Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambaye ameutangaza mwaka 2010 kuwa mgumu kwa mafisadi na kuongeza kuwa kuwa watavuna walichopanda |
MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ameutangaza mwaka 2010 kuwa mgumu kwa mafisadi, na hasa kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba.
Kilango alisema hayo wakati akipokea msaada wa Sh2 milioni uliotolewa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa ajili ya kusaidia watu waliokumbwa na maporomoka ya kifusi yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana wilayani Same, Kilimanjaro.
Mbunge huyo, ambaye ni kati ya wanachama wa CCM wanaojipambanua kuwa ni makamanda wa vita ya ufisadi, alikuwa kimya kwa muda mrefu tangu wakati wa mkutano baina ya wabunge wa chama hicho na kamati iliyoundwa kutafuta chanzo cha kuharibika kwa uhusiano baina ya wabunge na viongozi wa CCM kilichofanyika Dodoma.
Katika mkutano huo ambao wachunguzi wanaona kuwa ulitumiwa na watuhumiwa wa ufisadi kujibu makombora wanayorushiwa hadharani, Kilango alimwagiwa tuhuma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba kuwa yeye na mumewe, John Malecela pia walifadhiliwa kwa fedha za kifisadi wakati wa harusi yao na kwamba anajihusisha na biashara haramu.
Kilango hakujibu tuhuma hizo na aliibuka kwa kipindi kifupi wakati wananchi wa jimbo lake walipoangukiwa na kifusi cha mlima, na kueleza ubaya wa ufisadi kabla ya kutulia tena.
Jana Kilango, ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya chama tawala, alianza mwaka kwa kuendeleza vita hiyo dhidi ya ufisadi wakati alipotuma salamu za kwanza kwa watuhumiwa hao, akisema CCM haitakuwa na wakati mgumu katika uchaguzi huo bali mafisadi ndio watakaovuna walichopanda.
Kilango, ambaye alikuwa akijibu swali kuhusu mtazamo wa CCM kukabiliwa na hali ngumu katika uchaguzi huo kutokana na kutuhumiwa kukumbatia wanachama wenye kashfa za ufisadi ikiwemo Richmond, alisema:
"Sioni kama CCM inaweza kuwa na wakati mgumu, bali wale ambao wamepata fedha kwa njia ya ufisadi ndiyo watakaokabiliwa na hali ngumu. Ukisema chama si sahihi mbona hata vyama vingine kuna malalamiko ya kuliwa ruzuku."
Kilango alisema wananchi wanajua mbivu na mbichi, hivyo kila mtu mwenye tuhuma za ufisadi atapaswa kueleza alichokifanya.
"Kama mtu kajipatia fedha kwa njia chafu, wananchi wanajua na wataamua cha kufanya. CCM ni chama chenye wanachama milioni nne hivyo wale wenye matatizo yao ya ufisadi, ndiyo watakuwa katika hali hiyo ngumu," alisisitiza.
Mbunge huyo, ambaye alitunukiwa tuzo ya mwanamke shujaa na taasisi moja ya Marekani, alikitetea chama dhidi ya tuhuma za kushindwa kuchukulia hatua watuhumiwa wa kashfa ya Richmond, akisema: "CCM haijashindwa, usiihukumu."
"Mbona kuna watu kama wa (watuhumiwa wa wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje ndani ya Benki Kuu-BoT) EPA, tayari wamefikishwa mahakamani?"
Ingawa Kilango anataja watuhumiwa wa EPA, lakini hadi sasa kumbukumbu zinaonyesha kigogo pekee aliyefikishwa mahakamani ni mfanyabiashara maarufu, Jeetu Patel, lakini wananchi bado wanaona kuwa bado wahusika wengi wameachwa wakitamba mitaani, wakiwemo vigogo wa kampuni ya Kagoda Agriculture.
Kilango alisema ni mapema kukihukumu chama kwamba kimeshindwa kuwatoa nje ya nafasi zao vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi na kwamba "bado kuna Kamati ya Mzee Mwinyi haijamaliza kazi yake".
"Hapa tulipo bado tunasubiri matokeo ya Kamati ya Mwinyi... ilifanya kazi yake, lakini haijatoa mapendekezo yoyote, sasa huwezi kuhukumu kwamba CCM imeshindwa kuwaengua mafisadi."
Hata hivyo, Kilango alionya awali kwamba mwaka huu wa uchaguzi Watanzania wanapaswa kuwa makini na siasa chafu na za kichochezi ambazo zinaweza kulenga kuivuruga nchi.
Alisema anaamini Watanzania ni watu makini ambao wanaweza kuchekecha pumba na mchele huku akisisitiza kwamba, wanapaswa kukataa kulishwa habari zinazoweza kuivuruga nchi.
Katika mkutano huo na waandishi uliofanyika nyumbani kwake Sea View, Kilango pia alikanusha taarifa kwamba kuna michango ya maafa ambayo imeliwa au kutowafikia waathirika wa maporomoko ya ardhi jimboni kwake.
Mbunge huyo alisema taarifa hizo ni za upotoshaji ambazo hazina ukweli na zinazolenga kuchafua jitihada za serikali na wadau katika kusaidia waathirika.
Akipokea msaada huo na mingine iliyotolewa na wadau wengine, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, imekuwa ikiwafikia walengwa.
Alifafanua kwamba zipo kamati mbili; moja ambayo iko chini yake na vijiji viwili vilivyoathirika na ile inayoongozwa na mkuu wa Wilaya ya Same na kwamba michango inayotolewa inakwenda vizuri kupitia kamati zote mbili.
0 comments