IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
VURUGU kubwa jana zilizuka kati ya waumini, mchungaji na wazee wa baraza na kusababisha ibada tatu za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mtaa wa Makoka Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam kuvunjika.
Zogo hilo lilianza katika ibada ya kwanza, ambayo huwa huanza saa 12:00 asubuhi baada ya Mwinjilisti Nitisile Makarios kuwahi mapema asubuhi ili ajiandae kwa ajili ya ibada, lakini ghafla liliingia kundi la watu wanaosadikika kuwa ni wazee wa baraza waliovuliwa madaraka na kumwambia kwamba hangeweza kuongoza ibada na kumlazimisha akae chini.
Kipindi hicho idadi kubwa ya waumini ilikuwa nje kusubiri kuingia kanisani ndipo waliposikia zogo ndani ya kanisa hilo na mmoja kati ya wahumini hao, Makarios Simwinga, ambaye ni mume wa mwinjilisti huyo, aliingia ndani kumnusuru mkewe, lakini akasimamishwa na wazee hao akitakiwa arudi nje.
“Walikuwa wameanza kumvamia mwinjilisti na baada ya kuingia ndani kanisani ndipo wazee hao wakaniambia hayanihusu,” alisema Simwinga.
Wazee hao waliwalazimisha waumini kutoa mabenchi ya kukalia nje na kuamuru kuwa misa ifanyike nje na ndipo mlango mkuu wa kuingilia kanisani hapo ukafungwa na kufuli mbili tofauti ili kutokuruhusu ibada kufanyikia ndani.
Baada ya tukio hilo, mmoja wa waumini akampigia simu mchungaji wa usharika huo, Richard Anancha ili afike kanisanio kushuhudia tukio hilo.
Baada ya mchungaji huyo kufika kanisani hapo alimkuta kijana mmoja ambaye Mwananchi iliambiwa kuwa anaitwa Wilson Msiga ambaye alikuwa akichukua picha za video na ndipo mchungaji huyo alipomuhoji sababu kuchukua picha hizo maeneo hayo ya kanisani.
Mwananchi iliambiwa kuwa ghafla mchungaji huyo alipatwa na jazba na kujikuta akimpiga kibao muumini huyo na ndipo kundi la wazee lilipoanza kufanya vurugu kubwa zaidi, kitu kilichofanya waumini wengine waingilie kati kutatua ugomvi huo.
Wakati mvurugano huo ukiendelea polisi walifika eneo hilo wakiwa kwenye gari pamoja na pikipiki tayari kutuliza ghasia hizo na walifanikiwa kufanya hivyo.
Mchungaji wa usharika huo hakuwa tayari kuelezea tukio hilo zaidi ya kuwakusanya waumini wote na kuwaambia kuwa ibada za siku hiyo zimevunjwa na kwamba shughuli za kuabudu zitaendelea Jumapili ijayo kwa kuwa walikuwa wakielekea polisi kwa mahojiano.
“Tunawaomba radhi waumini kwa yote yaliotokea na kwa siku ya leo ibada imevunjwa mpaka Jumapili ijayo. Tunaelekea kituo cha polisi cha Mbezi Luisi kwa ajili ya mahojiano zaidi,” alisema Anancha.
Mchungaji huyo akamaliza kwa dhihaka akisema kuwa ibada hiyo ya jana itafanyika ndani ya gari la polisi aina ya Land Rover Defender .
Pia uongozi wa usharika huo ulitaka kamera iliyokuwa inatumiwa kuchukulia picha za video za tukio hilo, isalimishwe kwa vyombo vya usalama na kuwaomba waandishi wasitumie mkanda kwenye taarifa zao.
Waumini mbalimbali walihojiwa na Mwananchi kuhusu vurugu hizo walisema kuwa chanzo cha ghasia hizo ni uamuzi wa mchungaji wa usharika huo kuliengua baraza la wazee na kutangaza baraza jipya, hali iliyofanya wazee walioenguliwa kuchukia na kufanya kila vituko ili warejeshwe katika nafasi zao za mwanzo.
Kwa mujibu wa waumini kanisani hao, wazee walioenguliwa pia wamekuwa hawafurahishwi na Mwinjilisti Makarios wakidai kuwa ni kikwazo katika mipango yao.
Waumini hao walisema mgogoro wa kuenguliwa kwa wazee hao ulianza Machi 28 baada ya wazee hao kuiba sadaka pamoja na kumshinikiza mwinjilisti wa kanisa hilo kuruhusu uingizaji wa fedha kwa njia isiyo halali.
“Wazee hawa wa baraza walienguliwa baada ya kubainika kuwa wana tabia ya kuchukua sadaka kwa kiasi kikubwa. Mfano kama sadaka imepatikana Sh20,000, basi wazee hawa wanapeleka Sh8,000 tu na nyingine wanazichukua kwa ajili ya kufanyia mambo yao, hasa unywaji wa pombe pamoja na matukio mengi mabaya,” alisema muumini mmoja.
“Pia wazee hawa walikuwa wanamshinikiza mwinjilisti anunue kiwanja cha kanisa kwa gharama ya Sh28 milioni wakati kiwanja hicho ni Sh20 milioni wakiwa na lengo ya kuchukua Sh8 milioni kwa ajili ya manufaa yao.”
Alisema tukio hilo la uvunjwaji wa sheria lilifanya mwinjilisti huyo kugoma kufanya kama wanavyohitaji wazee wa baraza hilo.
Waumini hao waliongeza kuwa baada ya Mchungaji Anancha kuvunja baraza la wazee kwa mujibu wa kanuni na sheria za KKKT, aliamua kuteua baraza jipya wiki nne zilizopita ambalo mpaka sasa linafanya kazi kanisani hapo japokuwa bado kusimikwa rasmi.
Waumini hao walitawanyika huku wakiwa wamehuzunika kwa tukio hilo la kustajabisha ambalo limechafua kanisa hilo kongwe duniani.
“Wito wangu naomba kwa waumini pamoja na viongozi wote wajue kuwa hii ni dini na si sehemu ya biashara. Unapofanya mambo hayo ya wizi kwenye sehemu ya dini, moja kwa moja watu hao watakuwa na matatizo. Kama kweli walikuwa wanashiriki katika wizi wa mali za kanisa, Mungui atawadhibu,” alisema mama mmoja muumini wa kanisa hilo.
Kanisa hilo kwa mujibu wa ya vyanzo vya habari ilizopata Mwananchi lina waumini zaidi ya 400 na sadaka ya Jumapili moja ni takriban Sh450,000.
You Are Here: Home - - KKKT wazichapa kavukavu ibada tatu zashindwa kufanyika
0 comments