IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
RAIS wa Zanzibar, Amani Abeid Karume jana alitumia sherehe za miaka 33 ya kuzaliwa kwa CCM kupiga vijembe, akisema si kila anayetaka uongozi anaweza kupata kwa kuwa wapo walioutaka, lakini hawajaupata.
Karume amesema hayo wakati Wazanzibari wakiwa wameungana katika suala la kuanzishwa kwa serikali ya mseto kuviepusha visiwa hivyo kuingia kwenye vurugu ambazo hutokea kila baada ya matokeo ya uchaguzi wa rais kutangazwa.
Baraza la Wawakilishi liliridhia hoja binafsi ya kuundwa kwa serikali ya mseto baada ya uchaguzi mkuu, ikiwa ni njia ya kuondoa vurugu zinazosababishwa na upande mmoja kupinga matokeo, ambayo yamekuwa mazuri kwa CCM tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi.
Jana, kwa mafumbo huku akikwepa kugusia hali ya mambo visiwani Zanzibar, Karume alisema kwa mazingira ya sasa, CCM itabakia kuwa mwalimu kwa vyama vingine.
Karume ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), alikuwa mjini Bagamoyo, mkoani Pwani ambako alihutubia katika uzinduzi wa madhimisho hayo ya miaka 33 ya kuzaliwa CCM, ambayo iliundwa kutokana na muungano wa vyama viwili; Tanu, ambayo iliongoza harakati za uhuru Tanganyika, na ASP ambayo iliongoza mapinduzi visiwani Zanzibar.
Karume alisema CCM kama mwalimu inapaswa isichoke kwa kuwa mwalimu hachoki, hivyo inatakiwa ijijenge zaidi na kuimarisha umoja ndani ya chama kwa kuwa ni vitu muhimu katika nchi.
"Chama cha Mapinduzi lazima tuendelee kuwa mwalimu," alisema mtoto huyo wa kiongozi wa mapinduzi na rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
"Si kila anayetaka uongozi anapata na watu wana hamu nao... mwalimu hachoki na mwalimu mzuri ndio hachoki kabisa."
Rais Karume, ambaye anamaliza vipindi vyake viwili vya urais wa Zanzibar mwezi Oktoba na ambaye anapendekezwa aongezewa muda kidogo ili afanye marekebisho yatakayondoa siasa za chuki, alisema misukosuko ya kisiasa inaweza kudhibitiwa kwa kutumia meza za mazungumzo tu.
Alisisitiza kuwa wamepitia katika misukosuko mingi ya kisiasa, lakini mazungumzo na kujenga na kuimarisha chama kumesaidia kwa kuwa ni vitu muhimu katika nchi.
"Mengi yameshasemwa, lakini nawashukuruni kwa kujenga na kuimarisha umoja ndani ya chama kwa kuwa ni vitu muhimu sana katika nchi," aliongeza.
Katibu mkuu wa CCM, Yusufu Makamba alisema chama chao kina idadi kubwa ya wanachama, kitu ambacho kinakifanya kiongoze.
"CCM ina wanachama zaidi ya milioni nne na mashina zaidi ya 400,000 hivyo tutaingia kwenye uchaguzi kwa kishindo," alisema Makama.
Alisema chama hicho kitaingia kwenye uchaguzi kwa kutegemea mtaji wao ambao ni Rais Jakaya Kikwete, hivyo wale waliodai atoswe, wataendelea kuwa ni wehu.
"Mtaji wetu ni Rais Kikwete kwa kuwa anakubalika kuliko hata chama, ndio maana niliwaita wehu wanaodai tumtose," alisisitiza Makamba.
Katika maadhimisho hayo Rais Karume alikaribisha wanachama wapatao 13,174, waliojiunga na chama hicho kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini.
Naye makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa alisema kuwa yeye ndiye aliyemuandaa Rais Jakaya Kikwete tangu akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa kijana mdogo na kuwa alikuwa mwanachama mwaminifu tangu wakati akiwa kijana mdogo.
Akihutubia wanafunzi wa vyuo vikuu vya mjini Dodoma, Msekwa alisema CCM kinawaandalia wasomi hao mazingira ya kuundiwa mkoa wao wa kichama.
Msekwa, ambaye alikuwa na kazi ya kuwasimika makamanda wa vijana wa wilaya zote za mkoa wa Dodoma pamoja na kamanda wa mkoa, alisema kuwa utaratibu wa kuanzisha mkoa wa kichama sio mgeni kwa CCM kwa kuwa ulikuwepo tangu zamani wakati Jeshi lilipokuwa mkoa.
You Are Here: Home - - Karume apiga vijembe wanaotaka uongozi
0 comments