Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wanajeshi wa JWTZ watiwa mbaroni na Polisi kwa madai ya a kumuua mtoto wa Chifu Fundikira

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SIMANZI, MAJONZI VYATAWALA MSIBA WA FUNDIKIRA
Marehemu Swetu

HALI ya huzuni ilitanda nyumbani kwa marehemu Swetu Fundikira ambaye anasemekana alifariki kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jumamosi usiku baada ajali iliyohusisha gari lake na askari hao sehemu za Kinondoni kwa Manyanya. Tukio hilo lilisababisha marehemu kukimbizwa Hospitali ya Muhimbili ambako alifariki siku iliyofuata. Kwa mujibu wa kaka mkubwa wa marehemu, mazishi yatafanyika kesho katika makaburi ya Mwananyamala.


ASKARI wawili wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa Chifu Abdallah Fundikira baada ya kumshushia kipigo usiku wa kuamkia juzi.

Askari hao, ambao ni mtu na mkewe kutoka kambi ya Lugalo, wanadaiwa kumuua kijana huyo, Swetu Fundikira baada ya kumpiga wakiwa na mwanajeshi mwingine mmoja katika ugomvi wa barabarani uliotokana na askari hao kudai kuwa walifanyiwa fujo na kutukanwa na gari ambalo Swetu na wenzake walikuwa wamepanda.

Habari zilizolifikia Mwananchi jana kutoka kwa watu walioshuhudia tukio hilo na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Elias Kalinga zinasema marehemu alifariki jana usiku katika Hospitali ya Muhimbili, kufuatia kipigo cha wanajeshi hao.

Habari kutoka kwa watu walioshuhudia tukio hilo zinasema kuwa askari hao walimpiga kijana huyo juzi katika eneo la Kinondoni A kwa madai kuwa aliwachomekea na gari lake.

"Askari hao walimshusha kwenye gari eneo la Kinondoni A na kuanza kumshushia kipigo. Baada ya kumpiga walimchukua na kumwingiza ndani ya gari lao na kuondoka naye," alisema mmoja wa mashuhudua hao, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Shuhuda huyo aliongeza kuwa baada ya kuondoka naye walidhani kuwa wanajeshi hao walimua kumpeleka hospitalini baada ya kumuumiza kwa kipigo hicho, lakini walipofika njiani walimshusha na kuanza kumpiga tena hadi msamaria mwema mmoja alipowaona na kutoa taarifa kituo cha polisi cha Selander Bridge.

"Tulidhani wanampeleka hospitalini kumbe huko mbele ya safari walipofika karibu na Hospitali ya Muhimbili walimshusha na kuendelea kumpiga. Ndipo raia mwema alipowaona ma kutoa taarifa katika kituo cha Salender Bridge. Askari polisi walifika eneo la tukio na kuwakuta wakiendelea kumpiga ndipo wakawatia mbaroni wanajeshi hao," alisema shuhuda huyo.

Kamanda wa polisi mkoani Ilala, Faustine Shilogile alikiri kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa na askari wa kituo cha Polisi Salender Bridge, lakini akasema kesi hiyo iko Kinondoni na kwamba askari wake walisaidia tu kuwakamata askari hao na kuwapeleka kituo cha polisi cha Oysterbay.

"Wasiliana na RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) wa Kinondoni yeye atakupa taarifa kamili," alisema Kamanda Shilogile.

Kamanda wa polisi Kinondoni, Elias Kalinga alilithibitishia Mwananchi kuwa ni kweli watuhumiwa hao wanashikiliwa katika kituo cha Oysterbay kwa tuhuma za mauaji ya kijana huyo wa Chifu Fundikira.

"Ni kweli kabisa watuhumiwa hao tunao hapa kituoni. Mmoja anaitwa Sajenti Rhoda Robert, ambaye ni askari wa Jeshi la Wananchi kutoka Lugalo, na Koplo Ali Ngumbe, ambaye pia ni askari wa JWTZ," alisema Kamanda Kalinga.

Mbali na watuhumiwa ho wawili ambao alidai ndio waliohusika kumpiga marehemu, Kamanda Kalinga anasema mtuhumiwa mwingine anayejulikana kwa jina la Private Mohamed Ngumbe, ambaye pia alikuwa kwenye gari moja na watuhumiwa hao wawili hajakamatwa na bado anasakwa.

Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kumpiga marehemu usiku wa kuamkia juzi, baada ya kuonyesha ubabe wakati wakiendesha magari yao na kwamba marehemu alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Akielezea tukio Kamanda Kalinga alisema askari hao walikuwa wakitoka kwenye shughuli zao binafsi wakiendesha gari lao binafsi huku wakiwa wamevaa kiraia.

Alisema Swetu alikuwa akitoka kwenye shughuli zake na ndipo walipokwaruzana kutokana na marehemu kukataa kuwapisha wakati wakiwa kwenye makutano ya barabara.

"Askari hao walimpigia honi marehemu wakitaka awapishe, lakini akakataa ndipo walipompiga baada ya kukataa kuwapisha," alisema Kamanda Kalinga.

"Wao (watuhumiwa) wanadai kuwa marehemu aliwatukana kuwa lakini hata kama kweli aliwatukana, hiyo haiwezi kuwafanya kumpiga hadi kumuua. Kama aliwatukana hivyo na wao siyo hivyo, ni kwa nini wakasirike," alihoji Kamanda Kalinga.

Swetu anajulikana zaidi kwenye mambo ya burudani na michezo. Alikuwa akiendesha biashara za burudani, lakini pia alikuwa nahodha wa timu ya soka ya wachezaji wa zamani ya Mango Garden.

Kifo chake kilifanya bonanza la kula Jumapili la timu za wachezaji wa zamani linalofanyika kwenye viwanja wa Klabu ya Leaders lisifanyike hadi Jumapili ijayo.
Tags:

0 comments

Post a Comment