa ulinzi na wanafurahia Wana-CCM kupigwa, alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kaliua wilayani Urambo mkoani Tabora.
Watu waliokuwa kwenye mkutano huo waliiambia Mwananchi kuwa Kapuya aliwaambia wananchi kuwa wapinzani waliitumia Tucta ili kufanikisha mpango wao wa kuiangusha CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.
“Mgomo wa Tucta umeshawishiwa na vyama vya upinzani ili CCM isiweze kushinda katika uchaguzi mkuu,” mmoja wa watu waliozungumza na Mwananchi alimkariri mbunge huyo wa Urambo Magharibi.
“Polisi waseme kama wana hisa na vyama vya upinzani, kwanza wameshindwa kunipa ulinzi na pia wanafurahia kuona wanachama wa CCM wakipigwa na wale wa upinzani.”
Kwa mujibu wa watu hao walioongea na Mwananchi, katika mkutano huo uliofanyika kuanzia majira ya saa 6:00 hadi saa 8:00 mchana kwenye viwanja vya Center mjini humo na kuhudhuriwa na vijana pamoja na watoto, Kapuya alikwenda mbali na kusema kuwa kutokana na hisa walizokuwa nazo askari polisi, wanachama wa CUF wilayani humo wanawapiga kwa mapanga wanachama wa CCM.
Alitoa mfano kuwa katika uchaguzi mdogo wa serikali ya kijiji uliofanyika kwenye kijiji cha Usinge, wanachama wa CUF waliwapiga kwa mapanga wanachama wa CCM.
“Kama wanachama wa CCM nao wakiamua kuchukua hatua ya kujibu mapigo kwa kuwapiga hao wanachama wa CUF , hali itakuwaje,” alisema mtoaji habari huyo akimkariri Profesa Kapuya.
Hata hivyo, kamanda wa polisi mkoani Tabora, ACP Liberatus Barlow jana alisikitishwa na kauli ya Kapuya na kusema kamwe Jeshi la Polisi haliwezi kuegemea upande wowote na kwamba lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia pamoja na mali zao.
"Japo nipo likizo, lakini kwa haraka haraka ni maneno ambayo hayawezi kuingia akilini na ni ya kuyaapuuza. Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kila mtu na si vinginevyo na pia haliwezi kufanya hivyo," alisema ACP Barlow.
Hata hivyo, Kapuya aliwataka wananchi kuwa makini katika uchaguzi na kuwataka wajiepushe na vurugu ambazo zinaweza kuleta vita.
Katika mkutano huo, Profesa Kapuya, ambaye alikuwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa siasa kutoka wilayani humo, wakiwemo madiwani pamoja na katibu wake wa wizara, alisimikwa ukamanda wa vijana mkoani Tabora.
Pia, alipokea kadi nane za wanachama wa CUF, ikiwemo ya mjumbe mmoja wa serikali ya Kijiji cha Ugunga wilayani humo.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, wanachama wa CCM wa kijiji hicho walifanya maandamo ya baiskeli na pikipiki kutoka kata ya Ushokola hadi Kata ya Kaliua.
Katika hatua nyingine, Profesa Kapuya aliishukuru kampuni ya simu ya Vodacom kwa msaada wake wa Sh30 milioni iliyotoa kwa Shule ya Sekondari Kapuya.
You Are Here: Home - - Tucta wamsumbua Kapuya hadi jimboni
0 comments