Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dk Slaa amvaa Waziri Simba ataka Rais amwajibishe kwa kuiaibisha Serikali

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mbunge wa Karatu, Dk Willbroad Slaa ambaye amemtaka Rais Jakaya Kikwete kumchukulia hatua za kinidhamu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) Sofia Simba kwa kuiaibisha Serikali

MBUNGE wa Karatu, Dk Willbroad Slaa amemtaka Rais Jakaya Kikwete kumuwajibisha Sofia Simba iwapo waziri huyo wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), hatajiwajibisha kwa kujiuzulu kutokana na Bunge kuukataa muswada aliouwasilisha wa Sheria ya Baraza la Usalama wa Taifa wa mwaka 2009.

Hii ni mara ya pili kwa Bunge kuukataa muswada huo, ambao umeelezewa kuwa unalenga kumpunguzia mamlaka rais, ambaye ni amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama.

Dk Slaa alisema hayo jana wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Star Tv katika kipindi cha "Tuongee Asubuhi",

akisema kuwa suala hilo linaonekana kuwa dogo, lakini ni kubwa na iwapo litapuuzwa na kwamba itakuwa ni hatari kwa maslahi ya taifa.

"Kwa kuwa muswada huu umekataliwa kwa mara ya pili na Bunge, ni dhahiri kuwa Waziri Simba anatakiwa ajiuzuru na asipofanya hivyo, Rais (Jakaya) Kikwete ana jukumu la kumuajibisha," alisema Dk Slaa.

"Rais anaweza kulivunja Bunge endapo muswada wowote unapokataliwa kupitishwa na wabunge kwa mara ya pili mfululizo, lakini kwa sasa haiwezekana kwa kuwa tunaelekea katika uchaguzi mkuu. "

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa ibara ya 97 ya katiba ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 69 cha kanuni za Bunge, Waziri Simba angetakiwa kujiuzulu mara moja kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Lakini akaongeza kuwa Waziri Simba hana utamaduni huo na hivyo Rais Kikwete anapaswa kuchukua jukumu la kumuwajibisha.

"Lazima Rais achukue jukumu la kumuwajibisha Waziri Simba ajiuzulu kwa kuifikisha serikali katika hatua hiyo kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo... amemuhabisha rais na serikali yake," alisema mbunge huyo.

"Wakati nachangia hoja yangu Bungeni nilinukuu kifungu hiki nikitaka kuonyesha jinsi Waziri Simba alivyoifikisha serikali pabaya, lakini mheshimiwa Naibu Spika alifahamu hilo akaona hakuna haja ya kufika huko."

Pia alitaka watendaji walio chini ya rais pamoja na kamati ya Bunge iliyoupitia muswada huo kabla ya kupelekwa Bungeni, kuwajibishwa mara moja.

Akizungumzia kasoro zilizoko kwenye muswada huo, Dk Slaa alisema kifungu cha 5 (2) g, hakikueleza wazi maadui wa taifa, hivyo kinatoa nafasi kwa baadhi ya watu kuonekana maadui wakati sivyo.

Aliongeza kuwa muswada huo hauelezi wazi maslahi ya taifa yaliyokusudiwa jambo linaloweza kusababisha utata.

Wakati huohuo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally amesema kitendo cha mswada huo kukataliwa na Bunge mara mbili kina sura tatu, akidokeza kuwa mojawapo ni tatizo la makundi ndani ya CCM.

Bashiru alisema kuwa sura nyingine inayoonekana katika sakata hilo ni kuwa serikali haitilii maanani maoni ya Bunge na hivyo wabunge wameamua kuwa makini kwa kila jambo.

Kwa mujibu wa Bashiru, hali hiyo pia inatokana na wabunge kuzidi kuwa makini.

"Katika siku za hivi karibuni mahusiano kati ya Bunge na serikali yamekuwa yakisuasua, na mfano mzuri ni katika suala la (utoajo zabuni kwa kampuni ya) Richmond," alisema Bashiru.

"Kinachoonekana ni kuwa kamati ya wabunge wa CCM haina nguvu ya kuishawishi serikali na inawezekana ni kwa sababu ya mgawanyiko uliopo ndani ya chama.

Lakini pia hali hii inaweza kuwa imetokana na serikali kutotekeleza mambo ambayo Bunge linayasema, kwa mfano mambo ya Richmond. Kwa hiyo na wabunge nao wamekuwa makini na wameamua hakuna kitu kibovu kitakachipita."

Msomi huyo ambaye pia ni mchambuzi wa siasa za ndani na nje ya nchi alisema makundi ndani ya chama tawala yamesababisha serikali ishindwe kutumia kamati ya wabunge wa chama tawala kupitisha mambo yake ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Naye mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Samuel Ruhuza amesema kitendo cha kukataliwa mara mbili kwa muswada huo ni aibu na kuwataka waliohusika kuwajibika ama kuwajibishwa.

Ruhuza, ambaye kwa taaluma ni mwanasheria, alisema pia kuwa urafiki baina ya rais na baadhi ya watu unachangia kosoro hizi kutokea.

"Mimi ningemshauri rais awe kama Mungu... rafiki wa Mungu ni yule anayetenda mambo mazuri tu. Urafiki wake (rais) umezidi; watu hawawajibiki kabisa; wanadhani mtu kuwajibika ni mpaka akamatwe na rushwa tu," alisema Ruhuza.
Tags:

0 comments

Post a Comment