IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MTAMBO wa kusafisha mafuta ya petroli unaotarajiwa kuanza kujengwa nchini utakamilika ndani ya miaka minne kuanzia sasa na utasafisha mapipa 200,000 ya mafuta kwa siku.
Mtambo huo utajengwa eneo la Kisiju, Mkuranga wilayani Pwani na Kampuni ya Noor Oil and Industrial Technology Consortium (NOITC) katika eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 196.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Rais wa Chama cha Wenye Viwanda vya Mafuta na Gesi Urusi, Dk. Genady Shmal, alisema mtambo huo utasafisha mafuta ya petroli, dizeli, ya taa; ya aina zote yakiwamo mazito na mepesi.
Alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa, wanafanya taratibu za kiufundi na baada ya hapo, ujenzi utaanza ambao utachukua kati ya mwaka mmoja na mitatu.
Mafuta hayo yatatoka Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Iraki, Irani, Saudi Arabia, Urusi na Qatar na kuongeza: “Inawezekana wakati tunaanza ujenzi, mafuta yakapatikana nchini hivyo ikarahisisha, lakini lengo letu ni kuchukua mafuta maeneo ya karibu na Tanzania”.
Kwa sasa eneo la Mkuranga ni moja ya maeneo yanayofanyiwa utafiti wa mafuta ya petroli. Mbali na ujenzi wa mtambo huo, pia kampuni hiyo itajenga mabomba ya kusafirishia mafuta kwenda Mwanza na Kigoma na mradi ukiendelea vizuri, inatarajia kujenga bomba la kusafirishia mafuta kutoka Mwanza hadi Uganda.
Rais wa NOITC, Minoo Davar, alisema wanaendelea na mazungumzo na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) juu ya masuala kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta kwenda Mwanza na Kigoma.
Dk. Shmal alisema mradi huo utakaogharimu dola bilioni sita za Marekani (zaidi ya Sh trilioni sita), utaajiri Watanzania 5,000 kwa ajili ya ujenzi hadi kukamilisha mradi na kufafanua, “hatutaki kuchukua wafanyakazi kutoka India na China, tutaajiri Watanzania wa hapa hapa ili kukuza uchumi wa nchi”.
Rais huyo alisema baada ya kukamilika ujenzi na kuanza kazi, Watanzania 2,000 watapata ajira.
Dk. Shmal alisema Serikali ya Tanzania ina hisa ya asilimia tano kwa upande wa mtambo, asilimia 10 kwa mabomba na mradi huo una msamaha wa kodi kwa miaka 15.
“Sababu kubwa ya kujenga mtambo huu Tanzania ni kutokana na utulivu wa kisiasa, awali tulipata maombi mengi na ilikuwa tuujenge Kenya, lakini kule tuliona hakuna utulivu wa kisiasa na hapa ingawa kuna uchaguzi mkuu mwaka huu, taarifa zinaonesha hakutakuwa na machafuko ya kisiasa,” alisema Rais huyo.
Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa kushuka kwa bei ya mafuta hayo nchini baada ya mtambo kukamilika, Dk. Shmal alisema “sina hakika sana kama bei itashuka, lakini naona itakuwa ya kawaida kama ilivyo kwa Ulaya”.
Huu utakuwa ni mtambo wa pili kujengwa nchini, wa kwanza ukiwa ni wa Tiper uliokuwa Kigamboni, Dar es Salaam, ambao hata hivyo umekufa na ulikuwa ukisafirisha mafuta yake kwa mabomba ya Kampuni ya Tazama kwenda Zambia.
You Are Here: Home - - Mtambo wa kusafisha mafuta kujengwa Dar es Salaam
0 comments