IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MBUNGE wa Mtera ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela, amekanusha kuhusika na Chama Cha Jamii (CCJ), na kusema kuwa ndani ya CCM, haoni mtu yeyote atakayetoka kujiunga na chama hicho.
Amesema yeye yupo kwa ajili ya CCM na ni mwana CCM wa kweli hivyo hatarajii kuona chama hicho tawala kikivunjika kwa kuwa haoni wenye nia kama hiyo ndani ya chama hicho.
Malecela ametoa kauli hiyo jana alipozungumza kwa njia ya simu na Habari Leo Jumapili alipokuwa akijibu swali kuhusu madai ya kuhusishwa kwake kuwa miongoni mwa waasisi chama hicho.
Pamoja na kauli hiyo, katika tukio lingine juzi katika Kijiji cha Muungano, wilayani Chamwino, alitangaza kutatetea kwa mara nyingine kiti chake cha ubunge katika uchaguzi ujao baadae mwaka huu kama akipata ridhaa ya CCM.
Malecela ambaye pia alizungumza na waandishi wa habari kuelezea mambo kadhaa ya siasa ikiwemo kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu ukomo wa ubunge, alikana kupata mwaliko wa kuwa mtoa mada katika Kongamano la kupambana na ufisadi linalodaiwa linatafanyika Dar es Salaam mwezi ujao.
Kongamano hilo linalohusishwa na CCJ, linadaiwa lina lengo la kueneza chama hicho kilichoomba usajili siku chache zilizopita ambacho pia kinahusishwa na vigogo kadhaa ‘wanaopambana na ufisadi’ wanaodaiwa wataihama CCM na kujiunga nacho.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, mkongwe huyo wa siasa nchini alisema “Sina taarifa ya kongamano lolote, narudia tena, sina taarifa wala mwaliko wa kongamano lolote…na mambo yanayoendelea kuhusu chama ni uzushi wa watu wanaotaka kuharibu sifa ya Tanzania, mimi ni mwana CCM na kamwe nitabaki kuwa hivyo.”
Malecela katika mkutano wa juzi alisema: “Hiki chama nimekuwa nikikisikia katika vyombo vya habari, simfahamu kiongozi wake hata mmoja ambaye anatoka katika Chama Cha Mapinduzi na wala siamini kuwa kuna viongozi wa CCM wanataka kuvunja chama kwa ajili ya chama hicho kipya.”
Kuhusu nia yake ya kugombea ubunge tena, Malecela alifafanua kuwa ameamua kugombea tena baada ya wananchi kutoka kata zote za jimbo hilo kumtaka agombee tena.
Malecela alisema kutokana na maombi hayo ameamua kugombea nafasi hiyo ili kuwapa wananchi wake kile ambacho wanakitaka na kuongeza kuwa kila mtu ana haki ya kufanya kile anachoona kinafaa.
“Mimi ni Malecela na Mzindakaya ni Mzindakaya kwa hiyo kama yeye amepumzika siasa mimi wananchi bado wananihitaji nimeshasema kuwa ninagombea na ninarudia kuwa nitagombea”, alisisitiza alipokuwa akijibu swali.
Aidha amemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupeleka rasmi bungeni suala la ukomo wa ubunge ili wabunge watoe maoni yao kama hoja hiyo ni ya Serikali.
Hata hivyo Waziri Mkuu Pinda alisema hayo yalikuwa maoni binafsi kama angeulizwa na mtu na hivyo hayatafikishwa bungeni kwa kuwa haikuwa nia wala sera ya serikali.
Msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa aliliambia gazeti hili jana kuwa CCJ kwake si kitu cha muhimu kuacha shughuli nyingine za taifa na kukifikiria usajili wake na kwamba vipo vyama vingine vilivyopo katika msururu wa kuomba visajiliwe na chenyewe kitafuata baada ya vyama hivyo.
“Wameleta maombi, hata kusoma hatujasoma, kila kukicha nasikia kwenye vyombo vya habari CCJ, CCJ, ni nini CCJ, mimi nasema tunafanya mambo kwa mujibu wa sheria si chama fulani.
“Sasa hivi tuna mabo mengi ya muswada wa Sheria ya Uchaguzi na kanuni, hatufikirii kuhusu usajili,” alisema Tendwa ambaye pia alifafanua kuwa huenda Machi CCJ wakapata usajili wa muda ambao kwa mujibu wa sheria ni wa miezi sita kabla ya wa kudumu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa amewataka vigogo wanaodaiwa kuhusika katika CCJ kujitokeza hadharani kama ni wanaume kweli kweli badala ya kujificha nyuma ya mgogo wa watu wengine.
“Chama kipya! Kwanza sijui ni kina nani, mtu yeyote katika siasa akijificha si jasiri, hawezi kuleta mapinduzi, Mrema (wa TLP) alipotoka CCM alilitangazia taifa, sisi tuliweka mambo hadharani pia, sasa kama ni vigogo dani ya CCM na wana nia njema ya chama hicho (CCJ) na kama kweli ni wanaume, wangejitokeza, tuwatafsiri na kujadili nia yao,” alisema Dk. Slaa.
Akizungumzia uzoefu wake katika vyama vya siasa na endapo ujio wa CCJ utakitikisha CCM na vyama vingine vya upinzani, alisema chama hicho hakitakuwa na mapinduzi yoyote na kuongeza kuwa kinachoiua CCM ni dhana ya ‘huyu si mwenzetu au ni mwenzetu’ iliyomfanya akakihama chama hicho mwaka 1995.
Mkuu wa Idara ya Propaganda ya CCM, Tambwe Hiza, ambaye ana uzoefu wa kuhama hama vyama kutoka NCCR Mageuzi, CUF mpaka CCM, alisema cha hicho tawala kitaendelea kushika hatamu kwa kuwa mfumo wa vyama vya upinzani umejengwa katika misingi mibovu.
Amefafanua kuwa katika vyama hivyo mwenyekiti wa chama ndiye mmiliki wa chama na ndiye mwenye kauli ya mwisho na kwamba wanaotoka CCM, baada ya muda mfupi huporomoka kisiasa kwa kuwa umaarufu upo ndani ya chama na si kwa mtu.
Hata hivyo alisema: “Maisha ndani ya vyama yanafanana kiasi kikubwa, kuna fitina sana, lakini ikumbukwe kuwa fitina si ya chama bali wanachama, sehemu yoyote yenye watu wenye utashi, fitina ni lazima, kama vile hivi sasa watu watagombea nafasi mbalimbali kupitia vyama vyao, lazima wafitiniane na uchaguzi ukiisha, fitina nayo inakoma.”
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba yeye alisema kuwa CCM haitishwi na CCJ hata kidogo na kwamba anayetaka kutoka na kujiunga na chama hicho aende tu kwani akifika huko baada ya muda, ataporomoka na kusahahulika kwa kuwa chama hicho hakina ubavu wa kufurukuta mbele ya chama tawala.
You Are Here: Home - - Malecela akana kuasisi CCJ
0 comments