Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mpasuko mpya CCM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HUKU Kamati ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ikiwa imeongezewa muda kukamilisha usuluhishi miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kundi jipya limeibuka ndani ya chama hicho likitaka vigogo kadhaa wafukuzwe uanachama.
Kundi hilo limetoa majina 16 ya vigogo wa kufukuzwa, maazimio matano mazito na limezitaka serikali za nchi takriban nne zinazoaminika kutumika kuhifadhi mabilioni ya vigogo nchini zisaidie kurejesha fedha hizo.
Raia Mwema imetumiwa nakala ya tamko hilo, ambalo linaitaka Serikali za Tanzania kuomba msaada nchi za Uswisi, Costa Rica, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na serikali za visiwa vya Man na Jersey, na nchi nyingine zinazotumika kuficha taarifa za kodi, kurejesha fedha zilizowekwa huko na viongozi wa Tanzania.
Kutoka katika tamko hilo, wanaotajwa ili wafukuzwe ambao kwa sasa tunahifadhi majina yao ni pamoja na mmoja aliyepata kuwa waziri mkuu; mawaziri wawili wa Serikali ya Awamu ya Tatu; mbunge na mfanyabiashara maarufu; aliyepata kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi; na mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Katika orodha hiyo, wamo pia wabunge 11 wa Bunge la sasa wa Mikoa ya Arusha, Mara, Kagera, Kilimanjaro, Shinyanga, Dar es Salaam na Mbunge wa Viti Maalumu ambaye pia ni Waziri. Sehemu kubwa ya wabunge hao ni wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa na wengine ni waliowahi kuwa viongozi wa umma, wenye ukwasi mkubwa.
Kwa mujibu wa tamko la kundi hilo, vivogo hao wa ndani ya CCM wanahusishwa na kashfa 17 za kitaifa na kimataifa ambazo zimetajwa kuwa ni Loliondo, IPTL, Commodity Import Support, Mgodi wa Kiwira, Akaunti ya EPA, kampuni za Meremeta Ltd, Mwananchi Gold, Deep Green Finance, na Tangold.
Kashfa nyingine ni rada, ununuzi wa ndege ya Rais (Gulfstream 500), Richmond, Dowans, magari, silaha na helikopta za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), silaha haramu, dawa za kulevya, uuzaji wa maeneo wazi, misamaha ya kodi, ujenzi wa jengo Benki Kuu na uuzaji wa maeneo ya ufukwe Dar es Salaam.
Kundi hilo ambalo limesambaza tamko hilo kwenye mtandao, limejitambulisha kama wapiganaji wa kweli CCM- na kauli mbiu yake ni “Kwa ajili ya Taifa letu; sasa na baadaye.”
Katika mawasiliano hayo, ambayo Raia Mwema imeyapata, hakuna majina ya wanaoliunda kundi hilo, lakini limenukuu mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 na kuutumia kujenga hoja.
Mwongozo huo wa 1981 unasema: “Huko nyuma tulishinda katika mapambano yetu kutokana na umoja wetu wa kitaifa, usahihi wa siasa yetu na uongozi bora wa chama.
“Leo na katika siku za usoni tutahitaji umoja imara zaidi, siasa sahihi na uongozi bora wa chama.. vibepari na vibwanyenye vya humu nchini vimeonyesha dhahiri uhasama wao dhidi ya maslahi ya wakulima na wafanyakazi, umoja wa sasa lazima usimame juu ya misingi iliyo wazi na sahihi, misingi ya ujamaa; kwa hiyo ni umoja wa wakulima na wafanyakazi na wale wote wanaounga mkono kwa vitendo ujenzi wa ujamaa nchini.”
Kama alama ya utambulisho wake, kundi hilo linasema: “Sisi ni wananchi wa Tanzania. Sisi vile vile ni wana CCM ambao tumechoshwa na mwelekeo wa kisiasa nchini, na hasa kuhusishwa kwa baadhi ya wana-CCM na vitendo vya ufisadi ambavyo vimekipaka matope chama, lakini zaidi tumechoshwa na Serikali inayoongozwa na chama chetu kuhusishwa na ufisadi katika wizara, idara, wakala na taasisi zake mbalimbali.
“Kama Watanzania hatuwezi tena kukaa kimya na kusubiri watu wengine waje kutuletea mabadiliko; hatuwezi tena kukaa pembeni na kuacha raslimali za nchi yetu ziendelee kugawanywa mikononi mwa kikundi cha watu wachache kana kwamba ni haki yao ya kuzaliwa; hatuwezi tena kukaa kimya tukizionea haya chembechembe za ufisadi ndani ya chama na kwenye serikali.”
Kwa mujibu wa maelezo ya kundi hilo, mabadiliko yanahitajika ambayo yanapaswa kuwa ajenda kuu ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu. Kipengele hicho cha kuhimiza mabadiliko kinasema:
“Mabadiliko ya kweli yatakayofumua fumua mtandao wa uhalifu na ufisadi nchini na hatimaye kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao na kwa CCM na kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anayo nafasi ya kufanikiwa katika Taifa lake na kuhakikisha tunaweka misingi ya mafanikio kwa kizazi kipya cha Watanzania”.
Kundi hilo lmejitambulisha pia kuwa kuwa baadhi yao ni wabunge na viongozi wa CCM, wakiwamo kutoka baadhi ya jumuiya za chama hicho na wengine ni wanachama wa kawaida, na kwamba limetoa tamko hilo ikiwa ni sehemu ya juhudi ya wazi ya kujikosoa kwa mujibu wa mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 (ibara ya 58).
