IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta amesema atawaanika maadui wake wa kiasisa ambao wamekuwa wakimsakama na kutaka kumng’oa jimboni kwake.
Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalum kwa njia ya simu kutoka Geneva, Uswisi, mwishoni mwa wiki anakohudhuria mkutano wa maspika duniani, alisema kwa kipindi kirefu amekuwa akisikia mikakati mingi ya kumng’oa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
“Ni kweli nimekuwa narushiwa maneno mengi yakiwemo ya kuambiwa naandaliwa mkakati wa kung’olewa jimboni wakati huu wa uchaguzi mkuu,” alisema.
Alisema hivi sasa yupo nchini Uswisi akihudhuria mkutano wa maspika zaidi ya 150 kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kujadili masuala ya utendaji kazi wa kila siku wa masuala ya Bunge.
“Nadhani nikirudi nitakuwa katika nafasi nzuri ya kufafanua mambo yote ambayo yamekuwa yakielekezwa kwangu, kwani naelewa kuna mikakati mibaya inayoandaliwa dhidi yangu,” alisema.
Alisema katika masuala ya siasa, siku zote mwanasiasa hawezi kukosa maadui kutokana na msimamo wake wa kuwatetea wananchi wanyoge.
“Unajua ndugu yangu kwenye masuala ya siasa huwezi kukosa maadui, ndiyo sehemu yao ya kujinadi, lazima ukumbuke kuwa siku zote mwanasiasa makini hawezi kukosa maadui,” alisema Spika Sitta.
Alisema mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, atasafiri hadi mjini Istanbul, Uturuki ambako amepangiwa majukumu yahusuyo masuala ya wabunge.
“Natarajia nikimaliza hapa mkutano huu, nitaelekea Istanbul kwa ajili ya mkutano mwingine ambao unahusiana na masuala yetu ya kiutendaji,” alisema.
Spika Sitta hivi sasa anakabiliana na upinzani mkali ndani ya chama na bungeni kutokana na kujipambanua kuwa ni miongoni mwa wabunge wanaopambana na ufisadi.
Kiongozi huyo mkuu wa Bunge inadaiwa amekuwa kinara wa kuruhusu mijadala yenye kuishambulia serikali na viongozi wastaafu kiasi cha kuhatarisha mustakabali wa chama hicho kikongwe.
Sitta anadaiwa kuwa tangu kuibuka kwa kashfa za ufisadi, amekuwa mstari wa mbele kutaka wale wote wanaohusishwa na kashfa hizo wawajibishwe bila kujali nyadhifa zao katika chama au serikalini.
Kutokana na msimamo huo, Agosti mwaka jana katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Spika Sitta nusura apokonywe kadi ya uanachama baada ya wajumbe kutoa pendekezo hilo ili kukinusuru chama.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilibainisha kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya wajumbe ambao walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili ambapo moja lilikuwa likiunga mkono vita ya ufisadi iliyokuwa ikiongozwa na Sitta huku jingine likipinga kwa madai kuwa ni tuhuma zenye lengo la kuchafuana.
Mgawanyiko wa makundi hayo ndio uliokifanya chama kifikie hatua mbaya ambayo kama isingekuwa busara ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, Spika Sitta angevuliwa uanachama.
Tangu kuibuka kwa vita hiyo, Sitta amekuwa akilalamika kuwa kuna baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wakitembeza fedha jimboni ili kumuangusha kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.
Sitta alisema watu wanaofanya hivyo hawataweza kufanikiwa kwa kuwa ana uhakika wa kushinda na kurudi bungeni katika kiti chake cha uspika.
Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni kumeibuka upya taarifa za kuwapo kwa mikakati ya kuwang’oa Sitta na Naibu Spika, Anne Makinda ambao wanaonekana kuwa tishio kwa kundi fulani ndani ya chama.
Baadhi ya taarifa zinadai kuwa vigogo waliojeruhiwa katika vita ya ufisadi ndio walio mstari wa mbele kuhakikisha Spika Sitta harejei bungeni.
You Are Here: Home - - Sitta akunjua makucha • ATANGAZA KUWATAJA WANAOTAKA KUMNG?OA
0 comments