IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilinusurika majaribio 14 ya kupinduliwa, likiwamo lililosababisha kifo cha muasisi wa Mapinduzi, Sheikh Abeid Amaan Karume, Aprili 7, 1972.
Kwa mujibu wa wazee waliokuwapo wakati wa kuasisiwa kwa Muungano, majaribio hayo yalishindikana na mmoja wa wazee hao, aliyewahi kuwa Katibu wa Kwanza wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Afro Shiraz, Baraka Mohamed Shamte alisema kama si Muungano, baadhi ya majaribio hayo yangefanikiwa na kungeendelea kutokea mapinduzi zaidi ya mara sita.
“ Kama isingekuwa Muungano, tungepinduana zaidi ya mara sita,” alisema Shamte ambaye pia ni mtoto wa marehemu Muhammad Shamte, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Zanzibar iliyopinduliwa.
Alifafanua kuwa wafuasi wa utawala uliopinduliwa uliokuwa chini ya Sultan ambao walikuwa ndani na nje ya Zanzibar, ndio waliofanya majaribio hayo 14 katika kipindi kifupi cha kati ya mwaka 1964 na 1972.
“Yalikuwa majaribio ya mapinduzi ya kweli,” alisema Shamte na kuongeza kuwa sababu mojawapo kubwa ya kuundwa kwa Muungano ilikuwa kuipatia SMZ ulinzi na usalama, kwa kuwa baada ya Mapinduzi, Serikali iliyoundwa haikuwa na nguvu za kijeshi kujilinda dhidi ya maadui.
Lengo la pili kwa mujibu wa Shamte, lilikuwa kudumisha uhusiano kati ya Watanganyika na Wazanzibari ambao ulikuwa mkubwa kabla hata ya kuja kwa Wakoloni.
Hata hivyo, mmoja wa mawaziri wa Baraza la Kwanza la Mapinduzi, Hassan Nassoro Moyo, alipinga hoja kuwa Muungano ulianzishwa kwa malengo ya kuipa Zanzibar ulinzi na usalama na badala yake, akasema ulianzishwa na watu siku nyingi kabla hata baba yake hajazaliwa na kilichofanyika Aprili 26, 1964, ni kuuweka rasmi.
“Watu wa nchi hizi mbili walianza Muungano miaka mingi pengine hata kabla baba yangu hajazaliwa, si Muungano wa serikali kama watu wanavyosema kwa kuwa serikali huja ikaondoka.
“Maelewano haya msingi wake ulikuwa udugu na urafiki wa asili, Wakoloni ndio wakaja wakagawa nchi, sisi tukaja tukaendeleza walichoanzisha wazee wetu,” alisema Moyo.
Kuhusu ulinzi na usalama, Moyo alisema ulikuwa wa kawaida wa nchi mbili rafiki, “Zanzibar ilikuwa na Serikali haikuwa vibaya kumwambia mwenzako (Serikali ya Tanganyika), nisaidie,” alisema Moyo.
Alifafanua kwamba Karume hakuogopa kupinduliwa kwa kuwa Serikali ya Mwarabu ilishaondoka na waliopinduliwa walikuwa kizuizini.
Kuhusu majaribio 14 ya kumpindua Karume, Moyo alisema, “kama yalitokea tuliyakabili, naweza kusema ndio yalitokea, lakini hayakuleta athari yoyote, labda yaliyofanyika Aprili 7 (1972 wakati Karume alipouawa kwa risasi) ndio unaweza kusema lilifanikiwa, lilimuua kiongozi wetu.”
Naye Enzi Talib, aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kwanza wa Karume, alipinga hoja ya Shamte kwamba majaribio hayo ya Mapinduzi yangefanikiwa kama si Muungano.
Kwa mujibu wa Talib, baada ya Mapinduzi, mataifa mengi yenye nguvu duniani kuanzia Ulaya Magharibi mpaka Urusi, China na hata mataifa mengi ya Arabuni, waliitambua Zanzibar na mengine yalianzisha uhusiano wa kibalozi.
Talib, ambaye pia alithibitisha kuwa kulitokea majaribio hayo 14 ya kumpindua Karume, alisema nchi hizo zilizokuwa zimeitambua Zanzibar, zisingevumilia kuona ikipinduliwa.
Shamte alitaja mafanikio ya Muungano ambayo hayakukusudiwa wakati wa kuasisiwa kwake, kuwa ni Wazanzibari wengi kunufaika na ukubwa wa Tanzania Bara ambapo alisema wengi hasa kutoka Pemba, walihamia Bara, wameoa, wamejenga na kumiliki ardhi kubwa na maduka makubwa.
“Zamani ukimwambia mtu ahamie Bara ilikuwa vigumu lakini sasa kuna familia zimehama kabisa Pemba na wakirudi kwao ni kama kutembea tena wakikaa mwezi mmoja tu, wanaona taabu ndio maana kura za CUF zimekuwa zikipungua kila mara.
“Ukienda mpakani Kigoma, Tunduma, Mtwara, utawakuta na hata viongozi wakiwapo wabunge wa zamani wamejenga na kuhamia kabisa Dodoma, Hamad Rashid Mohamed (Kiongozi wa Upinzani bungeni) na Fatuma Maghimbi, wamejenga wapi? Si wapo Dar es Salaam hawa,” alisema.
Alifafanua kuwa hali hiyo ni tofauti na Watanzania kutoka Bara ambao tangu enzi ya Ukoloni wako sehemu mbili tu za Zanzibar ambazo ni Dole kisiwani Unguja na Makangale, kisiwani Pemba na kazi yao huko ni kilimo na ufugaji.
