Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CHAMA KIPYA KINACHOHUSISHA VIGOGO WA CCM, UPINZANI CHATINGA KWA MSAJILI WA VYMA VYA SIASA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter



CHAMA KIPYA KINACHOHUSISHA VIGOGO WA CCM, UPINZANI CHATINGA KWA MSAJILI WA VYMA VYA SIASA


WAKATI kukiwa na taarufa za baadhi ya vigogo wa CCM kujiengua, jana Msajili wa Vyama vya Siasa alipokea maombi ya usajili wa Chama Cha Jamii (CCJ), ambacho kinahusishwa na kumeguka kwa chama tawala.

Kuwasilishwa kwa maombi hayo kumekuja wakati hali ya hewa ndani ya CCM ikiwa imechafuka baada ya vita dhidi ya ufisadi kuonekana kuwagawanya vigogo wa chama hicho, huku hali visiwani Zanzibar ikizidi kuwagawa wanachama wa chama hicho tawala.


Wakati baadhi ya vigogo wa CCM wanaonekana kutoridhishwa na hali inayoendelea kwenye chama hicho tawala na kuhusishwa na mipango ya kuunda chama kipya, watu wawili jana walitinga ofisi za msajili wa vyama vya siasa kuwasilisha maombi ya usajili wa chama kipya.

"Ndio, leo walikuja kwangu watu wa Chama cha Jamii na nimepokea maombi yao. Kwa kifupi ni hivyo ukitaka zaidi njoo ofisini kwangu," alisema Msajili John Tendwa alipoulizwa kuhusu kuwasilishwa kwa maombi hayo na watu waliojitambulisha kuwa ni Richard Kiabo, ambaye anakuwa mwenyekiti wa muda na Renatus Muwadi, ambaye ni katibu mkuu wa muda.

Dira na lengo kuu la CCJ ni Ustawi na Hifadhi ya Jamii pamoja na demokrasia, kwa mujibu wa rasimu ya katiba ya chama hicho ambacho makao yake makuu yatakuwa jijini Dar es Salaam, huku ofisi ndogo zikiwa Zanzibar na Dodoma.

Kwa mujibu wa rasimu ya katiba ya CCJ bendera ya chama hicho itakuwa na rangi nne ambazo ni bluu, dhahabu, nyeusi na kijani, rangi ambazo zinapishana kidogo na za bendera ya taifa.

Rasimu hiyo, ambayo gazeti hili tayari limeipata, inafafanua kuwa rangi ya bluu ni ishara ya maji yanayounganisha pande mbili za Muungano yaani Zanzibar na Tanganyika, dhahabu, rasilimali za Tanzania, nyeusi ni watu na kijani ni kilimo, mazingira na uoto.

Imebainisha kuwa itikati ya CCJ ni demokrasia ya kijamii inayozingatia umoja wa taifa, utawala wa katiba na sheria, mgawanyo wa mamlaka ya dola, haki za binadamu, uhuru na ustawi wa jamii.

Aidha, misingi ya kiitikadi na nguzo za CCJ ni utawala wa dola na miiko ya uongozi ambapo imani yake kuu ni kwamba binadamu wote ni sawa, huzaliwa huru na Waafrika ni taifa moja. Pia kinaamini umoja wa Tanzania ni nguzo kuu ya umoja wa taifa la Waafrika na ni moja ya malengo makuu ya dola la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa viongozi hao wa muda wa CCJ wametangulizwa na baadhi ya vigogo kutoka ndani ya CCM ambao wanaandaa mikakati ya kukihama chama hicho katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Habari zinasema kuwa vigogo hao wa CCM, wakiwemo viongozi wa zamani na wabunge, wamekuwa na vikao vya mara kwa mara kujadili mkakati huo na mpango wao wa awali ulikuwa ni kupambana na Rais Jakaya Kikwete ndani ya chama katika uchaguzi wa Oktoba.

Hata hivyo, habari hizo zinadai, ilionekana kuwa vigumu kumshinda Kikwete katika kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais kutokana na kusaliwa na muda mfupi wa kukampeni na ndipo walipoamua kusajili chama kipya.

Inasemakana kuwa baada ya kuvuja kwa mpango wa kuanzisha chama, vigogo hao walitaka kuingia kwenye moja ya vyama vya upinzani, lakini baada ya majadiliano ilibainika kuwa mpango huo unaweza kusababisha matatizo kama ilivyokuwa kwa NCCR Mageuzi.

