Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) John Chiligati ambaye amedai kuwa Chama Cha Jamii (CCJ) hakina jipya hivyo wananchi wanatakiwa kukipuuza |
KAULI za viongozi wa CCM kuhusu kuanzishwa kwa chama kipya cha kisiasa, CCJ, zinaonekana kupuuza nguvu yake, lakini jinamizi chama hicho linaonekana bado linasumbua usingizi wa viongozi hao.
Tayari makamu mwenyekiti wa CCM, Pis Msekwa, katibu Yusuf Makamba, katibu wa itikadi na uenezi, John Chiligati, spika wa Bunge, Samuel Sitta na mkuu wa kitengo cha propaganda na uenezi, Tambwe Hiza wameshatoa kauli zinazoonyesha chama tawala hakihofii kuanzishwa kwa CCJ na kwamba wanachama watakaojiunga watakuwa wamepoteza mwelekeo.
Lakini kauli hizo zinaonekana hazitoshi na jana Chiligati alilazimika kutoa tamko, safari hii likionekana kuwatahadharisha wanachama wake wasijiunge na CCJ, ambayo kirefu chake ni Chama cha Jamii akisema "watakaojiunga nacho, watakuwa wameamua kusafiria chombo kilichotoboka na kupoteza umaarufu wao".
"Nimelazimika kusema jambo hilo ambalo nahisi kuwa linakuwa ni tabu sasa na linaleta migongano kwa jamii hasa ya wananchi walioko huko vijijini," alisema Chiligati.
"Wanachama wetu wa mikoani na vijijini hawajui nini kinaendelea, hivyo wanaposikia katika magazeti tu, wanadhani kuwa chama hicho ni kizuri hivyo ndio maana nimeamua kutoa tamko hilo rasmi na kuwataka wanachama wa CCM watulie."
Chiligati alisema CCJ, ambayo inadaiwa kuwa na uhusiano na baadhi ya vigogo wa CCM na wabunge, ni chama cha magazetini ambacho hata kikifanya miujiza, hakitaweza kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Chiligati alisisitiza tena kuwa CCM, ambayo ilitingishwa wakati waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Augustine Mrema alipojiondoa na kujiunga na upinzani mwaka 1995, haitameguka kwa sababu ya usajili wa CCJ, kwa kuwa chama hicho tawala kinakubaliwa na zaidi ya Watanzania milioni 4.4.
"Watanzania wengi wana imani na CCM na hata hawakuwa tayari kuukubali mfumo wa vyama vya vingi ulipoingia lakini, serikali ilitumia busara tu kuruhusu mfumo huo kwa kukubaliana na asilimia 20 iliyouunga mkono." alisema Chiligati.
Kauli ya Chiligati imekuja siku moja baada ya kikao cha wabunge wa CCM ambao walikutana juzi usiku katika bungeni mjini hapa.
Awali taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa moja ya agenda ya kikao hicho ilikuwa kujadili namna chama hicho kinavyokuja kwa kasi na jinsi ya kuwabaini wabunge wanaoelezwa kuwa wanahusika na chama hicho.
Hata hivyo, baadaye Chiligati alikanusha suala hilo kuwa miongoni mwa ajenda za kikao hicho juzi.
"Sisi hatukuzungumza juu ya CCJ, isipokuwa nimetoa kauli yangu hiyo kwa kuwa ni msemaji wa CCM na hiyo ni moja ya shughuli zangu," alisema Chiligati.
Lakini akatoa kauli inayoonekana kusifu viongozi wa CCM kuwa ni wenye akili timamu na hivyo hawawezi kujiondoa na kwenda kujiunga na CCJ.
"Viongozi wa CCM ni imara na wana akili sana hivyo siamini kama kuna kiongozi mwenye akili timamu ambaye atapenda kujiunga na chama hicho ambacho bado hakina hata mwelekeo wowote ili hali akijua kuwa chama hicho hakitaweza kushiriki uchaguzi wa mwaka huu," alisisitiza Chiligati.
"Hivyo taarifa kuwa kuna vigogo wengi wa CCM wataomba uteuzi wa urais na ubunge kupitia chama hicho ni sawa na kuingia katika boti iliyotoboka na kutaka kusafiri nayo baharini.
"Bunge linavunjwa mwezi Julai na wakati huo uteuzi wa wagombea utakuwa ukianza, sasa ni muda gani huo kwa kigogo wa CCM kuhama na kujiunga na CCJ," alihoji na kuongeza kuwa CCJ itafanya maajabu sana kufanikiwa kupata usajili kabla ya uchaguzi.
Wakati huohuo, kamati ya wabunge wa CCM ilikutana juzi usiku katika kikao cha faragha kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, huku taarifa zikieleza kuwa mvutano mkubwa uliibuka baina ya wajumbe.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya mkutano vinasema mvutano huo uliibuka wakati wa kujadili hoja ya marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta wa mwaka 2009.
Kwa mujibu wa habari wakati wa kujadili hoja hiyo liliibuka kundi la wabunge na kupinga kipengele kinacholazimisha makampuni ya simu kujiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), na kuuza hisa kwa Watanzania.
Mvutano ulidumu kwa muda kabla ya kuzimwa na kiongozi wa mkutano huo na makubaliano kufikiwa kuwa kipengele kinacholazimisha kampuni za simu kujiunga na DSE kiwepo.
Kwa mujibu wa muswada huo kampuni za simu zitalazimika kujisajili katika Soko la Hisa Dar es Salaam na kuuza hisa zake kwa Watanzania, hatua inayoelezwa kuwa itaweka wazi mapato makubwa ya kampuni hizo ambayo hayawekwi wazi.
Muswada huo uliwasilishwa jana bungeni na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla. Mbunge wa Nkasi, Ponsiani Nyami aliwatuhumu baadhi ya wabunge bila kutaja majina kuwa wamepokea fedha kutoka kampuni za simu ili wazitetee na kupinga zisijiunge na DSE.
Nyami alitoa tuhuma hizo alipokuwa akichangia muswada huo. Alisema:" Kampuni za simu zinapata mabilioni ya fedha, hazilipi kodi na zimejitahidi hata kuongea na baadhi ya wabunge wazitetee zisijiunge na DSE.
"Sasa watazengeaje wabunge wawatetee bila kuwapa pesa; wanaogopa wanajua Watanzania watafaidi, lakini hatuna haja ya kuogopa; wasajili DSE; wauze hisa kwa Watanzania na walipe kodi."
Lakini tofauti na vikao vingine, wabunge wengi hawakutaka kuzunguzia wala kudokeza yaliyojiri ndani ya kikao hicho huku badhi yao wakieleza kuwa iwapo watatoa kilichojadiliwa na kikao hicho, na kuandikwa gazetini, usalama wao na waandishi ungekuwa hatarini.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi juzi usiku baada ya kiako hicho kilichoanza saa 11:30 jioni na kumalizika saa 2:30 usiku, umebaini kuwa juzi mchana kabla ya kikao hicho Waziri mkuu Mizengo Pinda alikutana na kuteta na mtangulizi wake Edward Lowassa. Haikufahamika mara moja walizungumza nini.
Baada ya mazungumzo hayo, Pinda na Lowassa walirejea kwenye ukumbi wa Bunge na waziri akaenda karibu na mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru na kuteta naye kwa takriban dakika 15 na baadaye kurejea kwenye nafasi yake.
0 comments