SIKU moja baada ya naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kusisitiza kuwa ataendelea kumsaidia rafiki yake David Kafulila ili atwae ubunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, chama chake kimesema kauli hiyo ni nzito, tata, itajadiliwa na kutolewa maamuzi mazito.
Zitto pia alisema haridhiki na uamuzi wa chama chake kuwaengua Kafulila, ambaye alikuwa ofisa habari wa Chadema, na Danda Juju, aliyekuwa anashughulikia masuala ya Bunge, walienguliwa nyadhifa zao na Dk Willibrod Slaa ambaye kwa wadhifa wake wa katibu mkuu ndiye anayeongoza sekretarieti ya chama hicho.
Dk Slaa alimuelezea Kafulila kuwa ni kama sisimizi na kusisitiza kuwa watendaji hao, si kitu ndani ya Chadema na anaweza kuwashughulikia bila vikao vya chama.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC1, Zitto alisema ameamua kuweka hadharani mambo hayo kwa sababu hapendi siasa za kinafiki, jambo ambalo limeishtua Chadema na kuahidi kukaa ili kujadili, kutafakari na kutoa maamuzi dhidi ya kauli za Zitto.
Lakini jana, mjumbe wa baraza la wazee wa chama hicho, Bob Makani aliliambia gazeti hili kuwa Chadema itakutana ili kutafakari na kujadili kauli hiyo ya Zitto.
"Kauli ya Zitto kwamba ataendelea kumsaidia Kafulila kadri ya uwezo wake, ina utata... ina utata kwa sababu kina Kafulila walienguliwa nyadhifa zao ndani ya Chadema, wakaamua kuhamia chama kingine," alisema Makani.
"Sasa inapotokea 'a senior leader' (kiongozi mwandamizi) ndani ya chama anatangaza hadharani kwamba ataendelea kuwasaidia, inaleta utata... ni jambo zito linalohitaji tafakuri ndani ya chama chetu."
Makani, ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa Chadema, alisema akisisitiza kuwa kutokana na hali hiyo chama chake kitakaa ili kutafakari kabla ya kutoa maamuzi ya kumuita na kuzungumza naye au vinginevyo.
"Chama kitakaa ili kutafakari na kutoa maamuzi juu ya Zitto, kumuita na kuzungumza naye au maamuzi mengine ambayo chama kitaona yanafaa," alisema Makani ambaye pia ni wakili maarufu nchini.
Makani, ambaye ni miongoni mwa wazee waliomshawishi Zitto kuengua jina lake katika kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chadema ili kumpisha Freeman Mbowe kuwa mgombea pekee, alisema ni tatizo la msingi kwa kiongozi wa juu wa chama kusaidia chama kingine.
"Haiwezekani kiongozi wa chama kuamua kumsaidia kiongozi au mtu wa chama kingine pinzani katika harakati za kisiasa,"alisema Makani.
Kuhusu uwezekano wa kuwajibishwa na chama kutokana na mwenendo wake, Zitto alisema siasa haikuwa chaguo lake la kwanza na kudai kuwa ameshaandika barua nyingi za kuacha siasa, lakini amekuwa haziwasilishi kunakohusika. Lakini Makani alisema Zitto ndiye mwenye haki ya kuamua kubaki au kung’atuka kwenye siasa kwa sababu hayo ni maisha yake mwenyewe. "
Siasa ni maisha yake mwenyewe kwa hiyo yeye ndie mwenye uamuzi wa kubaki au kung'atuka kwenye siasa," alisema Makani ambaye alimuachia Mbowe uenyekiti wa Chadema.
Kuhusu kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Chadema kuwaengua kina Kafulila, Makani alisema Zitto ana haki ya kutoa maoni yake kidemokrasia dhidi ya uamuzi huo.
"Lakini ndani ya chama kuna ‘procedures’ (taratibu) za kulalamika ikiwa ni pamoja na kukata rufaa. Hata hivyo wa kulalamika ni kina Kafulila ambao ndio walioenguliwa na si Zitto ambaye ni kiongozi wa juu wa chama," alisema Makani.
Awali Dk Slaa aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu ajenda hiyo imeshafungwa.
"Nimesema sina kauli yoyote ya kusema na nimeshafunga ajenda hizo na sizihitaji. Nilisema nyinyi mna ajenda zenu," alisema Dk Slaa kwa sauti ya juu.
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei hawakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) Dk Benson Bana alisema anapoibuka kiongozi mkubwa ndani ya taasisi na kutoa kauli kama za Zitto, tafsiri yake ni kwamba amani hamna ndani ya taasisi hiyo.
"Kutokana na kauli za Zitto sisi watu wa nje tafsiri yetu ni kwamba ndani ya Chadema mambo si shwari na hakuna amani,"alisema Dk Bana ambaye pia ni mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa cha chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema Zitto ni kiongozi mzuri na bado anastahili kuwa kiongozi kwa sababu ya uwezo wake wa kujenga na kusimamia hoja hasa anapokuwa bungeni na katika vikao vya kamati ya kudumu ya mahesabu ya mashirika ya umma ni mkubwa.
"Uongozi kwa Zitto ni stahili yake kwa sababu ana uwezo wa kuongoza kwa kujenga na kusimamia hoja. Anapokuwa bungeni anasisimua kwa jinsi anavyojenga hoja mbele ya wabunge na Watanzania," alisema Dk Bana. Alisema Zitto ni mwalimu mzuri na anaweza sana kuwasaidia vijana wetu katika fani ya uchumi, kwa sababu shule zetu zina upungufu mkubwa wa walimu.
"Cha msingi Zitto awe na msimamo, atafute ushauri na baadaye afanye maamuzi, sisi tunapenda abakie katika siasa lakini yeye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho,"alishauri Dk Bana.
"Ni wakati mwafaka wa kuchukua uamuzi na anayo haki na nafasi nzuri ya kufanya hivyo kwa sababu yeye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho."
Aliwataka wazee wa Chadema na viongozi wake wa juu, kukaa pamoja na Zitto ili kumaliza matatizo yaliyopo baina yao na kukifanya chama kiweze kunawiri katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
0 comments