IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WABUNGE wa CCM jana walikutana kwa faragha katika kile kilichoelezwa kuwekana sawa kuhusu muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ambao tayari wabunge wengi wameonyesha kuupinga na kuishinda serikali baada ya hoja zao kukubaliwa.
Kikao hicho cha juzi kilifanyika kuanzia saa 8:00 mchana katika ukumbi wa Msekwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho, zinasema lengo kuu la wabunge wote wa CCM kukutana ni kuwekana sawa kuhusu muswada huo, ambao unaotarajiwa kuwasilishwa kwenye kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma.
Chanzo cha Habari kimeeleza kwamba wabunge wa CCM wameibuka na ushindi dhidi ya serikali kwa kufanikikiwa kushawishi kufanyika marekebisho makubwa katika muswada huo.
Kwa mujibu wa ratiba ya awali iliyorekebishwa na kamati ya uongozi ya bunge, muswada huo ulikuwa uwasilishwe jana na wabunge kupewa siku mbili za kuujadili, lakini haukuwasilishwa, taarifa zilizolifikia Mwananchi jana zinasema kuwa utawasilishwa kesho.
Muswada huo, ulirudishwa kwenye kamati ya katiba, sheria na utawala kwa ajili ya kuufanyia marekebisho kabla ya kurejesha bungeni kesho.
Spika wa Bunge Samuel Sitta alilitangazia Bunge jana kuwa kamati hiyo, itakutana kujadili na kuufanyia marekebisho muswada huo, huku akiwahimiza wabunge wenye michango yao kuhusu muswada huo kuwasilisha katika kamati ili ifanyiwe kazi.
"Kamati ya kudumu ya Bunge ya katiba, sheria na utawala itakutana leo saa 5:00 hii mchana (jana) kupitia muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, waheshimiwa ambao si wajumbe wa kamati, lakini wana maoni wanaweza kupeleka maoni yao kwa kamati," alisema Sitta.
Lakini habari zaidi zinabainisha kuwepo kwa mvutano ndani ya kikao hicho cha wabunge, huku wakishikilia msimamo wao wa kutaka muswada huo ufanyiwe marekebisho makubwa kadiri ya mapendekezo yao waliyoyatoa kwa nyakati tofauti.
"Kikubwa katika mkutano huo ni mjadala kuhusu Muswada wa sheria ya gharama ya uchaguzi, lengo ni kuwekana sawa ili kuwa na msimamo mmoja kuhusu muswada huo kama wabunge wa CCM," alisema mtoa habari wetu.
Alifafanua kuwa wabunge wameshikilia msimamo wao wa kutaka kuondolewa kwa baadhi ya vipengele kwenye muswada huo huku wakitaka uanze kutumika katika Bunge lijalo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mtoa habari huyo alitaja baadhi ya vipengele ambavyo wawakilishi wa wananchi, kupitia CCM wametaka viondolewe ni pamoja na kinachompa uwezo msajili wa vyama vya siasa kumowondoa mgombea Ubunge anapoona inafaa na kwa kushauriana na katibu mkuu wa chama husika.
Kwa mujibu wa habari hizo, wabunge hao wamedai kipengele hicho kinaondoa uwezo wa chama kuteua wagombea wake na kujenga mazingira yanayompa nguvu na jeuri msajili wa vyama na makatibu wakuu wa vyama vya siasa hivyo kuwa tishio la demokrasia ndani ya vyama hivyo.
"Msimamo tulioweka ni kuwa muswada ufanyiwe marekebisho makubwa ndipo uletwe bungeni, eneo kama msajili anapopewa nafasi ya kuondoa mgombea tumelikataa, pia tunataka muswada uanze kutumika bunge lijalo,"alisema mmoja wa wabunge hao.
Habari zimeeleza kuwa kutokana na ukweli wa kuwepo kwa kasoro nyingi ndani ya muswada huo, wabunge wamependekeza ufanyiwe marekebisho makubwa kabla ya kuwasilishwa bungeni, huku wakionya kuwa iwapo serikali itawasilisha bila marekebisho yaliyopendekezwa utakwamishwa kama ulivyokuwa Muswada wa Sheria ya Baraza la Usalama wa Taifa.
"Kamati inakutana leo (jana), lengo ni kufanyia marekebisho makubwa muswada tuliyopendekeza sisi wabunge wa CCM, hilo halina mjadala kwani jana tulikubaliana hilo,"alisema mmoja wa wabunge wa CCM.
Wakishiriki katika semina kuhusu muswada huo juzi iliyoandaliwa na Chama Cha wabunge cha Kupambana na Rushwa Afrika (APNAC), tawi la Tanzania chini ya Mwenyekiti wake, Zainab Gama ambaye ni mbunge wa Kibaha mjini, takriban wabunge wote waliochangia mada waliukataa muswada huo wakishauri kuondolewa kwa mapungufu waliyoainisha ndipo uwasilishwe bungeni.
You Are Here: Home - - Wabunge CCM waishinda serikali, ni kuhusu muswada gharama za uchaguzi
0 comments