Kwa upande wa Moyo alisema, uhamiaji wa Wazanzibari Bara na Watanganyika Zanzibar ni moja ya malengo ya Muungano na kuongeza kuwa yamafanikiwa sana.
“Baada ya Nyerere (Mwalimu Julius) na Karume kusaini makubaliano ya Muungano Aprili 22, 1964, Karume aliitisha Baraza la Mapinduzi siku ile ile, alisema Zanzibar ni nchi ndogo na uchumi wake ni mdogo unaotegemea karafuu na mbata (nazi) ambao asingeweza kuwahakikishia wote ajira.
“Pia (Karume) alisema watu tunazaliana na ardhi haiongezeki na bahari inakula kisiwa, kuungana na Tanganyika ni kuungana na nchi kubwa, tutapata kazi, biashara, elimu na kulima na hata kuzaliana zaidi na sifa yetu huko ni utanzania wetu,” alisema Moyo na kuongeza kuwa hayo yote leo hii yanaonekana na kusisitiza kuwa yeye kamwe hataona haya kusema Wazanzibari wanafaidi Bara.
“Mimi nilioa Bara mwaka 1955, watu wengi hawajui na mpaka leo mke wangu ninaye,” alijitolea mfano na kukumbushia kuwa yeye ni mfano kwamba Muungano wa watu ulianza siku nyingi.
Hata hivyo, Talib alipinga mtazamo huo kuwa Wazanzibari wengi ndio waliohamia Bara na badala yake akaongeza, kuwa Watanzania wanaotoka Bara ndio walioongeza idadi ya watu Zanzibar kutoka 300,000 baada ya Mapinduzi hadi zaidi ya milioni na kazi yao kubwa ni ujasiriamali.
Mafanikio mengine yameelezwa kuwa ni upatikanaji wa bidhaa nyingi za matumizi ya chakula katika masoko ya Zanzibar ambazo zinatoka Bara.
“Wajasiriamali kutoka soko la Mwanakwerekwe, asilimia 90 bidhaa wanazitoa Bara,” alisema Shamte na kuongeza kuwa Muungano ukivunjika, Wazanzibari wataathirika kwa umasikini na njaa.
Hata hivyo Shamte na Talib, walielezea wasiwasi kwamba hali ya sasa ya Muungano inaonesha hatari ya kuvunjika kuliko kuimarika huku Moyo akipinga na kuhoji kwa nini watu wanazungumzia mambo hasi ya kesho wakati kesho yenyewe hawaijui.
“Muungano ni kitu kizuri na viongozi waliuanzisha kwa nia njema lakini wakauacha na upungufu mkubwa,” alisema Shamte.
Moja ya upungufu mkubwa aliouzungumzia Shamte ni katika tafsiri ya Muungano ambapo alisema baadhi ya watu wanasema wanataka Serikali moja kutoka mbili.
Alidai Karume hakuwa na mtazamo wa Serikali moja na ndiyo maana wakati wa Azimio la Arusha, alimwambia Mwalimu Nyerere, Azimio hilo liishie Chumbe (mpakani mwa Dar es Salaam na Zanzibar).
Shamte na Talib walibainisha kwa nyakati tofauti kuwa upungufu mkubwa wa Muungano unatokana na kutofanyika kwa mapitio ya Katiba ya Muungano kama ilivyokubaliwa wakati wa kuasisiwa kwake, kwamba mapitio hayo yangefanyika baada ya miaka miwili.
Shamte alisema Muungano uliundwa kwa haraka na Katiba yake ilitakiwa kufanyiwa mapitio baada ya miaka miwili, jambo ambalo halikufanyika tangu wakati wa Nyerere na Karume mpaka leo.
Muasisi huyo wa Afro Shiraz alionya kwamba kwa jinsi mapitio hayo ya Katiba yanavyoachwa yafanyike na badala yake kukaundwa vikao, kikiwamo cha Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi, ndivyo hali ya kuvunjika Muungano inavyokuwa mbaya.
Kwa upande wa Moyo, ambaye wakati wa Muungano alikuwa Waziri wa Sheria wa Zanzibar, alisema baada ya kusaini makubaliano ya Muungano, walikubaliana kuipitia upya Katiba ya Muungano baada ya mwaka mmoja na si miwili kama walivyosema Shamte na Talib.
Moyo alifafanua kwamba 1964, walirekebisha Katiba ya Tanganyika, ili iwe ya Muungano na wakati wa marekebisho Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi, walikutana na kukubaliana marekebisho hayo ndiyo yawe Katiba ya Muungano.
Hata hivyo mwaka uliofuatia, 1965 walishindwa kufanya mapitio ya Katiba ya Muungano kama walivyokubaliana katika kikao chao na kulitolewa tangazo katika Gazeti la Serikali kuahirisha mapitio hayo ya Katiba.
Kwa mujibu wa Moyo, kuahirishwa huko kulichukua muda na ilipofika mwaka 1977, wakati wa kuunganisha vyama vya TANU na ASP, kuliundwa kamati ya watu 20, kumi kutoka Bara na kumi Zanzibar ambao walipewa kazi ya kushughulikia uunganishwaji wa vyama hivyo na kuzaa CCM.
Alifafanua kuwa baada ya kuundwa CCM, watu hao hao ambao hakuwakumbuka, walipewa jukumu la kuipitia Katiba ya Muungano na mapendekezo yao ndiyo yaliyounda Katiba ya sasa ya Muungano ambayo ni ya mwaka 1977.
Moyo alishauri kuwa si vibaya Katiba ya Muungano ikapitiwa upya kwa kuwa wanasheria wanahoji uhalali wa watu hao 20 kupitia Katiba, wakati makubaliano ya kuipitia yalifanywa na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na wabunge.
You Are Here: Home - - Zanzibar yanusurika kupinduliwa mara 14
0 comments