Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Ocampo akutana na watu walioathirika na ghasia za uchaguzi wa Kenya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


 

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa Luis M. Ocampo amekutana na wanachama wa kundi linalojisaidia lenyewe mjini Nairobi ambalo limeshuhudia matukio ya kinyama wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya.

 
Luis  Moreno  Ocampo  amesema  jana   kuwa  amefanya ziara   katika  eneo  linalokumbwa  mara  kwa  mara   na uhalifu  nchini  Kenya la  mtaa  wa  mabanda  la Mathare  ili kufahamu maoni  ya  baadhi  ya watu walioathirika  na ghasia  za  baada  ya  uchaguzi, ambazo  zimesababisha watu  zaidi  ya  1,000  kuuwawa. Mtaa  wa  mabanda  wa Mathare  unafahamika  kwa  kiwango  chake  cha  juu  cha uhalifu  na  kusambaa  kwa  utengenezaji   na  matumizi ya  pombe za  kienyeji.
Mwendesha  mashtaka  amesema  anaamini  uhalifu  dhidi ya  ubinadamu  umefanyika  wakati  wa ghasia  hizo. Majaji wa  mahakama  ya  kimataifa  ya  uhalifu  wa  kivita waliidhinisha  mwezi  uliopita  kuwa  Moreno  Ocampo anaweza  kuanza  kufanya  uchunguzi  kuhusu  suala  hilo.
Serikali  ya  Kenya   jana  iliahidi  kutoa  ushirikiano   kwa mahakama  hiyo  kuhusiana  na  uchunguzi  huo. Tamko hilo  limetolewa  katika  mkutano  mjini  Geneva  baina   ya baraza  la  umoja  wa  mataifa  la  haki  za  binadamu  na ujumbe  wa  serikali  ya  Kenya  ukiongozwa  na  waziri  wa sheria  wa  Kenya.
Katika  muhtasari  wa  mkutano  huo , Kenya  imesema itatoa  ushirikiano  kamili   kwa  mahakama  hiyo  ya kimataifa  na  kutoa  uhakikisho  wa  kuwalinda mashahidi dhidi  ya vitisho vya kutaka kuwadhuru.
Ahadi  ya  kuwalinda  mashahidi  ambao   huenda  wakatoa ushahidi   imekuja  baada   ya  ombi  la  kufanya  hivyo lililotolewa  na  Austria, Korea  ya  kusini, Ireland, Australia , Norway  na  Ureno. Kenya  pia  imekubali  kuchukua  hatua zaidi  kuzuwia  hali  ya  kuepuka  kuchukuliwa  hatua  kwa wale  waliohusika  katika  ghasia  hizo  za  baada  ya uchaguzi.
Luis Moreno-Ocampo , mwendesha   mashtaka  mkuu  wa mahakama  ya  kimataifa  ya  uhalifu  wa  kivita , ICC, ambayo  ni mahakama  pekee ya  kudumu   ambayo  ni huru  duniani ,  amekwenda  nchini  Kenya  wiki  iliyopita kukutana  na watu walioathirka na  ghasia  zilizosababisha kumwagika  damu  nchini  Kenya.
Akizungumza  mjini  Nairobi , amesema  kuwa  ni  muhimu kufanya  uchunguzi  wa  uhalifu  huu ili kuhakikisha   kuwa uchaguzi  wa  mwaka  2012  nchini  Kenya  unakuwa  wa amani. Ameongeza kusema kuwa  uchunguzi  huo unapaswa  kuwa  onyo  kwa  mataifa  mengine  ya  Afrika ambayo  yanakaribia  kufanya  chaguzi.
 Ocampo amesema  kuwa  katika  mwaka  mmoja  na  nusu ujao , kutakuwa  na  karibu  chaguzi  15  katika  bara  la Afrika na wao wanapaswa  kuhakikisha  kuwa  chaguzi  hizi zinakuwa  za  amani. Kenya  itatoa  ishara  kwa  nchi  zote kwamba  ukifanya  uhalifu  dhidi  ya  ubinadamu utapelekwa  The  Hague  katika  mahakama  ya  kimataifa ya  uhalifu  wa  kivita.
Ethiopia, Rwanda, Burundi, Tanzania  na  Uganda  ni baadhi  ya  nchi  za  Afrika  ambazo  zinatarajia  kufanya uchaguzi mnamo  muda  wa  miaka  miwili  ijayo.
Tags:

0 comments

Post a Comment