Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Slaa amuwakia Pinda • ASEMA SERIKALI INAWAOGOPA ROSTAM, MKAPA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amesema kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na serikali yake inawaogopa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Mbunge wa Igunga Rostam Azizi (CCM) wanaotuhumiwa kwa kuhusika kwenye ufisadi, ndiyo maana hawajachukuliwa hatua hadi leo.
Dk. Slaa alitoa tuhuma hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya ukumbi wa Bunge mjini hapa.

Katika maelezo yake Dk. Slaa alisema kuwa kutokana na tamko lililotolewa juzi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo inaonyesha wazi kuwa matamshi yake yanaiweka serikali pabaya; inawalinda watu wanaohusika na ufisadi mkubwa unaoliangamiza taifa hili.

“Juzi Waziri Mkuu Pinda aliliambia Bunge kuwa hana jibu, sasa sisi wabunge tuna mamlaka ya kuhoji serikali juu ya mambo mazito ya kitaifa, lakini alichojibu ni usanii mtupu,” alisema Dk. Slaa.

Slaa alisema kuwa ana ushahidi wa vielelezo vinavyoonyesha kuwa Mkapa na Rostam walikutana chini ya mwanasheria aliyemtaja kwa jina moja tu la Sanza na kupanga mikakati yote ya kuchota fedha hizo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Alisema Mkapa na Rostam walikutana katika kikao cha siri na kupitisha maamuzi ya kuchota kiasi cha sh bilioni 40 katika Kampuni ya Kagoda.

Katika hilo, Slaa alisema hata Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nayo imehoji upotevu wa fedha hizo, lakini katika hali ya ajabu mpaka sasa haijapata majibu.

Alisema kwamba mnamo Agosti 1, 2005, Rostam na Mkapa walikutana kupanga mikakati ya kuwawezesha kuchota kiasi hicho kupitia Kampuni ya Deep Green na ilipofika Agosti 4 mwaka huo huo wakati wa mchakato wa kupata mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walifanikiwa.

“Tulitoa nyaraka kuonyesha wizi mbalimbali kuomba wazifanyie uchunguzi kampuni za Kagoda, Mwananchi na Deep green kama EPA, lakini haijafanyika kutokana na ukweli ambao tunao kuwa walizichota wao kwa ajili ya uchaguzi” alieleza na kuzidi kufafanua kuwa katika wizi wa Deep Green mambo yote yalikamilika Agosti 4 wakati CCM walipokuwa kwenye harakati za mchakato wa kupata mgombea wao kwenye kura za maoni.

“…. Hili tunalo uhakika kwani nilishawahi kuwapa mpaka Bank Statement, tulitaka uchunguzi sasa tatizo linatoka wapi kipindi chote hiki?” alihoji.

Alisema serikali imekuwa na kigugumizi kikali kutoa majibu katika kampuni mbalimbali zikiwemo Mwananchi, Tangold na Kagoda hali ambayo inaibua maswali mengi juu ya serikali kuwajibika.

“Nimetaja makampuni mengi lakini mpaka leo hii hata ile Kampuni ya Meremeta ambayo wanasema ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameshindwa kuitolea maelezo… hii inashangaza.

“…hapa tatizo si Meremeta ndugu zangu, bali tatizo ni mtu aliyehusika kwani wote wapo na wamelisababishia taifa hasara karibu sh bilioni 700 au 800, hizi zote kama zingerudi leo hii tusingekuwa na shida katika maeneo mbalimbali na kuongeza kuwa wizi hauna jeshi,” alisema Dk. Slaa.

Alisema Meremeta pekee inatuhumiwa kuchota kiasi cha bilioni 155, wakati kampuni ya Tangold inadaiwa kuchota bilioni 13 huku Mwananchi ikidaiwa kuchota bilioni 5, fedha ambazo ni nyingi kuliko za EPA.

Alisema fedha hizo zingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa madarasa, kusambaza huduma za maji, umeme, kujenga zanahati na kulipa madeni ya walimu.

Alisema ni wazi kuwa serikali haina dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi, hali ambayo inaiweka pabaya kwa vile wananchi wataihukumu kutokana na makosa yake.

Hata hivyo, Rostam amekuwa akikana kuhusika katika ufisadi huo.

Alipoulizwa jana kwa njia ya simu, alisema maneno hayo ni ya kipuuzi.

“Hayo maneno ni ya kipuuzi; mnaniuliza kila siku na nimeshayatolea ufafanuzi?

“…Watu wamechanganyikiwa; hawajui cha kufanya katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwaka huu.

“Ni mambo ya kipuuzi na siasa zisizo na maana, kwa nini kila siku wanaendeleza hayo? Hakuna kitu cha kufanya? Tafadhali naomba msiendelee, wameshindwa kisiasa siwezi kujibishana naye,” alisema Rostam
Tags:

0 comments

Post a Comment