Dikteta wa zamani wa Panama, Manuel Antonio Noriega, amewasili mjini Paris leo baada ya Marekani kumhamishia huko ili afikishwe mahakamani nchini Ufaransa kwa madai ya kusafirisha fedha za biashara ya madawa ya kulevywa kinyume na sheria.
Ndege ya shirika la ndege la Ufaransa iliyomchukua kiongozi huyo wa zamani wa Panama, mwenye umri wa miaka 74, imewasili katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle asubuhi ya leo na alipelekwa moja kwa moja mahakamani ili kusikiliza mashtaka dhidi yake.
Kiongozi huyo wa zamani wa Panama aliondolewa kutoka katika jela mjini Miami jana Jumatatu ambako ametumikia kifungo cha miaka 17 baada ya kuondolewa madarakani mwaka 1989 wakati rais wa zamani wa Marekani, George Bush, alipotuma vikosi vya jeshi la nchi hiyo nchini Panama kwenda kumkamata.
Noriega amekuwa kwa muda wa miaka kadha akipinga kupelekwa nchini Ufaransa , ambako katika mwaka 1999 alihukumiwa akiwa hayuko mahakamani kwa kusafirisha fedha za mapato ya biashara ya madawa ya kulevywa na kuhukumiwa kwenda jela kwa muda wa miaka kumi. Ufaransa ilikubali kufanya kesi hiyo upya.
Noriega alitakiwa kufikishwa mbele ya jaji mahakamani mjini Paris , ambaye alitakiwa kuamuru kuwa arejeshwe rumande akisubiri kufanyika kesi yake ambayo inaweza kuanza kusikilizwa katika muda wa miezi miwili, wamesema maafisa wa Ufaransa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, alitia saini mjini Washington hati ya kupelekwa Noriega nchini Ufaransa jana Jumatatu, na kufikisha mwisho miaka kadha ya mvutano wa kisheria kuhusu hali ya baadaye ya Noriega. Mawakili wa Noriega wanataka aachiliwe mara moja, wakisema kuwa kukamatwa kwake na kupelekwa nchini Ufaransa ni kinyume na sheria.
Akiwa kama mtu muhimu sana kwa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, hapo zamani , Noriega aliingia madarakani nchini Panama akiwa mkuu wa idara ya upelelezi katika jeshi la nchi hiyo na baadaye kama mkuu wa jeshi katika miaka ya 80. Lakini uhusiano wake na Marekani uliharibika kutokana na ripoti kuwa amejiingiza sana katika biashara ya madawa ya kulevywa na kutiliwa shaka kuwa alikuwa pia akishirikiana na Cuba.
Desemba mwaka 1989, Bush aliamuru kukamatwa kwa Noriega ili aweze kufikishwa mahakamani nchini Marekani , na kutuma majeshi nchini Panama katika operesheni iliyopewa jina la 'kitendo cha haki'.
Baada ya Noriega kukimbilia katika ubalozi wa Vatican mjini Panama City, akiomba hifadhi humo, majeshi ya Marekani yalilizingira jengo hilo, na kupiga muziki kwa sauti ya juu ili kumfanya ashindwe kuvumilia. Siku kumi za mkwamo zilimalizika Januari 2 ,1990 wakati Noriega alipojitokeza nje ya jengo hilo la ubalozi na kujisalimisha kwa majeshi ya Marekani ambayo yalimsafirisha hadi Miami , jimboni Florida nchini Marekani. Alihukumiwa kwa makosa ya kufanya biashara ya madawa ya kulevywa na kusafirisha fedha za madawa hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 40 jela. Hukumu hiyo ilipunguzwa na kuwa miaka 17 kutokana na kuwa na tabia nzuri.
Tangu wakati huo alibakia katika mamlaka ya serikali ya Marekani wakati akipambana dhidi ya ombi la kupelekwa nchini Ufaransa.
0 comments