Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Tendwa ajiandaa kuifuta CCJ

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SIKU moja kabla ya kutoa hati ya usajili wa muda hapo jana kwa Chama Cha Jamii (CCJ), Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, tayari aliiweka hatma ya kisiasa ya chama hicho njia panda baada ya juzi kutangaza kuanza uchunguzi kuona kama kilianza shughuli za kisiasa miaka miwili iliyopita kabla ya usajili.

Jana Tendwa alihitimisha safari ya miezi miwili ya CCJ kusaka usajili wa muda, lakini tayari akiwa amekiweka pabaya chama hicho, baada ya juzi kunukuliwa na kituo cha ITV akisema ofisi yake inafanya uchunguzi wa kina ili kuthibitisha kama chama hicho kilianza siasa kabla ya kusajiliwa miaka miwili iliyopita na ikithibitika atakifuta.

Kauli hiyo ya kitisho ya Tendwa akiitoa siku moja kabla ya kukabidhi hati hiyo huku akisisitiza kwamba, chama hicho kitapaswa kufuata taratibu za kisheria katika utendajikazi wake.

CCJ chama ambacho kimesababisha mtikisiko ndani ya CCM kimekuwa kikifuatilia usajili wa muda katika Ofisi ya Msajili kwa karibu miezi miwili sasa tangu kuwasilisha maombi yao Januari 20, mwaka huu.

Hofu ya CCJ kuanza kazi za kisiasa miaka miwili nyuma, inaangaliwa na wadadisi wa mambo ya kisiasa kama inayotokana na nguvu zake ikiwemo mtandao mpana nchi nzima huku viongozi wake wakitangaza jana kwamba, wanatarajia kukamilisha kazi ya kuzunguka nchi na kupata idadi ya wanachama 200 katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu baada ya kupata hati hiyo badala ya miezi sita.

Habari zaidi zinadai kwamba kwamba baadhi ya vigogo serikalini na katika CCM walikwishafuatwa wakiwemo wakuu wa mikoa ambao baadhi walikubali kuunga mkono na wengine kukataa.

Lakini wakati Tendwa akitoa hati hiyo na onyo la kukifuta chama hicho, Mwenyekiti wa CCJ Richard Kiyabo, alitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa tuhuma mbalimbali dhidi ya chama hicho na kusema hakina uhusiano wowote na Idara ya Usalama wa Taifa kwani mpango huo una lengo la kukivuruga ili kionekane ni chama pandikizi.

Kiyabo alifafanua kwamba, CCJ ni chama tofauti na vingine vya upinzani kwani kimejipanga vema kuhakikisha kinakidhi mahitaji ya msingi ya kidemokrasi kwa Watanzania.

"CCJ siyo chama cha Idara ya Usalama wa Taifa, ni chama cha usalama wa maisha ya Mtanzania, ni chama makini tofauti na vingine vya upinzani kwa hiyo kuna tofauti kubwa," alisisitiza.

Mwenyekiti huyo ambaye alikuwa akibebwa juu pamoja na katibu wake Renatus Muabhi na baadhi ya wanachama waanzilishi, alisema lengo, nia na madhumuni ya CCJ ni kushiriki uchaguzi wa Oktoba.

Aliweka bayana mkakati huo kwamba, katika kufanikisha azma hiyo CCJ imejipanga kukusanya wanachama wanaotakiwa kisheria ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na nusu.

"Tumejipanga kushiriki uchaguzi, nia tunayo na hadi sasa maandalizi ni mazuri tu kwani tutaweza kukusanya wanachama wetu ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na nusu," aliongeza.

Kuhusu usajili wa wanachama, alisema tayari walizundua mchakato huo rasmi siku hiyo ya jana baada ya kupata usajili huo na kuongeza: "Hata ninyi waandishi wa habari mnakaribishwa."

Akizungumzia kuhusu kuwepo vigogo ndani ya CCM, Kiyabo alirudia kwamba wao wanalenga wanachama 20 milioni na hadi sasa hawana vigogo wowote ndani ya chama hicho tawala.

"Sisi hatuzungumzii sijui vigogo, hatuna vigogo ndani ya CCM tunachozungumzia ni namna ya kuwapata wanachama 20 milioni nchini kote, inawezekana sasa wanachama ukichanganya na CCM waliopo ni 10 milioni," aliongeza.

CCJ ujio wake unaangaliwa na wadadisi wa mambo ya kisiasa kama tishio kwa CCM na Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kutajwa kuhusisha vigogo wa chama hicho tawala ambao wanataka kujitenga na kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Tayari Spika wa Bunge Samuel Sitta, aliwahi kusema kwamba, haoni tatizo la kusajiliwa CCJ huku pia akisema hawezi kuzuia watu kumhusisha na chama hicho kama mgombea hapo Oktoba.

CCJ imekuwa ikitikisa nchi tangu taarifa zake kuchapishwa kwenye vyombo vya habari, kwani kuna majina makubwa yanatajwa kuwemo akiwemo Spika Sitta, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, John Malecela, lakini wote wamekanusha.

Hata hivyo, mwasisi wa CCM Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuonya kwamba bila CCM madhbuti nchi itayumba na upinzani wa kweli ungetoka ndani ya CCM onyo ambalo wadadisi wa mambo ya siasa anaona kama linakaribia.
Tags:

0 comments

Post a Comment