IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SHINIKIZO lililokuwa likitolewa na Chama cha Wananchi (CUF), kutaka Katiba ya Zanzibar ivunjwe ili Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume aongezewe muda wa kuongoza limegonga ukuta baada ya Rais Karume kuikataa hoja hiyo na kuwasihi Wazanzibari wote kumuunga mkono katika hilo.
Aidha shinikizo lingine la kutaka kuundwe kwa serikali ya mseto Zanzibar limekubaliwa, lakini limetakiwa kufuata azimio la Butiama la kutaka uamuzi huo ufanyike baada ya kuamuliwa na Wazanzibari wenyewe kupitia kura ya maoni.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Salehe Ramadhan Ferouz, alitoa msimamo huo jana baada ya kumalizika kwa kikao cha wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoka Zanzibar kilichojadili hoja kubwa tatu zinazohusu mustakabali wa Zanzibar kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Karume.
Katika ajenda ya kwanza ya kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Dk. Ali Mohamed Shein, Rais Karume alitakiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu yaliyozungumzwa katika kikao chake na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika majadiliano hayo, Rais Karume aliweka bayana kuwa Seif ndiye aliyemfuata kutaka mazungumzo naye na walizungumza masuala ya kujenga umoja wa Wazanzibari, kuacha siasa za chuki na kujenga Zanzibar mpya ambapo wajumbe walipokea vyema taarifa hiyo.
Ajenda ya pili ya kikao hicho kilichoanza saa nane mchana na kukamilika saa moja usiku, ilihusu zilizoitwa kuwa ni tetesi za kutaka Katiba ya Zanzibar ivunjwe ili Rais Karume aongezewe muda wa kuongoza baada ya kumalizika kwa kipindi chake cha pili cha uongozi ambacho kwa mujibu wa katiba hiyo, alitakiwa kupumzika.
Rais Karume alisisitiza wakati wa kujadili ajenda hiyo kuwa msimamo wake ni kama alivyoutangaza wakati wa sherehe za miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuweka msisitizo kuwa hataki kuongezwa hata siku moja.
Aidha Karume aliwasihi Wazanzibari wote ambao walikuwa wakishinikizwa na kushawishiwa na CUF kupitia makongamano na maandamano, kumuelewa kuwa asingependelea kuongezewa hata siku moja ya Urais baada ya muda wake kikatiba kumalizika.
Ajenda ya tatu ambayo imeelezwa kuwa ilichukua muda mrefu kidogo, ni iliyohusu kuundwa kwa Serikali ya mseto. Katika kujadili ajenda hiyo, wajumbe walikubaliana kutoingia kwa undani zaidi kuwa kambi ya upinzani inaiandaa kwa ajili ya kuifikisha katika Baraza la Wawakilishi ili ijadiliwe kwa kina.
Hata hivyo, ilibidi wakumbushiane maazimio ya mkutano wa NEC ya CCM uliofanyika Butiama mwaka 2008 ambayo yalitaka wananchi wa Zanzibar waamue kuhusu uundwaji wa serikali hiyo kupitia kura za maoni jambo ambalo pia lilikubaliwa.
You Are Here: Home - - CUF wagonga mwamba
0 comments