IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAHOJI UMAKINI WA NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI KATIKA SUALA HILO
James Magai na Hussein Kauli
NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali jana alikuwa kwenye wakati mgumu mbele ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa wakati mabosi wa mhimili wa sheria hao walipohoji umakini wake katika kushughulikia rufaa dhidi ya uamuzi wa kuruhusu mgombea binafsi.
Wakiongozwa na Jaji Mkuu Augustine Ramadhani, majaji hao waliamua kuwa hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya kuruhusu mgombea huru ndiyo inayotambuliwa wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba na baadaye hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Ilifikia wakati Jaji Mkuu Ramadhan alisema: "Inasikitisha kuwa (Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju) unatoka kwenye ofisi ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali), lakini unalalamika kuwa hujasoma list of authorities. Sijui tunawapa mfano gani wengine!"
Mahakama Kuu iliruhusu mgombea binafsi baada ya mwenyekiti wa chama cha kisiasa cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila kufungua kesi akidai kuwa sheria za nchi kuhusu haki ya kupiga kura na kupigiwa kura inapingana na katiba ya nchi kutokana na kutamka kuwa mgombea ni lazima apitishwe na chama.
Lakini tangu hukumu hiyo ilipotolewa mwezi Juni, 2006 ikitaka mchakato wa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi ufanyike katika kipindi cha miezi sita, hakuna kilichofanyika na badala yake serikali ilikata rufaa ikipinga mamlaka ya Mahakama Kuu kutafsiri katiba.
Rufaa hiyo ilitarajiwa kusikilizwa jana mbele ya jopo la majaji hao saba wa Mahakama ya Rufaa, lakini serikali iliomba suala hilo liahirishwe kwa muda wa miezi minne ili ijipange kikamilifu.
Akiwasilisha maombi hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu (DAG), George Masaju alisema sababu za maombi yao ni kutokuwepo kwa wakili mwenza anayeshirikiana naye ambaye anaifahamu vizuri kesi hiyo na ambaye anauguliwa na mgonjwa.
Alidai kuwa yeye (DAG) hakupata muda wa kuipitia orodha ya kesi zitakazotumiwa na upande wa utetezi kwa kuwa walichelewa kuipata, akidai kuwa waliipata Jumamosi ambayo ni siku ya mapumziko.
"Mheshimiwa Jaji, kama utaridhia naomba shauri hili liahirishwe ili tupate muda wa kuzipitia hoja za upande wa pili ili tuweze kuisaidia mahakama kwa kuwa tuliwapelekea wenzetu List of ‘Authorities’ (orodha ya kesi za rejea wakati wa usikilizwaji kesi husika) Ijumaa na wenzetu walituletea list of authorities zao Jumamosi," alisema Masaju.
"Hivyo hatukuweza kupata muda wa kuzipitia. Pia mwenzetu mmoja (wakili mkuu wa serikali, Mathew) Mwaimu alinipigia simu kuwa baba yake ni mgonjwa hivyo akalazimika kwenda kushughulikia matibabu yake. Hivyo hataweza kushiriki vizuri kutokana na tatizo hilo."
Maelezo hayo yalionekana kumshangaza Jaji Ramadhani na akamuuliza maswali mengi kutokana na kitendo cha serikali ambayo ni mrufani kuchelewa kupeleka orodha hiyo ili nao wapewe orodha ya upande wa pili mapema wakati suala hilo lilikuwa likijulikana kwa muda mrefu.
Sehemu ya mahojiano baina ya Jaji Mkuu Ramadhani na Naibu Mwanasheria Masaju ni kama ifuatavyo:
CJ: Hili suala lilijulikana tangu Januari mwaka huu, kilichowafanya mpeleke list of authorities Ijumaa ni nini?
DAG: Mheshimiwa Jaji, suala hili ni nyeti na tunakuja hapa ili kuisaidia mahakama hivyo tulihitaji kufanya ‘research’ (utafiti) ili tuje na majibu ya kuridhisha.
CJ: Nakubali hili ni suala nyeti lakini ninyi ndio mliokata rufaa na hiyo research ilipaswa kufanyika mapema. Sasa ilikuwaje mpaka Ijumaa ndio mnakurupuka kupeleka list of authorities?
DAG: Mheshimiwa Jaji mimi hili suala nililipata kwa mara ya kwanza nilipoteuliwa kuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali kwa hiyo nilikuwa sijapata muda wa kutosha kulifanyia kazi.
