Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sitta: Zitto achana na ndoto za Geita

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter Sitta: Zitto achana na ndoto za Geita

Vijana wa jamii ya kimasai wakilima mahindi katika kijiji cha Olerien Magaiduru wilayani Ngorongoro kamawalivyokutwa na mpigapicha wetu juzi. Vijana hao wameamua kuanza kilimo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo mwaka jana yalisababisha vifo vya mamia ya mifugo yao ndipo wakaamua kuanzisha kikundi cha Waera ili wafanye kazi hiyo waweze kupata chakula. Picha Mussa Juma



SPIKA Samuel Sitta jana alimshauri Zitto Kabwe kuachana na ndoto za kuwania ubunge wa jimbo la Geita, lakini muda mfupi baadaye kiongozi huyo wa Bunge akaomba msaada wa sala kutoka kwa paroko ili aweze kushinda uchaguzi kwenye jimbo lake.

Spika alitoa ushauri huo baada ya Zitto, ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, kuomba kuuliza swali la nyongeza kuhusu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Geita wakati wa kipindi cha maswali na majibu jana kwenye Mkutano wa 19 wa Bunge unaoendelea mjini hapa.

Swali la msingi kuhusu mradi huo liliulizwa na mbunge wa Geita Mjini, Ernest Gakeya Mabina, ambaye alitaka kujua kama serikali inatambua kuwa mgodi wa dhahabu wa wilayani humo uko tayari kutoa kiasi cha dola 500 milioni za Kimarekani kwa ajili mradi huo.

Baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Aggrey Mwanri kujibu kuwa serikali haina taarifa hizo, Zitto, ambaye ameeleza kuwa huenda atalitosa jimbo lake na kugombea ubunge wa Geita, alisimama na kuelezea matatizo ya maji yanavyoisumbua Geita na kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa fedha za kusambaza maji kutoka kwenye matanki.

"Kwa kuwa mgodi utatoa fedha za kukutoa maji kutoka Ziwa Victoria hadi kwenye matanki, ni vizuri serikali ikatafuta fedha ili ifanye kazi ya kusambaza maji kwenda sehemu mbalimbali," alishauri Zitto.

Lakini kabla ya kumkaribisha Mwanri kutoa maelezo, Spika Sitta alisema: "Kwanza naibu waziri ningependa kumshauri kidogo Zitto. Naomba uachane na mambo hayo ya kugombea ubunge wa Geita. Ni vizuri ukarudi kwenye jimbo lako."

Kauli hiyo ya Spika Sitta iliamsha kicheko kutoka kwa wabunge wengine.

Akizungumzia kitendo chake cha kuzungumzia masuala ya Geita mara baada ya kumalizika awamu ya asubuhi ya Bunge, Zitto alisema suala hilo halina uhusiano na uamuzi wake wa kutaka kugombea ubunge wa Geita na kwamba amekuwa akiamini ni mbunge wa watu wote na kutoa mfano jinsi alivyokuwa mstari wa mbele katika sakata la mgodi wa Buzwagi.

“Nimekuwa nikitetea Watanzania wote bila ya kujali mipaka ya majimbo, mfano ni wakati nazungumzia suala la Buzwagi. Mimi sikuwa mbunge wa Kahama, lakini nililizungumzia,” alieleza mbunge huyo kutoka Chadema.

Hadi sasa, Zitto bado hajaamua agombee wapi kati ya Kigoma Kaskazini na Geita baada ya kufanya uchunguzi ambao alisema ungetoa picha ya nini afanye kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Uchunguzi wake, ambao alisema ulifanywa na watu wake, ulihusisha majimbo ya Kinondoni, Kahama, Geita, Kigoma Mjini na jimbo lake Kigoma Kaskazini lakini baadaye akasema kuwa ameachana na majimbo matatu na kubakiwa na Geita na Kigoma Kaskazini na kwamba angetangaza uamuzi wakati wowote.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Sitta naye alijikuta kwenye masuala ya uchaguzi wakati alipomuombaparoko wa Parokia ya Urambo Mashariki kumuombea dua ili aweze kurudi bungeni mwaka 2011.

Spika, ambaye amekuwa akidai kuwa mafisadi wanamuandama kwenye jimbo lake na wakati fulani kuomba aongezewe ulinzi, alitoa kauli hiyo wakati akitambulisha wageni waliofika bungeni jana baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Alikuwa akitambulisha kikundi cha wanakwaya 36 kutoka Urambo ambacho kilitembelea Bunge jana kikiwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam kurekodi albamu yao.

“Jamani mwaka huu ni mgumu kweli, kwa hiyo nyinyi watu wa dini mtuombee sana kwa Mungu kwa sababu hali ni ngumu kwetu,” alisema Spika Sitta.

“Kwa hiyo mkirudi jamani, mtuombee na mumwambie Baba Paroko Mongela atuombee ili aliyebora apite Urambo Mashariki.

“Sio lazima mimi lakini atuombee ili aliyebora apite na kuwa mbunge katika jimbo la Urambo Mashariki mkoani Tabora.”

Wakati akiwatambulisha wanakwaya hao wa Kikundi cha Mtakatifu Cecilia kutoka Urambo, Sitta alisema kikundi hicho kinaongozwa na mwalimu kutoka Kenya ambaye anafundisha shule ya kimataifa ya mtakatifu huyo.

Baadaye akaipigia debe shule hiyo akisema: “Jamani sio muwapeleke (watoto) kwenye shule za mjini, hata shule za vijijini kama shule yetu ya kimataifa ya Urambo Mashariki.

“Halafu, Waziri wa Maji, shule yetu ile ya kimataifa ya Urambo haina maji, kwa hiyo nakuomba ufanye utaratibu wa kutupatia maji.”
Tags:

0 comments

Post a Comment