Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Majimbo ya uchaguzi yagawanyw

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo imetangaza kugawa majimbo saba ya sasa ya uchaguzi ambapo bunge lijalo mwakani linatarajiwa kuwa na nyongeza ya wabunge saba wa kuchaguliwa kutoka 232 waliopo hadi 239.

Wabunge hao saba wa ziada watapatikana baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu kulingana na tangazo hilo la NEC.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Lewis Makame, majimbo yatakayogawanywa ni Nkasi mkoani Rukwa; Tunduru (Ruvuma); Maswa (Shinyanga); Kasulu Mashariki (Kigoma); Bukombe (Shinyanga); Singida Kusini (Singida) na Ukonga (Dar es Salaam).

“Taarifa zaidi kuhusu majimbo hayo mapya yatakayoanzishwa itatolewa baada ya Tume kukutana na wadau wa majimbo husika,” ilieleza taarifa ya Jaji Makame kwa vyombo vya habari leo.

Awali, NEC ilitangaza kwamba halmashauri zilizokuwa zikitaka majimbo yao yagawanywe, zitume mapendekezo yao kwa Tume hiyo hadi Februari 28 mwaka huu, na kwamba baada ya kufanya tathimini yake ingetangaza majimbo yanayogawanywa Aprili 10, mwaka huu.

Katika mapendekezo hayo, Tume ilisema imepokea mapendekezo kutoka halmashauri 47 nchini, zikiomba majimbo yao kugawanywa. NEC haikuzitaja halmashauri hizo. Kwa mujibu wa sheria, majimbo ya uchaguzi hufikiriwa kuongezwa kila baada ya miaka 10.

NEC ilisema maombi hayo ya halmashauri 47 yalizingatia vigezo 13 ilivyovitoa kwa majimbo yenye sifa ya kugawanywa ambavyo baadhi yao ni mawasiliano, hali ya kijiografia, idadi ya watu kwa kutumia takwimu za mwaka juzi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu; ambacho ni kigezo kikuu katika kuamua majimbo gani yagawanywe.

Kwa mujibu wa NEC, mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu katika majimbo ya uchaguzi yaliyopo katika maeneo ya vijijini ni 206,130 wakati majimbo ya mjini ni 237,130.

Vigezo vingine ni uwezo wa ukumbi wa Bunge na viti maalumu vya wanawake ambavyo kwa sasa ni asilimia 30. Vingine ni mazingira ya Muungano, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala na kata moja kutokuwa ndani ya majimbo mawili.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, alikaririwa akisema kuna maombi zaidi ya 66 kutoka wilaya mbalimbali yaliyowasilishwa serikalini yakitoa mwito wa kuongeza idadi ya majimbo, kugawa majimbo na halmashauri mbalimbali kugawanywa.

Kati ya halmashauri zilizoomba kugawanywa majimbo ni ya Mufindi, Iringa; Kilosa na Mikumi mkoani Morogoro; Mbarali, Rungwe Magharibi na Mbozi mkoani Mbeya na Ruvuma ni Mbinga.

Maombi hayo pia yalisikika kutoka mikoa mbalimbali nchini ikiwamo Singida, Arusha, Manyara, Dar es Salaam (Ukonga na Kigamboni); Dodoma katika halmashauri za Kondoa na Bahi na Kigoma.

Kuhusu ratiba ya Uchaguzi Mkuu, Jaji Makame alisema uteuzi wa wagombea utakuwa Agosti 19 na kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 20 hadi Oktoba 30, mwaka huu.

“Kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi, Tume itawatangazia wananchi rasmi, tarehe ya kutoa fomu za uteuzi kwa wagombea,” alieleza Jaji Makame katika taarifa yake. Zanzibar pia imetangaza kuwa uchaguzi wake utafanyika Oktoba 31, mwaka huu.
Tags:

0 comments

Post a Comment