NCCR, ambayo ilichomoza kwa nguvu na kujipatia wanachama wengi kiasi cha kuitikisa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, nusura isambaratike baada ya wanachama kuanza kumpinga Augustine Mrema aliyepewa uenyekiti na ugombea urais baada ya kujiengua CCM.

Habari zinasema kwamba tofauti na Mrema ambaye alitoka CCM akiwa peke yake, vigogo wa CCM watakuwa na kundi kubwa la vigogo wa CCM.

"Wanaweza kuwako zaidi ya wabunge 20 wa CCM, vilevile, kuna wabunge wa upinzani nao watakuwako katika kundi hilo. Kinachosubiriwa ni muda wa kufanya maamuzi hayo," alisema mtoa habari ambaye ameshiriki kila hatua ya kuanzisha chama hicho.

Habari za ukakika zinadai kuwa CCJ kimeratibiwa kwa karibu na vigogo wa CCM kwa kushirikiana na wanasheria makini.

"Chama hiki kimeanzishwa kutokana na maombi ya wanachama wa CCM, wanachama wa vyama vya upinzani na wananchi," alisema katibu wa CCJ, Muwadi.

"Ni mawazo ya wananchi, wafanyakazi, wastaafu, baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani na chama tawala cha CCM."

Hata hivyo, viongozi hawa wa muda watarajiwa kuwaachia madaraka vigogo hao wa CCM ambao wana ushawishi mkubwa kwa jamii mara watakapotangaza hatua ya kukihama chama tawala.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanatabiri kwamba kuanzishwa kwa CCJ kunaweza kuvuta vyama vingine vya upinzani kama NCCR-Mageuzi, Chadema na hata CUF kwa upande wa Bara na kushirikiana hivyo kutoa changamoto kubwa kwa CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Vilevile, CCJ huenda kikachukua wabunge wengi wa sasa kutoka CCM ambao wanaweza kuangushwa katika kura za maoni, hivyo kikawa na nguvu zaidi.

Ni kwa mantiki hiyo pia wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona nguvu ya vyama vya upinzani vilivyopo sasa kupungua kutokana na uwezekano wa kupoteza wapenzi na wanachama kwa chama hiki kipya.

Vita ndani ya CCM imeonekana kuwa ni kubwa tangu kuibuka kwa kashfa ya Richmond iliyosababisha mgawanyiko mkubwa kuanzia kwa vigogo hadi wanachama wa CCM. Vita hiyo imekuwa ikipiganwa ndani ya chama, Bunge na nje, kiasi kwamba halmashauri kuu iliunda kamati ya watu watatu kujaribu kuondoa tofauti hizo.

Hata hivyo, habari zinasema kuwa kamati hiyo inaonekana kushindwa kuibuka na mapendekezo ya maridhiano yanayoweza kuridhisha pande zote mbili, hali ambayo imesababisha kila kundi kuanza mikakati yake kwa ajili ya Uchaguzi Kuu ujao.

CCM ilikuwa iitishe vikao vyake vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu, lakini ilishindikana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuingiliana kwa ratiba ya vikao hivyo na vile vya Baraza la Wawakilishi.

Hata hivyo, hali si nzuri visiwani Zanzibar ambako urafiki mpya wa Rais Amani Abeid Karume na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Seif Sharrif Hamad unaendelea kukomaa kiasi cha chama hicho kupendekeza mtoto huyo wa muasisi wa taifa la Zanzibar aongezewe muda.

Pendekezo hilo la CUF limeungwa mkono na wanachama wa CCM wanaoonekana kumuunga mkono Karume, huku wapinzani wake wake wakipinga maafikiano hayo na mpango wa kumuongezea muda kiongozi huyo wa SMZ.

Tayari mwakilishi wa CUF ameshawasilisha kwa katibu wa Baraza la Wawakilishi hoja yake binafsi ya kutaka marekebisho ya katiba ili Karume aongezewe muda kuhitimisha kazi aliyoianza ya kuondoa siasa za chuki na kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi, ambao umeelezewa kuwa ndio chanzo cha machafuko visiwani humo.
Tags:

0 comments

Post a Comment