Tamko hilo linaeleza kuwa Watanzania wengi wamechoshwa na ufisadi uliokubuhu na utendaji duni na wa kusikitisha wa vyombo vya Serikali, hali inayowafanya kutojali masuala muhimu ya nchi huku kila mmoja akitazama masuala binafsi na ya familia.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, tamko hilo linaweka masharti kwa CCM kuekelea Uchaguzi Mkuu kwamba; “Chama cha Mapinduzi hakiwezi na hakipaswi kusimama kuomba kura tena kwa wananchi isipokuwa baada ya ushahidi wa wazi wa vitendo wenye kung'oa chembechembe zote zenye kuendeleza vitendo vya rushwa na hongo, uzembe, kutokuwajibika, ubadhirifu, ufujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka kwa ajili ya manufaa binafsi ya watu wafanyao hayo, yaani ufisadi.
Kutokana na mtazamo huo, kundi hilo limebainisha maazimio yake matano. Azimio namba moja linasomekana: “Tunakataa mpango wowote, juhudi zozote na mchakato wowote utakaolenga kutafuta umoja na upatanishi kati ya chembe za ufisadi ndani ya chama, tunaamini hakuna umoja na ushirika wa kweli unaoweza kupatikana na mafisadi au na wale wanufaikaji wa ufisadi. Chama cha Mapinduzi hakina nafasi kwao au makuwadi wao.
Azimio namba mbili linaeleza: “Tunakataa juhudi zozote za kujaribu kuwaondoa wanachama wenye uwezo wa kuongoza na walioonyesha uwezo huo kwa vitendo kwa kisingizio cha umri ili kuwapisha “vijana”. Tunaamini kama Taifa tutafanya kosa kubwa sana kuamua mara moja kuliacha Taifa mikononi mwa vijana kwa sababu ya umri tu. Tunaamini kila mwana CCM mwenye uwezo wa kuongoza na anayekubalika kwa wananchi wake asinyimwe nafasi ya kuongoza kwa kisingizio cha umri.
“Tunawaunga mkono wana CCM ambao mbali ya kuwa na uwezo wa kuongoza wameamua kukaa pembeni ili kuruhusu wanachama wengine kuingia katika safu ya uongozi. Uamuzi huu usionekane kuwa ni udhaifu au ni njia ya kuwalazimisha wengine kuufuata. Kustaafu nafasi ya uongozi kunaweza kufanywa na mtu yeyote pasipo kujali umri wake.
Azimio namba tatu linaeleza: “Kutetea raslimali za Taifa letu na utajiri wa nchi yetu kwa kukusudia kuzuia mikataba na mipango yoyote yenye kurundika utajiri wetu mikononi mwa wafanyabiashara wakubwa bila kujali maslahi ya leo ya Taifa au yale ya kizazi kijacho.
“Tunachukua msimamo huo tukiamini kuwa kama viongozi wa CCM tunalojukumu la kichama kueneza matunda ya Uhuru kwa wananchi wote kwa ajili ya manufaa yao na maendeleo ya Taifa kwa jumla. Kwa mujibu wa Ibara ya 17:2 ya Katiba ya CCM. Jukumu hili si la wapinzani au wafadhili wa kigeni; ni jukumu letu kama Watanzania na kama wana CCM.”
Azimio namba nne: “Kupigania haki ya kila Mtanzania kugombania nafasi ya uongozi pasipo kulazimishwa kujiunga na chama cha siasa. Kama Watanzania kwanza na kama wana CCM, tunaamini haki ya kuchaguliwa isiunganishwe na ulazima wa kujiunga na chama
cha siasa kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vile vile kupingana na Tamko la Haki za Binadamu la 1948 ambalo Tanzania imeliridhia.
“Chama cha Mapinduzi na wana CCM hatuogopi wagombea binafsi, kwani tunaamini chama chetu kinakubalika, kina uwezo wa kuongoza bila kujali wagombea wengine wanatoka wapi au wanapatikana vipi.”
Azimio namba tano: “Kuhakikisha mfumo bora wa kuwajibika na kuwajibishana unakuwapo katika Serikali kwa kupendekeza mabadiliko ya Katiba na sheria mbalimbali ili hatimaye mfumo ambao umefungua milango ya kifisadi unakosolewa, kubomolewa na kubadilishwa na mfumo ambao hautatoa nafasi kwa watu na vikundi vya watu kuneemeka kwa kutumia mbinu za kifisadi.
“Bila ya kuubadili mfumo huu tunaamini mafisadi wataendelea kuibuka kati yetu na kama Taifa tutaendelea kupiga kambi kwenye hili bonde la ufisadi miaka nenda rudi. Ni lazima tuubadili mfumo huu tukizingatia vile vile malengo ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupamba na Umasikini namba mbili (MKUKUTA II).”
Katika hatua nyingine inayoweza kuhusishwa na juhudi za kundi mojawapo kati ya yanayopingana CCM, Chama Cha Jamii (CCJ) jana Jumanne kilipata usajili muda jana.
Chama hicho kama ilivyo kwa kundi hili linalojitambulisha kama wapiganaji wa kweli, kimekuwa kikihusishwa na baadhi ya vigogo wa CCM lakini ambao hawajajitokeza hadharani.
Hali hiyo ya kuhusishwa vigogo wa CCM na CCJ, na kisha kuibuka kwa kundi hili jipya la wapiganajii wa kweli, inatajwa kuchochewa na udhaifu wa kiuongozi ndani ya CCM.
Hata hivyo, wananchi wengi wamekuwa wakishangazwa na vigogo wanaodai wanapenda mabadiliko ndani ya CCM lakini waoga kujitokeza hadharani, ikielezwa kuwa kujificha huko ni udhaifu mkubwa kwa makundi hayo kwa kuwa huo si ujasiri unaostahili kuchochea mabadiliko nchini.
Tags:

0 comments

Post a Comment