CJ: Kwa hiyo mnahitaji muda gani wa kutosha kufanya research yenu?
DAG: Hizi zenyewe sijazisoma (list of authorities za utetezi), sitaki kuwa muongo. Nitazijibuje hata sijazisoma? Mkiridhia naomba shauri hili liahirishwe hadi hapo msajili atakapopanga.
CJ: Ninyi ndio mtuambie ni lini mtafanya hiyo research.
DAG: Muda wowote atakaopanga.
CJ: Msajili anaweza kupanga hata kesho
DAG: Tunaomba muda wa kutosha kwa sababu hata hicho kilichomo kwenye hizi list of authorities sikijui.
CJ: Muda gani? Mnatakiwa muwe 'specific'(muainishe muda) kwa sababu nyie ndio mnajua ni muda gani utakaowatosha.
DAG: Mheshimiwa Jaji, hata huko mahakama imekuwa ikipanga bila kutuhusisha
CJ: Sasa leo mnahusishwa hivyo tajeni muda ambao mnaona utawatosha.
DAG: Tunaomba mahakama ipange tu.
CJ: Inasikitisha kuwa unatoka kwenye ofisi ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) lakini unalalamika kuwa hujasoma list of authorities sijui tunawapa mfano gani wengine!
DAG: Mheshimiwa Jaji, suala hili si sawa na hesabu za moja jumlisha moja ni sawasawa na mbili.
CJ: Mkata rufaa tena kutoka ofisi ya AG ndio kiongozi wa bar lakini bado unalalamika kuwa hukusoma list of authorities.
DAG: Kwa hili sitaweza kujitetea sana
CJ: Hakuna kujitetea, tuwapeni muda gani mjiandae ?
DAG: Tunaomba miezi minne tuweze kujipnga vizuri.
Baada ya mahojiano hayo, wakili Richard Rweyongeza, anayemwakilisha Mchungaji Mtikila alikubaliana na upande wa serikali wa kuahirisha rufaa hiyo, lakini akasema: "Ili haki itendeke kwa upande wetu, tuko tayari kuahirishwa kwa muda wa wiki moja."
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote kesi hiyo iliahirishwa kwa muda ili kuwapa nafasi majaji kuamua na baadaye Jaji alisema mahakama imekubali kuahirisha shauri hilo kwa muda wa miezi miwili hadi Aprili 8 mwaka huu, lakini akaagiza mchakato wa mgombea binafsi uendelee kama kawaida kwa kuwa uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu bado unasimama hadi hapo uamuzi wa Mahakama ya Rufaa utakapotolewa vinginevyo. Kabla ya kuomba kesi hiyo kuahirishwa, DAG Masaju aliomba mwongozo wa mahakama kuhusu kesi hiyo kusikilizwa na jopo la majaji saba badala ya watatu.
Katika kutia uzito hoja zake, DAG Masaju alinukuu Ibara za 118 (i), 122, zinazozungumzia idadi na majaji wanaopaswa kusikiliza kesi katika Mahakama ya Rufaa, pamoja na kanuni ya 27 ya Mahakama.
Jaji Ramadhani alikubaliana na maelezo ya ibara hizo, lakini akasema hakuna kosa kwa majaji zaidi ya watatu kusikiliza kesi kwa kuwa ibara hizo zimetaja kiwango cha chini tu kuwa wasiwe chini ya watatu.
Alitoa mfano kuwa hata mwaka 1984 akiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Jaji Mkuu wa Tanzania Francis Nyalali alitumia jopo la majaji watano kusikiliza rufaa ya kesi ya mauaji na kwamba kama ni kosa basi hilo kosa lilishafanyika siku nyingi.
"Lakini kwa sababu hilo halikuwa kosa, ndo maana katiba haikutaja kuwa lazima wawe watatu tu bali inasema wasiwe chini ya watatu. Kwa sababu ulitaka mwongozo basi ndo umeshapata mwongozo wa kesi hiyo basi sasa sidhani kama una hoja ya kupinga na naomba tuendelee,"alisema Jaji Ramadhani.
Majaji wengine katika rufaa hiyo ni Eusebio Munuo, Januari Msofe, Benard Luanda, Mbarouk Mbarouk, Engela Kileo na Sauda Mjasiri.
You Are Here: Home - - Majaji: Mgombea binafsi ruksa 2010
0 comments